\Serikali imepandisha maradufu ada kwa wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vya ualimu nchini kuanzia muhula ujao wa masomo.
Ada hizo
kwa wale wa ngazi za cheti na stashahada ambazo zimeongezwa kwa karibu
mara mbili au zaidi ya zile zilizokuwa zikilipwa awali. Uamuzi huo ambao
huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi ambao waliona ualimu kama kimbilio,
unaelezwa na baadhi ya wadau wakiwamo walimu, wanafunzi na hata
wakufunzi wa baadhi ya vyuo nchini kuwa ni wa ghafla.
Kwa
mujibu wa baadhi ya wakufunzi, uamuzi huo umetolewa kupitia waraka wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na unatarajiwa kuanza kutekelezwa
muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai 2, mwaka huu.
Kabla ya
kupandishwa kwa ada hizo, wanafunzi wanaosomea ualimu kwa ngazi ya cheti
walikuwa wakilipa Sh200,000, lakini sasa watalazimika kulipa Sh300,000,
ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.
Kwa wale
wanaochukua stashahada watalazimika kulipa Sh400,000 kwa masomo ya Sanaa
na Sh600,000 kwa masomo ya Sayansi kutoka Sh200, 000 za awali.
Mhasibu
wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara, aliyekataa kutaja jina lake kwa kuwa siyo
msemaji wa chuo hicho, alithibitisha kupokea waraka wa Serikali
unaowataka kupandisha ada, lakini alisisitiza kuwa Mkuu wa Chuo ndiye
angeweza kufafanua zaidi kuhusu ongezeko hilo.
"Taarifa
hizo ni za kweli ada imepanda, kama umezipata kutoka wizarani hivyo
ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu ya kupata taarifa zaidi kutoka
kwetu," alisema mhasibu huyo.
Awali,
habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Serikali imefikia uamuzi
huo kutokana na uhaba wa fedha na ugumu wa kuviendesha vyuo hivyo.
Habari
zinasema kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikidaiwa na wazabuni
fedha nyingi, jambo ambalo limeathiri pia uendeshaji wa vyuo vikiwamo
vya ualimu.
Baadhi ya
wakufunzi wameeleza kuwa fedha za ada sehemu yake itatumika kutatua
matatizo ya uhaba wa fedha ambao umekuwa ukiwakabili na hivyo kuathiri
utoaji wa huduma zikiwamo za vyakula.
Wizara ya Elimu
Msemaji
wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema viwango
vilivyoongezwa siyo vikubwa ikilinganishwa na hali ya ugumu wa maisha
ilivyo sasa nchini.
"Unamweka
mtu mwaka mzima anakula, analala, anasoma...kweli unaona hiyo ada hiyo
ni kubwa? Bado siyo kubwa kiasi cha kushtua watu," alisema Bunyazu.
Aidha,
Bunyazu alisema kuwa wanafunzi watakaopata daraja la kwanza katika
masomo ya Sayansi na Hisabati na kuingia katika vyuo vya ualimu vya
Serikali watasomeshwa bure na wale watakaopata daraja la pili na la tatu
watapewa mkopo.
Wengine wazungumza
Meneja wa
Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika la HakiElimu, Godfrey
Boniventura akizungumzia suala hilo jana, alisema kuwa siyo kweli kwamba
serikali haina fedha za kutosha ndiyo maana inaongeza ada, ila inadhani
kuwa idadi ya walimu waliopo inatosha.
"Serikali
imeamua kupandisha ada kwa kudhani kuwa walimu waliopo wanatosha,
lakini ikumbuke kuwa kuna walimu wengi wazee wanaostaafu kila mwaka,
wengine hawaripoti shuleni, hivyo tunahitaji kuwa na benki ya walimu,"
alisema Boniventura.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment