Friday, 13 December 2024

MWILI WA MWANAMKE ALIYESOMBWA NA MTO WAPATIKANA, WACHACHE WAMZIKA

...
Mwili wa marehemu ukiopolewa mtoni
Mwili wa Leah George (Nkwimba) mwenye umri wa miaka 44, mkazi wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, aliyefariki dunia baada ya kusombwa na maji katika daraja la Machimu lililopo mtaa wa Tambukareli mjini Shinyanga, umezikwa leo katika makaburi ya Dodoma mjini Shinyanga.

Mazishi yamefanyika leo majira ya saa 11 jioni, na kuhudhuriwa na watu wachache wakiwemo ndugu wa marehemu kwa kuwa tayari ulikuwa umeshaharibika, hali iliyolazimu upitilizwe moja kwa moja makaburini na kuwanyima fursa watu waliokuwa wakisubiri nyumbani kwa ajili ya kuaga kabla ya mazishi kama ilivyo katika desturi za kijamii.


Kwa mujibu wa Afisa Oparesheni wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga Inspector Edward Seleman, ambaye alikuwa akiongoza kikosi cha kuutafuta mwili huo, amesema wameupata leo kwenye kijiji cha Mwagala (B) Kata ya Ibadakuli katika Manispaa ya Shinyanga, baada ya kupewa taarifa na raia wema majira ya saa tatu asubuhi, ambapo waliukuta ukiwa umenasa kwenye mizizi ya mti uliopo kwenye ukingo wa mto.

Leah alifariki dunia Desemba 9, 2024, majira ya jioni, baada ya kusombwa na maji wakati akijaribu kuvuka daraja, kufuatia mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga na kusababisha baadhi ya madaraja kufunikwa na maji.

Awali Mama mzazi wa Leah Bi. Rachel Faustine (72) aliiambia Redio Faraja kuwa, siku ya tukio mwanaye aliondoka nyumbani asubuhi na kwenda mtaa wa Tambukareli kwa shughuli zake, lakini hakurudi mpaka kesho yake Desemba 10, 2024, alipopigiwa simu na kuelezwa kuwa amesombwa na maji katika daraja la Machimu, wakati akijaribu kuvuka kurudi nyumbani baada ya mvua kukatika.


Alisema baada ya kupata taarifa hizo alishirikiana na majirani kuwataarifu viongozi wa mtaa, ambapo Mwenyekiti wa Mtaa huo alifika na kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji ambalo lilifika eneo la tukio na kuanza kuutafuta mwili wa Leah bila mafanikio.


Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome Bw. Solomon Nalinga Najulwa, amelishukuru Jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na wananchi kwa namna walivyofanya juhudi mpaka kufanikisha kupatikana kwa mwili huo, ambao wameutafuta kwa muda wa siku tatu bila kukata tamaa mpaka ulipopatikana na kuzikwa kwa heshima zote za kibinadamu.

Chanzo- Faraja Fm
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger