UNAWEZA kusema ni kufuru, kwani tayari Yanga imefanikiwa kumsainisha Marcio Maximo mkataba wa miaka miwili na anatua nchi kesho saa saba 7:55 mchana tayari kuanza kazi.
Maana yake kuanzia leo, hesabu saa 24 wakati Wabrazil hao watatu watakapotua Yanga ambayo inaweka rekodi mpya ya kuajiri Wabrazil watatu kwa wakati mmoja.
Maximo hatakuwa peke yake, anatua akiwa na msaidizi wake, Leonardo Neiva Martins ambaye pia amesaini mkataba wa kuifundisha Yanga kwa miaka miwili pia wataongozana na kiungo mshambuliaji mmoja aitwaye Andrey Ferreira Coutinho.
Watatu hao watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Johannesburg nchini Afrika Kusini, alifajiri na wataondoka hapo saa 3:30 asubuhi kuja jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji huyo ambaye Maximo amewaambia Yanga kuwa ni tishio anayeweza mikiki ndiye chaguo lake baada ya kuambiwa aje na mchezaji mmoja ambaye aanaamini atakuwa msaada kwa Yanga na kwake pia.
Watatu wote hao watatua nchini wakiwa ndani ya dege la Shirika la Ndege la Afrika Kusini maarufu kama SAA na mara moja watapelekwa kupumzika kabla ya siku inayofuata kukutana na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.
Coutinho ambaye amewahi kucheza soka pamoja na mshambuliaji nyota wa Brazil, Neymar wakiwa makinda, atamalizana na uongozi wa Yanga mara tu baada ya kutua nchini.
Championi kilikuwa chombo cha habari cha kwanza nchini kueleza kuhusiana na ujio huo wa Maximo ambaye mara ya kwanza aliichoropoka Yanga kidogo tu na nafasi yake ikachukuliwa na Ernie Brandts raia wa Uholanzi.
Hadi anatua Yanga, Coutinho alikuwa anakipiga katika klabu ya Pysandu inayoshiriki Ligi Darala la Pili nchini Brazil maarufu kama Serie C.
Amezaliwa Januari 12, 1990, maana yake ana umri wa miaka 24 na ameahidi kuonyesha uwezo mkubwa ili iwe nafasi kwake kusonga mbele zaidi ya hapa Tanzania.
Hata hivyo, Coutinho alikuwa ameichezea Pysandu mechi tatu tu dhidi ya Luverdense, Araguaina na Rio Branco-AC.
Hata hivyo, Yanga haitakuwa klabu ya kwanza kuleta mchezaji rais wa Brazil, moja wapo ni Coastal Union iliyofanya hivyo msimu uliopita, lakini mchezaji huyo akashindwa na kurejea kwao huku akisisitiza mazoezi yalikuwa makali kama ya riadha.
Lakini inawezekana Coutinho akawa na nafasi nzuri ya kucheza kwa kuwa atakuwa chini ya Wabrazil wawili ambao wanaujua uwezo wake.
Neiva ambaye ni msaidizi, moja kwa moja anachukua nafasi ya Mkwasa ambaye amepata kazi nchini Saudi Arabia na sasa atainoa Shaolah FC akiwa chini ya Hans van der Pluijm aliyekuwa bosi wake Yanga.
0 comments:
Post a Comment