Showing posts with label NEWS. Show all posts
Showing posts with label NEWS. Show all posts

Wednesday, 27 May 2026

JUMUIYA ZA KIRAIA 126 ZIMESAJILIWA NCHINI 2025/26- WAZIRI KATAMBI



Na mwandishi wetu,Dodoma

Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Jumla ya Jumuiya za Kiraia 126 zimesajiliwa Nchini, 12 kati yake zikiwa ni Jumuiya za kidini na 114 zisizo sa kidini.

Takwimu hizo zimebainishwa leo Jumatatu Mei 25, 2026 Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi wakati akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2026/27, akibainisha kwamba ukaguzi wa jumuiya 350 ulifanyika na Wizara yake katika kipindi kama hicho cha Julai 2025 hadi Aprili, 2026, lengo likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa masharti ya usajili pamoja na kubaini mchango wa Jumuiya hizo katika maendeleo.

"Mhe. Spika, pia Wizara imeanzisha programu za ushirikishwaji ili kuimarisha uelewa na uwajibikaji wa viongozi wa jumuiya za kiraia katika uendeshaji wa jumuiya zao. Kupitia programu hiyo, jumla ya viongozi wa jumuiya za kidini na zisizo za kidini 2,500 walipatiwa mafunzo kuhusu uendeshaji wa jumuiya unaozingatia sheria na kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. 

Katika mwaka 2026/27, Wizara imetenga Shilingi bilioni 1.57 kwa ajili ya shughuli za usimamizi na uratibu wa Jumuiya za Kiraia nchini." Amesema Waziri Katambi.
Share:

Tuesday, 26 May 2026

WAZIRI SANGU AZINDUA BODI YA SABA YA USHAURI YA OSHA.


-Asisitiza Utekelezaji wa Viwango vya Kimataifa vya Usalama na Afya katika Maeneo ya Kazi

Na, OWM-KAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amezindua Bodi ya Saba ya Ushauri ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali, Sura ya 245 Toleo la mwaka 2023 chini ya Kifungu cha 6 cha sheria hiyo.

Amezungumza hayo tarehe 25 Mei, 2026 wakati wa uzinduzi huo, Waziri Sangu amesema bodi hiyo ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa OSHA ili kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo na kuhakikisha mikakati inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kuzingatia dira, dhima na malengo ya Serikali.

Amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo ni kushauri kuhusu uandaaji na utekelezaji wa mpango mkakati wa OSHA, kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi kupitia taarifa za mwaka na hesabu za wakala, pamoja na kutoa ushauri kuhusu maslahi na stahili za watumishi kwa lengo la kuongeza motisha, uwajibikaji na tija mahali pa kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameielekeza bodi hiyo kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 155 na 187 ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vya usalama na afya mahali pa kazi vinaendelea kuzingatiwa nchini.

Aidha, ameitaka bodi hiyo kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya kidijitali, ikiwemo mfumo wa Workplace Information Management System (WIMS), kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali.

"Majukumu haya yatekelezwe kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali pamoja na misingi ya uwajibikaji, uadilifu, ubunifu, ushirikiano kazini na uwazi" amesema Waziri Sangu.

Sambamba na hilo, amesema bodi hiyo inaanza majukumu yake katika kipindi muhimu ambapo Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, huku uzinduzi wa Mpango Mkakati wa OSHA ukiwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo.

Waziri Sangu pia ameisisitiza bodi hiyo kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo iliyowekwa, huku akiitaka kutoa nafasi kwa menejimenti ya OSHA kusimamia shughuli za kila siku bila kuingiliwa. Amesema jukumu kuu la bodi ni kutoa ushauri na usimamizi wa kimkakati ili kuhakikisha kila upande unatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri OSHA, Makwaia Makani, ameishukuru Serikali kwa imani iliyowaonesha na kuahidi kuwa bodi hiyo itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bi. Zuhura Yunus, amewapongeza wajumbe wa bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa, akiwataka kutumia weledi na umahiri wao katika kuisimamia OSHA kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema bodi zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taasisi hiyo na kwamba menejimenti ya OSHA ipo tayari kushirikiana na bodi mpya ili kuendelea kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma.
Share:

MTWARA YAFUNGUA FURSA MPYA KATIKA SEKTA YA CHUMVIMTWARA YAFUNGUA FURSA MPYA KATIKA SEKTA YA CHUMVI

- Serikali yapunguza gharama za leseni ya Madini Chumvi, wachimbaji wanufaika

📍Mtwara

Mkoa wa Mtwara umeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji katika sekta ya chumvi kutokana na uwepo wa fukwe zinazofaa kwa uzalishaji, maboresho ya mazingira ya biashara na ongezeko la uzalishaji linalofikia takribani tani 90 kwa majaruba manne katika baadhi ya maeneo ya uzalishaji.

Kutokana na hatua hiyo, wachimbaji na wazalishaji wa chumvi wameanza kunufaika na fursa mpya za kiuchumi kupitia kuongezeka kwa uzalishaji, ajira na upanuzi wa maeneo ya uzalishaji.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Winnifrida Mrema, amesema sekta ya chumvi mkoani humo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchakataji wa chumvi.

Amesema maboresho hayo yanalenga kuongeza ubora wa chumvi kwa matumizi ya majumbani, viwandani na mifugo, huku yakichochea ajira kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka mashamba ya chumvi.

“Mtwara ina mazingira rafiki kwa uzalishaji wa chumvi na Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hii ili kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Mrema.

Katika Kijiji cha Mnete, Kata ya Nalingu Halmashauri ya Mtwara Vijijini, msimamizi wa mashamba ya chumvi, Salum Amani, amesema mashamba hayo yanamilikiwa na Zamda Khatibu na yana leseni mbili za uvunaji chumvi pamoja na majaruba 24 yanayotumika kwa uzalishaji.

Amesema kwa sasa wanaendelea na shughuli za usafishaji wa majaruba baada ya msimu wa mvua ili kuruhusu maji ya chumvi kuingia tayari kwa uzalishaji mpya.

Kwa mujibu wa Salum, uzalishaji wa chumvi hutegemea hali ya hewa, ambapo jua kali huwezesha chumvi kukauka ndani ya siku 30, huku hali ya baridi ikifanya mchakato huo kuchukua hadi siku 40.

“Kwa kawaida majaruba manne huzalisha takribani tani 90 za chumvi kwa msimu mmoja, huku shughuli hizi zikitoa ajira kwa wafanyakazi tisa katika eneo hili,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Mkoa wa Mtwara na  Mwenyekiti wa Kamati ya Chumvi kupitia  FEMATA, Khalfan Nassoro, amesema kupunguzwa kwa gharama ya ada ya pango ya leseni za chumvi  kutoka Shilingi 45,000 hadi Shilingi 20,000 kumeongeza uwezo wa wazalishaji kupanua maeneo ya uzalishaji.

Amesema hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wawekezaji na wachimbaji wadogo, huku akisisitiza kuwa mazingira bora ya uwekezaji yataifanya Mtwara kuwa kitovu kikuu cha uzalishaji wa chumvi nchini.

Nassoro amesema pia ukuaji wa sekta hiyo unaweza kuchochea ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya chumvi na hivyo kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.






Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE MEI 26,2026


Magazeti





Share:

Monday, 25 May 2026

FOUNTAIN GATE FC YAJIANDAA KWA VITA YA MECHI ZA MWISHO LIGI KUU

Na Bora Mustafa, Arusha.

Kocha Mkuu wa Fountain Gate FC, Felix Minziro amesema licha ya timu yake kukabiliwa na changamoto ya kikosi kuwa kipana, muda wa mapumziko walioupata umeisaidia timu kujiandaa vyema kuelekea michezo iliyosalia ya Ligi Kuu. 

Amesema miongoni mwa michezo hiyo ipo dhidi ya vigogo kama Azam FC pamoja na Young Africans SC katika mechi tano za mwisho wa msimu.

Akizungumza Minziro amesema hayo Leo 25, mei, ,2025  jijini Arusha ambapo timu hiyo imeweka kambi maalum kwa ajili ya kuimarisha utimamu wa mwili na akili kwa wachezaji wake baada ya ratiba ngumu ya michezo ya mfululizo..

 Pia amesema mapumziko ya wiki moja yaliyopatikana yamekuwa msaada mkubwa kwa wachezaji kurejea kwenye kiwango kizuri kabla ya kuendelea na mechi zilizobaki.

Hata hivyo, Minziro amebainisha kuwa changamoto kubwa waliokuwa nayo si majeraha makubwa bali ni uchovu pamoja na majeraha madogomadogo yaliyotokana na ushindani wa ligi hiyo.

 Ameongeza kuwa mazingira mazuri ya mazoezi yanaendelea kuwasaidia wachezaji kurejea kwenye ubora wao kwa haraka.

Aidha, amesema benchi la ufundi linaendelea kufuatilia maendeleo ya kila mchezaji kwa karibu ili kuhakikisha timu inaingia kwenye michezo iliyobaki ikiwa kwenye hali bora zaidi.

 Kwa upande wake, Meneja wa Fountain Gate FC, Zamkufo Elias amesema timu hiyo bado inaendelea kufanya tathmini ya michezo iliyopita kwa lengo la kurekebisha makosa yaliyojitokeza kabla ya mechi zijazo.

Zamkufo amesema ushindani wa ligi kwa sasa ni mkubwa kutokana na baadhi ya timu kupigania ubingwa huku nyingine zikisaka nafasi ya kubaki salama kwenye ligi, hali inayofanya kila mchezo kuwa na ushindani mkubwa zaidi.


Kwa upande wake, mchezaji wa Fountain Gate FC, Shomari Mponzi amesema wachezaji wameendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri katika michezo iliyobaki ya ligi. Pia amewataka mashabiki kuendelea kuiunga mkono timu hiyo katika kipindi hiki muhimu huku akisisitiza kuwa kila mchezaji anaendelea kutekeleza majukumu yake kwa nidhamu na kujituma kwa ajili ya mafanikio ya klabu hiyo.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger