MATOKEO ya Mtihani wa Majaribio (Mock)
kwa mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu na Kidato cha Sita mwakani,
yatachangia alama 10 za Alama Edelevu (CA). Kwa utaratibu huu, matokeo
ya mwisho ya mtahiniwa, yatatokana na asilimia 30 ya Alama Endelevu na
asilimia 70 ni mchango wa Alama za Mtihani wa Taifa.
Asilimia 30 za Alama Endelevu,
zitapatikana kutokana na mitihani mbalimbali. Kwa Kidato cha Nne mwaka
huu, alama hizo zitatokana na matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha
pili ambao utakuwa na alama 10, matokeo ya kidato cha tatu muhula wa
kwanza na wa pilialama tano, matokeo ya mtihani wa majaribio( mock) wa
Kidato cha Nne ni alama 10 na majaribio ya kazi alama tano.
Utaratibu huu umetokana na viwango vipya
vya ufaulu, vilivyoainishwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)
kwenye kitabu cha Mwongozo wa Matumizi ya Viwango vya Ufaulu na
utaratibu wa kutunuku matokeo ya kidato cha nne na sita. Kwa Kidato cha
Sita, zitatokana na matokeo ya mtihani wa kidato cha tano muhula wa
kwanza na pili alama 15, matokeo ya ‘mock’ alama 10 na kazi mradi
itakuwa ni alama tano.
“Katika somo ambalo mtahiniwa hakufanyia
Kazi za majaribio, alama za matokeo ya Mitihani ya ‘Mock’ ya Kidato cha
Nne na Kidato cha Sita, itachangia alama 15 badala ya 10
zilizoainishwa,” imefafanua sehemu ya mwongozo huo.
Hata hivyo, katika Mtihani wa Kidato cha
Nne mwaka jana na Kidato cha Sita mwaka huu, mchanganuo wa alama 30 za
Alama Endelevu ni alama 15 zinazotokana na matokeo ya mtihani wa taifa
wa kidato cha pili, asilimia 10 ilitokana na maendeleo ya mitihani ya
kidato cha tatu muhula wa kwanza na pili na matokeo ya muhula wa kwanza
kidato cha nne na kazi za majaribio asilimia tano.
Kwa Kidato cha sita, alama endelevu ni
matokeo ya kidato cha tano kwa mihula yote miwili ni alama 15, muhula wa
kwanza wa kidato cha sita ni asilimia 10 na kazi za majaribio ni
asilimia tano.
Aidha, Baraza limebadili utaratibu wa
kupanga madaraja ya kufaulu, kutoka mfumo wa pointi na kuwa wa Wastani
wa Alama za Mtahiniwa (GPA).
Mfumo unaotumiwa sasa wa pointi,
huonesha wastani wa pointi alizopata mtahiniwa kwa masomo aliyofaulu
zaidi, na kupanga madaraja kuanzia la kwanza hadi la nne.
Madaraja ya mfumo wa GPA, hupangwa
katika utaratibu wa Distinction, Merit, Pass na Fail. Daraja la
Distinction ni la ufaulu wa juu zaidi na daraja Pass ni ufaulu wa chini.
Mtahiniwa hutunukiwa madaraja A, B+, B,
C, D, E au F kutegemeana na ufaulu wake katika somo ambapo uzito wa
alama katika madaraja A = 5, B+= 4, B = 3, C=2, D = 1, E = 0.5 na F = 0
Mtahiniwa atahesabiwa kuwa amefaulu somo, endapo atapata Daraja D ambayo
ni sawa na uzito wa alama moja.
Ukokotoaji wa jumla ya GPA ya mtahiniwa
hufanyika kwa kuzingatia masomo, ambayo mtahiniwa amefaulu angalau kwa
daraja D na kuendelea (D, C, B, B+ na A).
GPA anayopata mtahiniwa hutokana na
wastani wa pointi alizopata katika masomo saba aliyofanya vizuri zaidi
kwa Mtihani wa Kidato cha Nne au masomo matatu ya mchepuo kwa Mtihani wa
Kidato cha Sita.
Muundo wa madaraja ya GPA kwa kidato cha
nne, Distinction ni 3.6-5.0, Merit 2.6 -3.5, Credit 1.6-2.5, Pass
0.3-1.5, Fail 0.0-0.2 wakati Kidato cha sita ni Distinction 3.7-5.0,
Merit 3.0-3.6, Credit 1.7-2.9, Pass 0.7-1.6, Fail 0.0-0.6.
0 comments:
Post a Comment