Makala haya ni mwendelezo wa makala yaliyoanza
wiki iliyopita. Madhumuni ya makala hizi ni kupitia kamati zote za Bunge
Maalumu kiuchambuzi ili kubaini mapendekezo ambayo yanadhoofisha
Muungano. Aidha, uchambuzi huu utawawezesha wadau wote katika mchakato
wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania ikiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba kuwa na utambuzi wa kina kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya.
Kamati namba 1 katika ukurasa wake wa 8 inasema
“kiutawala na kimamlaka” Serikali ya Muungano kama ilivyopendekezwa
katika Rasimu inatenganishwa na wananchi kwa sababu haihusiki na mambo
yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Hoja hii ya Kamati haina mashiko na
haiakisi uhalisia sasa wa namna Serikali inaevyoenenda kiutawala na
kimamlaka, lakini pia huu sio uhalisia wa yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba Mpya Toleo la Pili.
Katika Muundo wa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano
hana uhusiano wa moja kwa moja na raia wa Tanzania waishio Tanzania
Zanzibar hasa katika masuala ya maendeleo ambayo ndiyo yanayowagusa watu
wa kawaida moja kwa moja. Mambo haya si ya Muungano Kikatiba. Mfano
mzuri ni sekta zote muhimu si mambo ya Muungano kivitendo, sekta hizi ni
pamoja na Kilimo, Afya, Uchukuzi, Miundombinu na Elimu.
Aidha, kwa kuzingatia marekebisho ya Katiba ambayo
yameshafanyika hasa kwa Katiba ya Zanzibar na mabadiliko yasiyo rasmi
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Uhalisia ni kwamba, Rais wa
Jamhuri ya Muungano hushughulikia mambo ya Maendeleo Kikatiba kwa
Watanzania waishio Tanzania Bara au Tanganyika pekee. Kitendo hiki
kinawatenga Watanzania waishio Zanzibar na kinamwondolea Rais wa Jamhuri
ya Muungano wajibu wa moja kwa moja wa kuwahudumia Watanzania kutoka
pande zote mbili za Muungano kwa usawa.
Rasimu inapendekeza Sura nzima ya Pili
inayozungumzia Malengo Makuu na Misingi ya Mwelekeo Shughuli wa Serikali
na Sera za Kitaifa. Hapa ndiyo tunazungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa
ambayo Mamlaka zote Tatu zinapaswa kuitekeleza kupitia Mambo ya
Muungano (rejea Ibara ya 63) na Mambo yasiyo ya Muungano (rejea Ibara ya
64, 65 na hasa Ibara ya 111[1][b]).
Unapowianisha sera na sheria kwa mambo yasiyo ya
Muungano chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Muungano, ndiyo dhana
inayostawisha usawa, haki, ushiriki wa moja kwa moja, mshikamano,
kusaidiana na kupelekea maisha bora kwa kila Mtanzania kokote anapoishi
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwe ni Tunduru au ni Tumbatu.
Kitendo hiki ndio ambacho hasa Rasimu ya Katiba
inapendekeza katika nchi yetu, kitendo hiki sio tu kitaimarisha Muungano
wetu na kutatua kero na changamoto za wananchi bali ndio kitendo
kitakachoimarisha Jamhuri ya Muungano ikiwa na umoja wa kitaifa na
usalama.
Kamati inaendelea katika taarifa yake ukurasa wa 9
kwa kuweka pendekezo la eneo la Jamhuri ya Muungano linalosomeka eneo
la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote laTanzania Bara na eneo lote la
Zanzibar na linajumuisha sehemu zake zote za bahari, maziwa, mito na
maeneo mengine yatakayoongezwa.
Ili kulielewa pungufu la pendekezo hili yapasa
kuelewa mambo kadhaa, Kwanza ni usanifu na uandishi wa Katiba na namna
Rasimu ilivyoandikwa. Pili ni uwepo wa Mikataba ya Kimataifa
inayosimamia mipaka ya nchi na hapa nitafafanua Mikataba ya Kimataifa
ambayo inasimamia mipaka ya Tanzania katika ardhi (iwe tambarare,
milima, vilima au mabonde) na kwenye maji (iwe mito, maziwa au bahari
sehemu ya nchi pamoja bahari kuu) na tatu ni mifano ya nchi nyingine.
Usanifu na uandishi wa Katiba ni stadi na ni
muundo wa namna Katiba inavyoandikwa na kupangwa kwa maana ya sura,
sehemu na vifungu. Uandishi na usanifu unazingatia kuhakikisha vifungu
vinafahamiana, vinasomeka pamoja, vinashirikiana na kwa namna yoyote
havigongani. Katiba katika usanifu yaweza kuchukua muundo ambao
umejikita katika kueleza misingi pekee au kuweka misingi pamoja na
masharti yanayojifafanua au Katiba ikaandikwa ikiwa na masharti
yanayojifafanua kwa kina kwa kiingereza ‘prescriptive.’
Usanifu wa Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili
umezingatia muundo unaojumuisha Misingi na Masharti yanayojifafanua kwa
pamoja. Muundo huu ndiyo uliotumika kuandika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya 1977 Toleo la Mwaka 2005. Ili kuielewa Rasimu ni lazima
usome masharti yake kwa pamoja au ‘in tanderm’ kwa lugha ya Kiingereza.
Nachelea kusema kama uandishi wa pendekezo la Kamati ulizingatia
uhalisia huu.
Ukitaka kuielewa Ibara ya 2 ya Rasimu
inayozungumzia eneo la Jamhuri ya Muungano (kama Msingi) ni lazima
uisome na Ibara ya 49 inayohusu pamoja na mambo mengine, wajibu wa raia
kuilinda Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 51 inayozungumzia ulinzi wa mali
ya umma, hii ikijumuisha eneo letu la ardhi kama Nchi na Taifa na Ibara
ya 235(2) inayozungumzia ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano.
Utagundua hasa Ibara 235(2) inaweka masharti yanayotoa ufafanuzi wa
Ibara ya 2 katika muktadha wa ulinzi wa eneo la Jamhuri ya Muungano
ikijumuisha ardhi, anga na bahari kuu. Mito na maziwa ni sehemu ya pande
la ardhi.
0 comments:
Post a Comment