HATIMAYE staa wa sanaa za maigizo Bongo, marehemu Said Ngamba ‘Mzee Small’ amezikwa juzi Jumatatu katika Makaburi ya Segerea jijini Dar es Salaam, Risasi Mchanganyiko lilikuwepo msibani hatua kwa hatua.
Msiba huo ulihudhuriwa na mamia ya watu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Kikwete na ujumbe wake kutoka Ikulu, mastaa mbalimbali na wadau wengine wa filamu.
BONGO MUVI WAJITOKEZA
Awali, ilionekana kuwepo harufu ya wasanii wa Bongo Movies Unity kutohudhuria baada ya kutoonekana msibani hapo tangu siku ya msiba na mkesha wa kuamkia siku ya mazishi.
Wasanii walioonekana mstari wa mbele walikuwa ni wale wa vichekesho wakiongozwa na Habib Mrisho ‘Sumaku’, Hemed Maliyaga ‘Mkwere’, Jumanne Shabaan ‘Matata’ na wengineo huku wasanii wa filamu wakiwa wa kuhesabu.
Mpaka Jumapili usiku, wasanii wa filamu walioonekana nyumbani kwa marehemu Mzee Small walikuwa ni Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Wastara Juma na Simon Mwakifwamba ambaye ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’.
MASTAA WAMGOMBEA JK
Rais Kikwete aliingia msibani hapo na kulakiwa na mwenyeji wake, Rais wa TAFF, Mwakifwamba kisha kusalimiana na watu waliokuwepo msibani ambapo wasanii walionekana kumgombea JK ili washikane naye mkono.
Akizungumza baada ya kushikana mkono na JK, mmoja wa wasanii wa Bongo Muvi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema: “Ni bahati ya mtende kushikana mkono na rais ndiyo maana hakuna aliyekuwa tayari kuipoteza.”
WAKONGWE
Mbali na mzee Olotu, wakongwe wengine walioonekana msibani hapo ni pamoja na Mashaka, Mbembe, Mohammed Fungafunga ‘Jengua’, Fatuma Makongoro ‘Bi. Mwenda’, Hashim Kambi ‘Ramsey’ na wengine wengi.
Timu ya Risasi Mchanganyiko inatoa pole kwa wafiwa wote, ndugu jamaa na marafiki. Mungu awape wepesi katika kipindi hiki kigumu cha mpito. Inshaalah!
Innalillah Wain illah Rajiun.
0 comments:
Post a Comment