Monday, 31 August 2026

NMB YAFUNGUA NJIA MPYA YA MIKOPO KWA WAFANYABIASHARA, WABUNGE WAIJIVIA

...




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

BENKI ya NMB imepanua wigo wa huduma za mikopo kwa kuanzisha mfumo wa kidijitali unaowawezesha wateja kukopa hadi Sh milioni tano bila kuweka dhamana, hatua inayolenga kuwafungulia fursa zaidi wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali.

Hatua hiyo imekuja wakati benki hiyo ikiendelea kuboresha huduma zake za kifedha kupitia teknolojia, huku tathmini ya uwezo wa mteja kukopa ikifanyika kwa kuangalia historia ya miamala yake badala ya kutegemea zaidi dhamana za mali.

Akizungumza katika Bonanza la Bunge lililowakutanisha wabunge, wizara na taasisi mbalimbali jijini Dodoma, Afisa Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, alisema maboresho hayo yanalenga kufanya huduma za mikopo kuwa rahisi, haraka na kupatikana kwa watu wengi zaidi.

Alisema kupitia huduma ya NMB Mkononi, mteja anaweza kutumia huduma ya mkopo wa kidijitali ya MshikoFasta bila kulazimika kufika katika tawi la benki au kupitia taratibu ndefu za maombi.

Kwa mujibu wa Mponzi, mteja wa kawaida anaweza kukopa hadi Sh milioni mbili bila kujaza fomu wala kuweka dhamana, huku mfumo ukitumia historia ya miamala katika kutathmini uwezo wa mteja kurejesha mkopo.

“Mkopo huu ni suluhisho kwa wananchi wetu, wakiwemo wabunge, mamalishe, bodaboda na wafanyabiashara wengine. Hakuna dhamana inayohitajika, tunaangalia miamala yako,” alisema.

Alisema mfumo huo unalenga pia kuwasaidia wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishindwa kupata mikopo kutokana na masharti yanayohitaji dhamana, pamoja na taratibu nyingi za kifedha.
WAJASIRIAMALI KUFIKIA SH MILIONI 5

Mponzi alisema NMB imeboresha pia huduma zake kwa wajasiriamali, ambapo wafanyabiashara wanaweza kupata mikopo ya hadi Sh milioni tano bila kuweka dhamana.

Alisema katika huduma hiyo, uwezo wa biashara kukopa unatathminiwa kwa kuangalia mwenendo na taarifa za miamala ya biashara, hatua inayolenga kuifanya historia ya biashara kuwa sehemu muhimu ya kupata huduma za kifedha.
NMB YABADILI MFUMO WA KIBENKI

Mbali na maboresho ya huduma za mikopo, Mponzi alisema NMB imeingia katika mfumo mpya wa kibenki baada ya kutumia mfumo wa awali kwa takribani miaka 15.

Alisema mabadiliko hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma na kuiwezesha benki kutoa huduma za kisasa zaidi, hususan katika eneo la huduma za kidijitali.

“NMB tumeingia kwenye mfumo mpya. Tunatarajia kuona mambo mazuri zaidi katika huduma zote kutokana na kuingia kwenye mfumo huu mkubwa,” alisema.
MBUNGE AIPONGEZA NMB

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Machano Ali Machano, aliipongeza NMB kwa mchango wake katika shughuli za Bunge, akisema wabunge wanatambua na kuthamini ushirikiano unaotolewa na benki hiyo.

Alisema ushirikiano huo umeonekana pia katika shughuli za michezo, ikiwemo bonanza lililowakutanisha wabunge, wizara na taasisi mbalimbali jijini Dodoma.

Machano alisema mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki yanatarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi Desemba mwaka huu, yakishirikisha wabunge kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Tanzania na wadau wake, ikiwemo NMB, wanapaswa kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo.
SILLO: MICHEZO NI SEHEMU YA AFYA YA WABUNGE

Naye Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, alisema Bunge lipo tayari kushirikiana na Serikali katika kufanikisha mashindano ya AFCON, akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya, umoja, udugu na nidhamu.

Sillo alisema michezo ni muhimu pia katika kupunguza msongo wa mawazo, jambo alilosema ni muhimu kwa wabunge kutokana na majukumu yao ya kutunga sheria, kusimamia Serikali na kufanya maamuzi.

“Nimefurahishwa kuona idadi kubwa ya washiriki katika michezo ya leo. Michezo hupunguza msongo wa mawazo na mwili wenye afya ni suluhisho muhimu katika kufanya maamuzi mazuri,” alisema.

Aliwapongeza washindi na washiriki wote wa bonanza hilo, huku akiishukuru NMB kwa kufanikisha shughuli hiyo.

Alisema ushirikiano huo umewezesha wabunge kupata muda wa kushiriki michezo na kurejea katika majukumu yao wakiwa na afya bora na nguvu mpya.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger