Saturday, 8 August 2026

TBS YENDELEA KUTOA ELIMU YA UTHIBITISHAJI UBORA WA BIDHAA NANENANE MOROGORO

...
Meneja wa TBS Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji akitoa elimu ya Viwango kwa Wajasiriamali wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam  katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea Mkoani Morogoro

*********

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanathibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kuongeza wigo wa masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Akizungumza wakati wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki, Meneja wa TBS Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, amesema shirika hilo linaendelea kuwasaidia wazalishaji na wajasiriamali kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vinavyotakiwa, hatua inayoongeza uaminifu wa bidhaa katika soko.

Amesema katika kutambua umuhimu wa kuwawezesha wazalishaji wa bidhaa mbalimbali, TBS kwa kushirikiana na Shirika la Viwango la Afrika (ARSO), imezindua rasmi Alama ya Ubora ya Afrika, ambayo inalenga kusaidia bidhaa zinazokidhi viwango kuingia katika masoko ya Afrika kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Aidha, amewahamasisha wajasiriamali kuchangamkia fursa ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwa kuwa Serikali inagharamia huduma hiyo, hatua ambayo itawasaidia kuondokana na baadhi ya vikwazo vya kibiashara na kuongeza ushindani wa bidhaa zao.

“Hapo awali, bidhaa zilizothibitishwa na TBS ziliweza kuingia katika masoko ya nchi za Afrika Mashariki bila vikwazo vikubwa, lakini sasa wigo wa soko umeongezeka na bidhaa hizo zinaweza kunufaika na fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA),” amesisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Mhandisi Cyril Kimario, amewataka wananchi kuhakikisha wananunua na kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na TBS, huku akiwahimiza kujenga utamaduni wa kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio.

Amesema kufanya hivyo kutawasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu bidhaa wanazonunua na kuhakikisha wanapata bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango.

“Kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake humhakikishia mwananchi usalama wa afya yake pamoja na uchumi wake, kwani anakuwa amepata kitu bora chenye thamani katika afya na uchumi,” amesema.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wananchi katika kuchagua bidhaa zenye alama na taarifa sahihi za ubora ni sehemu muhimu ya kujenga soko lenye ushindani na kulinda afya na maslahi ya watumiaji.
Meneja wa TBS Kanda ya Mashariki, Mha. Cyril Kimario akitoa elimu ya Viwango kwa Wajasiriamali wa Halmashauri ya Kibaha katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea Mkoani Morogoro
Meneja wa TBS Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji akitoa elimu ya Viwango kwa Wajasiriamali wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam  katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea Mkoani Morogoro
Afisa udhibiti Ubora Mkuu (TBS) Bw. Stephen Rwabunywenge akitoa elimu ya viwango kwa wajasiriamali kutoka halmashauri mbali mbali za mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea Mkoani Morogoro
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger