Wednesday, 26 August 2026

MICHEZO KWA WATUMISHI WA HALMASHAURI ITUMIKE KUIMARISHA AFYA, MSHIKAMANO, TIJA KIUTENDAJI - PRO. SHEMDOE

Na: OWM – TAMISEMI, Mbeya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka Halmashauri zote nchini kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha afya, ustawi, mshikamano na tija kwa watumishi, ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. 

Prof. Shemdoe ametoa wito huo Agosti 23, 2026 jijini Mbeya wakati akifungua rasmi Mashindano ya Michezo ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA), kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyarejesha tena mashindano ya SHIMISEMITA mwaka 2023 baada ya  kusitishwa, akitambua kwamba michezo ni sehemu muhimu ya kujenga afya ya mwili na akili, kuimarisha mahusiano kazini na kukuza ushirikiano miongoni mwa watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali nchini.

 “Leo hii mmekutana watumishi zaidi ya 5,000 kutoka katika Halmashauri 177. Kila mmoja anao wajibu wa kujenga mahusiano mazuri na watumishi wa Halmashauri nyingine, kwani michezo ni afya, michezo ni kiunganishi. Hivyo, tumieni fursa hii kujenga afya zenu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu,” amesema.

Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha ushiriki wa michezo unawahusisha watumishi kutoka maeneo mbalimbali, badala ya watumishi wa Makao Makuu pekee. Amesema watumishi kutoka ngazi za kata, vijiji na vitongoji wanapaswa kupewa fursa ya kushiriki, kwa kuwa michezo itawajengea ari na morali ya kutekeleza majukumu yao, ikiwemo ukusanyaji wa mapato, ikizingatiwa kuwa mtumishi mwenye afya njema ya mwili na akili atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amezitaka Halmashauri kuwaandaa na kuwajengea uwezo wananchi kutumia fursa zitakazotokana na Mashindano ya Soka kwa Timu za Taifa Barani Afrika (AFCON 2027). Amesema mashindano hayo si suala la michezo pekee, bali yatatoa fursa za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na hususan katika sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuiingizia Tanzania fedha za kigeni.

Kutokana na umuhimu wa michezo kwa afya na utendaji wa watumishi wa umma, Prof. Shemdoe amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha michezo ya SHIMISEMITA inawekewa kifungu katika bajeti zao na kutengewa fedha ili kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu. Amesema uwekezaji katika michezo ni uwekezaji katika afya ya mwili na akili za watumishi, jambo litakalosaidia kuongeza morali, ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuyaleta mashindano ya SHIMISEMITA mkoani Mbeya, na kuahidi kuwa uongozi wa mkoa umejipanga kuhakikisha usalama na ustawi wa wanamichezo wote wakati wa mashindano hayo. Aidha, Mhe. Malisa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia mashindano ya SHIMISEMITA kuendelea kufanyika nchini.

Naye, Katibu Mkuu wa SHIMISEMITA, Bw. Henry Kapella, ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, ikiwa mlezi wa SHIMISEMITA, kuendelea kuzihimiza Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha watumishi kushiriki mashindano hayo kila mwaka. Ameshauri pia TAMISEMI kuweka kigezo cha uwepo wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya michezo ya SHIMISEMITA katika mchakato wa kupitisha bajeti za Halmashauri, ili kuhakikisha watumishi wanapata fursa endelevu ya kushiriki michezo.

Mashindano ya SHIMISEMITA mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Tuko Tayari kwa AFCON 2027,” ikiwa ni ujumbe unaosisitiza utayari wa Tanzania kutumia fursa za michezo, kuimarisha afya na mshikamano wa watumishi, pamoja na kunufaika na fursa za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiutalii zitakazotokana na AFCON 2027.
Share:

TUME YA MADINI YATOA SIKU 30 KUREKEBISHA MAPUNGUFU KATIKA MIRADI YA UCHIMBAJI MDOGO


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Tume ya Madini imewapa siku 30 wamiliki na wawezeshaji wa miradi ya uchimbaji mdogo yenye Mikataba ya Msaada wa Kiufundi kurekebisha mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi, ikionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza matakwa ya sheria watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa ridhaa za Msaada wa Kiufundi.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Tume kukagua miradi 128 ya uchimbaji mdogo, ambapo miradi 42 ilibainika kutofanya kazi, huku mingine 86 ikiendelea na shughuli za uchimbaji lakini ikiwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli na uzingatiaji wa masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi.

Akizungumza jijini Dodoma leo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amesema wamiliki wa miradi 42 iliyobainika kutofanya kazi wamepewa Hati za Makosa zenye muda wa siku 30 ili kutoa mrejesho wa hatua walizochukua kurejesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na masharti ya ridhaa za Msaada wa Kiufundi.

Amesema ukaguzi huo ulifanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, yaliyotolewa Aprili 27, 2026, wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa mujibu wa Mhandisi Lwamo, ukaguzi umebaini miongoni mwa changamoto katika miradi inayofanya kazi kuwa ni kutotekelezwa ipasavyo kwa mipango inayotakiwa kisheria, ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa Mazingira ulioidhinishwa, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia, Mpango wa Uchimbaji na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi.

Aidha, amesema wamiliki wa miradi 86 inayofanya kazi lakini yenye mapungufu, pamoja na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi, wanatakiwa kurekebisha kasoro hizo ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025.

“Endapo wahusika wa miradi hiyo watashindwa kutekeleza matakwa yaliyowekwa ndani ya muda huo, Tume ya Madini itachukua hatua zaidi za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi,” amesema Mhandisi Lwamo.

Amesema Tume itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika miradi inayotekelezwa kupitia Msaada wa Kiufundi ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Madini, kanuni zake na masharti ya ridhaa zilizotolewa.

Wakati huo huo, Mhandisi Lwamo amewataka wanufaika wa Msaada wa Kiufundi pamoja na wachimbaji wadogo kuendelea kuzingatia matakwa ya utunzaji wa mazingira, usalama na afya mahali pa kazi.

Amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari zaidi katika shughuli za uchimbaji, hususan katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mvua za El Niño, ili kulinda usalama wa wachimbaji, mali na mazingira yanayozunguka maeneo ya migodi.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya uchimbaji mdogo, kuhakikisha Msaada wa Kiufundi unatolewa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, sambamba na kuongeza tija, usalama na uendelevu wa shughuli za uchimbaji madini nchini.
Share:

Tuesday, 25 August 2026

WMA YASHIRIKI TANZANITE MARATHON MANYARA, YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO


📍“Tukimbie kwa Afya, Tupime kwa Usahihi!”

📍"Afya Bora, Vipimo Sahihi, Maendeleo Endelevu!”

📍"Tupime Sahihi, Tulinde Afya, Tujenge Taifa!”

Na WMA - Manyara

Wakala wa Vipimo (WMA) imeshiriki katika mbio za hisani za Manyara Tanzanite Marathon zilizofanyika mjini Babati mkoani Manyara tarehe 22 Agosti, 2026, ambapo watumishi wa Wakala walishiriki mbio za kilomita 5 na 10.

Ushiriki wa WMA katika mbio hizo ulikuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Wakala na Mkoa wa Manyara, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya njema na matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mgeni rasmi katika mbio hizo alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Baran Sillo, akimwakilisha Waziri Mkuu. Mhe. Sillo aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Manyara kwa ubunifu wa kuanzisha mbio hizo, akieleza kuwa tukio hilo lina umuhimu katika kuhamasisha jamii na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga na watoto njiti.

Katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alieleza kufurahishwa na ushirikiano kati ya WMA na Mkoa wa Manyara, akisisitiza kuwa vipimo sahihi vina umuhimu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Mhe. Sendiga alisema vipimo sahihi si muhimu katika shughuli za biashara pekee, bali afya njema na pia ni kipimo sahihi cha utekelezaji wa majukumu yetu kwa ufanisi na kufikia Dira ya Taifa ya  Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Manyara Bw. Dennis Misango aliwahimiza wananchi na wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi katika shughuli zao, akieleza kuwa kufanya hivyo ni muhimu katika kumlinda mlaji na muuzaji.

Alisema matumizi ya vipimo sahihi yanasaidia kujenga uaminifu, usawa na haki katika shughuli za kibiashara, huku yakihakikisha kuwa maslahi ya mlaji na muuzaji yanalindwa.

Manyara Tanzanite Marathon 2026 imefanyika ikiwa na kaulimbiu “Hatua Moja, Okoa Maisha ya Mtoto Njiti”, ikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi na uwezeshaji wa wodi maalum ya kuwahudumia watoto njiti.

Akihitimisha tukio hilo, Mhe. Queen Sendiga aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuchangia kufanikisha mbio hizo, akisema mafanikio ya tukio hilo yametokana na ushirikiano wa Serikali, taasisi mbalimbali, wafanyabiashara, wanariadha na wananchi.

Mhe. Sendiga aliwashukuru pia washiriki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Manyara kwa kujitokeza kwa wingi, akisema ushiriki wao umeongeza hamasa na kuonesha nguvu ya mshikamano wa jamii katika kuchangia maendeleo, hususan kuboresha huduma za afya kwa watoto njiti.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa wa Manyara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha dhamira ya kuimarisha huduma za afya inafikiwa, huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa wananchi.

“Tukimbie kwa Afya, Tutumie Vipimo sahihi”.

Share:

PROF SHEMDOE, WANANCHI WARIDHISHWA NA UJENZI WA BARABARA ZA AFCON 2027 DAR ES SALAAM


Na OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara zinazoingia kwenye viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo na mazoezi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) jijini Dar es Salaam, huku wananchi wakifurahia hatua hiyo na kuipongeza Serikali kwa ujenzi wa miundombinu  itakayosaidia kutatua changamoto ya usafiri katika maeneo hayo.

Prof. Shemdoe amesema hayo Agosti 24, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Kigamboni, Uwanja wa Taifa (Benjamin Mkapa), Leaders Club pamoja na eneo la Mbweni kuelekea Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo.

Amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, akieleza kuwa ujenzi wa barabara za Kigamboni umefikia asilimia 75, barabara za Uwanja wa Taifa asilimia 20, Leaders Club asilimia 70, huku barabara za Mbweni kuelekea Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo zikifikia asilimia 20. Kwa ujumla, Prof. Shemdoe amesema utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo umefikia wastani wa asilimia 50.

Prof. Shemdoe amesema ametoa maelekezo kwa wakandarasi katika maeneo yote yanayotekeleza miradi hiyo kuhakikisha wanaongeza kasi ya ujenzi na kufanya kazi kwa saa 24, ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha ifikapo Agosti 30, 2026, utekelezaji unafikia wastani wa zaidi ya asilimia 60. 

Kwa upande wake, Mkazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Malindi Estate, Bi. Maria Bilia, amesema wananchi wa Mbweni wamefarijika kuona ujenzi wa barabara hizo ukiendelea, kwa kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya usafiri katika eneo hilo.

Bi. Bilia amemuomba Prof. Shemdoe kufikisha salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara kuelekea AFCON 2027.

Ameongeza kuwa ameshuhudia wakandarasi wakifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, hatua ambayo amesema inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Malindi Estate, Kata ya Mbweni, Manispaa ya Kinondoni, Bi. Selina Mkonye, amesema wananchi wa eneo hilo wanaunga mkono jitihada za Serikali kwa vitendo, ikiwemo kuwa na mpango mkakati wa miaka mitano wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 30 kwa kiwango cha lami na kilomita 60 kwa kiwango cha changarawe.

Bi. Mkonye amesema ujenzi wa barabara zinazotekelezwa kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 umekuja kuchagiza na kuimarisha mpango mkakati huo wa wananchi wa kuboresha miundombinu katika eneo lao.

Ujenzi wa barabara hizo unalenga kuboresha upatikanaji na mtiririko wa usafiri kuelekea viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michezo na mazoezi ya Fainali za AFCON 2027 jijini Dar es Salaam, sambamba na kuboresha miundombinu kwa manufaa ya wananchi.

Kwa sasa, miradi minne (4) inatekelezwa, ambayo ni ujenzi kwa kiwango cha zege wa Barabara ya Taifa yenye urefu wa kilomita 1.3, Litapwasi kilomita 0.43 na Sotele kilomita 0.2; ujenzi kwa kiwango cha zege wa Barabara ya Yanga yenye urefu wa kilomita 0.7; ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Dahomey yenye urefu wa kilomita 0.5; ujenzi wa Barabara ya Mbalizi yenye urefu wa kilomita 0.8, pamoja na uboreshaji wa maegesho ya VVIP katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo.


Share:

NMB: ELIMU ,UJUZI NI NGUZO UCHUMI WA KIPATO CHA JUU





Na Oscar Assenga, TANGA

BENKI ya NMB imesema uwekezaji katika elimu, ujuzi wa vitendo na ubunifu unaowawezesha Watanzania kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili nchi ni muhimu katika kufikia uchumi wa kipato cha juu.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mwandamizi wa Maabara ya Ubunifu ya NMB, Maria Mwamyalla, alipokuwa akitoa salamu za wadhamini kwa niaba ya wadhamini wote katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika mkoani Tanga.

Mwamyalla alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaendana na mkakati wa NMB wa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu, vijana na ujumuishaji wa kifedha.

Alisema kupitia Agenda 2030, benki hiyo imeweka teknolojia, ubunifu, uwekezaji kwa vijana na ujumuishaji wa kifedha kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa ukuaji.

“Mwelekeo huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa ushindani unaotumia maarifa, ujuzi na teknolojia,” alisema.

Alisisitiza kuwa teknolojia pekee haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwapo kwa watu wenye maarifa na ujuzi wa kuitumia ipasavyo.


NMB yawekeza Sh bilioni 2 kwa vijana

Mwamyalla alisema kupitia NMB Foundation, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika elimu na malezi ya uongozi kwa vijana, hususan wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.

Alisema kupitia programu ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni mbili tangu mwaka 2022, kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi 121 katika vyuo vikuu 11 nchini.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, wanafunzi hao wamekuwa wakisaidiwa mahitaji mbalimbali yakiwamo ada, malazi na vitendea kazi kama kompyuta mpakato.

Alisema wanafunzi 21 tayari wameingia katika soko la ajira, huku wengine 42 wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu.

“Tunatarajia kufungua dirisha la tatu la programu hii mwezi Septemba mwaka huu,” alisema.
Wabunifu wanufaika

Aidha, Mwamyalla alisema NMB inaendelea kutekeleza programu ya SEP kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Save the Children pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Alisema programu hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuwapatia vijana elimu ya vitendo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA.

Katika eneo la teknolojia na ubunifu, alisema NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni 232, huku sehemu kubwa ya suluhisho za kiteknolojia zikitengenezwa na wataalamu wazawa.

Alisema uwekezaji huo unalenga kujenga utaalamu wa Watanzania, kuimarisha usalama wa mifumo pamoja na kupunguza muda wa kupeleka bidhaa za kidijitali sokoni.

Alitaja miongoni mwa suluhisho hizo kuwa ni huduma ya NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki kupitia simu zao za mkononi, ikiwamo kutuma na kupokea malipo ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, huduma hizo zimechangia kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 10 wa NMB.

Alisema kupitia programu ya PesaTek, iliyoanzishwa mwaka 2022, benki hiyo imezindua Innovation Sandbox na kuendelea kuwawezesha vijana pamoja na wabunifu katika sekta ya teknolojia kupima na kuendeleza suluhisho zao.

Mwamyalla alisema NMB itaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi za elimu kuhakikisha elimu, ujuzi na ubunifu vinageuzwa kuwa suluhisho zinazochochea biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE AGOSTI 25,2026





Magazeti



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger