Na Hellen Kwavava-DAR ES SALAAM
MRADI wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) umekuwa ni kichocheo cha ukuaji wa Uchumi katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na kurahisisha hali ya usafiri kwa Jamii hiyo.
Meneja Usalama Tawi la Tanzania, kutoka Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC), Li Yuling amesema hayo jijini Dar es Salaam alipozungumza na Waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya Jiao Zhu China -Tanzania.
Wakati anazungumzia mradi huo wa BRT, awamu ya nne sehemu ya tatu amesema mradi huo ni sehemu muhimu ya urafiki wa China na Tanzania, na kwamba sio tu unaboresha usafiri wa umma wa Dar es Salaam ambao ni mji wa kibiashara wa Tanzania.
"Mradi huu unajumuisha ujenzi wa vituo muhimu vya usafiri, vituo vya mabasi na vifaa vingine vya trafiki. Unalenga kuboresha ufanisi wa usafiri wa mijini, kupunguza msongamano na kuimarisha hali ya usafiri ya wakazi wa eneo hilo," amesema.
Li amesema nia yao kubwa katika kuadhimisha siku hii ni kuonyesha watanzania juu ya dhamira ya makampuni ya Kichina katika maendeleo ya miundombinu inayoyafanya.
"Ili kuendeleza mafanikio hayo na kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, kampuni ya ujenzi ya China tawi la Tanzania imekutana na waandishi wa habari, kuzungumzia mafanikio hayo," amesema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkandarasi katika mradi huo, You Xudong amesema mradi huo unaendelea katika eneo la Kivukoni, utachukua miezi 18.
Amesema wanajenga jengo la ulinzi, choo, jengo la tiketi namba moja na jengo la tiketi namba mbili.
Pamoja na hayo Mradi huo unaoendelea katika eneo la kivukoni jijini Dar es Salaam umeweza kushirikisha wanafunzi wazawa wanaosomea uhandisi kutoka Taasisi ya teknolojia Dar es Salaam(DIT).
Kwa upande wake Mwalimu Alvin Rujweka kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT), amesema wamekuwepo na wanafunzi wao wanaosomea uhandisi kwa ajili ya masomo ya vitendo katika kampuni hiyo ya kichina ya CCCC.
"Wanafunzi wanaoandaliwa kuwa wahandisi, wanapewa elimu ya vitabu na vitendo. Njia nyingine tunawapeleka kwenye miradi mbalimbali inayoendelea nchini, tunawaunganisha na soko kupitia fani walizosomea, " amesema.
Naye Mhitimu wa Diploma DIT mwaka huu 2024, Benson Mbilinyi amesema amepata nafasi ya kujiunga na kampuni hiyo ya CCCC na anafanya kazi kama mhandisi msaidizi Jambo ambalo anajivunia kupata nafasi hiyo hasa kwa vitendo.
Hata hivyo Mhitimu huyo ameendelea kutoa Ushauri kwa wanafunzi kujitokeza kwenye fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondoa utegemezi katika Jamii.
0 comments:
Post a Comment