Sunday, 2 August 2026

KAPINGA: WAKULIMA WASIZALISHE BILA UHAKIKA WA SOKO

...

Serikali yaweka mkakati wa kuondoa tatizo la wakulima kuvuna mazao bila kuwa na uhakika wa soko, ikisisitiza kuwa kuanzia sasa uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi unapaswa kuongozwa na mahitaji ya soko badala ya utaratibu wa kuzalisha kwanza na kuanza kutafuta wanunuzi baada ya mavuno.

Mkakati huo unalenga kubadili mfumo wa uzalishaji nchini ili kuongeza kipato cha wakulima, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuimarisha viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kufungua masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) wakati akifungua Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Agosti 01, 2026 mkoani Morogoro.

Kapinga amesema kuwa uzoefu umeonesha kuwa ongezeko la uzalishaji pekee haliwasaidii wakulima endapo halitaambatana na masoko ya uhakika.

Kwa muda mrefu wakulima, wafugaji na wavuvi wamekuwa wakiongeza uzalishaji bila kuanza kwa kutambua mahitaji ya soko, hali iliyowafanya baadhi yao kuuza mazao kwa bei ya chini, kukosa wanunuzi au kupoteza sehemu ya mazao yao.

Kapinga ameongeza kuwa Maonesho ya Nanenane yanapaswa kuwa zaidi ya sehemu ya kuonesha teknolojia, yakitumika kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi, wasindikaji, vyama vya ushirika, taasisi za fedha na wasafirishaji ili kujenga mikataba ya kudumu ya biashara.

Hata hivyo Serikali sasa inataka kuona ongezeko la bidhaa zinazoongezwa thamani, viwanda vinavyojengwa karibu na maeneo ya uzalishaji, ajira mpya na mapato yanayobaki kwa wananchi badala ya kuendelea kuuza malighafi pekee.

Aidha, aliwahamasisha wawekezaji kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika usindikaji wa nafaka, matunda, mbogamboga, viungo, maziwa, nyama, ngozi, samaki na mazao mengine pamoja na huduma za uhifadhi, usafirishaji na utengenezaji wa vifungashio.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima aliwataka wakulima, wafugaji na wananchi kutoka ndani na nje ya mkoa huo kutumia siku zote za Maonesho ya Nanenane kujifunza teknolojia mpya zitakazowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji.

Alisema maonesho hayo yamekusanya taasisi za utafiti, wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuzitumia katika maeneo yao ili kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoshirikisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," inayolenga kuhamasisha uzalishaji unaoendana na mahitaji ya soko na kukuza uchumi wa viwanda.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger