Wednesday, 18 December 2024

REA YATENGA FEDHA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI TANGA

...
Na Hadija Bagasha Tanga,

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji lengo likiwa ni kuwezesha huduma ya nishati safi ya kupikia na hatimaye kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia Nchi.

Hivyo kupitia mpango huo itatoa mitungi ya gesi 26,040 kwa wilaya nane za mkoa wa Tanga zitakazokuwa na thamani ya shilingi milioni 455.7 ambazo zitagawiwa wananchi kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaotokana na watu kutumia nishati ya mkaa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa uuzwaji mitungi ya gesi ya LPG ya uzito wa kilo sita kwa bei ya ruzuku katika mkoa wa Tanga Mkurugenzi wa Teklonojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, wa REA Mhandisi Advera Mwijage katika hafla fupi ya kumkabidhi mradi huo Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian, alisema kila wilaya za mkoa huo utapatiwa mitungi 3,255.

Alisema mitungi hiyo ambayo wananchi watalazimika kununua kwa kiasi cha sh, 17,500 na serikali itaongeza sh. 17,500 na msambazi katika mkoa wa Tanga itakuwa kampuni ya Manjis ambao wataisambaza kwa wakala watakaowachagua hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema Tanzania ina uwezo wa kuhakikisha upatikanaji wa nisahati safi, bora na rafiki wa mazingira katika maeneo ya vijijini, lakini pia idadi kubwa ya watu wanatumia mazao yanayotokana na misitu kupikia hivyo kuleta uharibifu mkubwa wa mazingira.

Mhandisi Mwijage alisema utafiti uliofanywa mwaka 2016 unakadiriwa kuwa watu 33,024 hufariki dunia kabla ya wakati kila mwaka ambayo ni sawa na asilimia 8.49 ya vifo vyote nchini kutokana na magonjwa ambayo yanachangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba wakati wa upikaji kwa kutumia nishati isiyo safi na salama.

“Hivyo serikali kupitia wakala wa nishati vijiji REA umetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi LPG katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji kupitia mradi wa ufadhili unaotegemea matokeo (RBF) lengo ni kukukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresdha upatikanaji wa nishati safi na salama.

Mhandisi Mwijage alisema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na malengo ya makakati wa Kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya mwaka 2024-2034 uliozinduliwa Mei 2024 na Rais Dkt Samia Sukuhu Hassan  ambao unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya Watanzania wote wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Akipokea mradi huo Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Burian wa unaendelea kumpongeza Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuwa kinara wa maono baada ya kuzindua mpango huo ambao utasaidia wananchi kutunza mazingira kwa ajili ya nchi. 

Alisema mkoa huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wametoa elimu kwa wananchi ili waweze kuachana na matumizi ya nishati za kuni na mkaa badala yake waweze kutumia nishati safi na salama na wameweka mpango kuhakikisha ziara ya rais hivi karibuni mkoani hapa watagawa mitungi hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi matumizi ya nishati hiyo.

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa huyo alitoa rai kwa REA kuhakikisha wanatoa elimu kwa vijana ili waweze kutengeneza majiko makubwa ya gesi ambayo yatatumika na wananchi hasa mamantilie ambao mitungi ya gesi inayosambazwa haiwezi kukidhi mahitaji yao ya kupika chakula na mboga.

“REA kaeni na taasisi hizi,  vijana wetu hawana ajira wabuni na watengeneze majiko yatakayowasaidia mamantilie kuweza kupika chakula na mboga kwa wakati mmoja, lakini pia hakikisheni mnatengeneza mitungi ya gesi ya lita tatu ili wananchi wetu vijijini waweze kumudu kununua,” alisema Balozi Burian.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger