WAKATI
muswada wa kupunguza misamaha ya kodi unatarajia kujadiliwa wakati
wowote, kuna hofu kwamba baadhi ya wabunge wamehongwa na wafanyabiashara
waliopiga kambi mjini hapa ili kuukwamisha.
Kuenea
kwa taarifa za kuhongwa kwa wabunge, zimemfanya Spika wa Bunge, Anne
Makinda, kuiita bungeni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) ili kuchunguza tuhuma hizo.
Taarifa
za kuwapo kwa wafanyabiashara hao zilianza kuzagaa tangu wiki iliyopita
wakati wabunge wakichangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2014/2015
inayofikia sh trilioni 19.2 ambapo idadi kubwa ya wabunge waliunga mkono
uamuzi wa serikali wa kutaka kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija kwa
taifa.
Katika
mijadala ya wabunge ikiwemo taarifa ya Kamati ya Bajeti, ilikuwa
ikilalamikia misamaha ya kodi ambayo kwa mwaka 2012/2013 ilikuwa sh
trilioni 1.5 na hadi Aprili mwaka huu ilifikia sh trilioni 1.4.
Tanzania
Daima ilidokezwa kuwa baadhi ya wabunge, wakiwemo wa Kamati ya Bajeti
wamegawanyika katika makundi mawili ambapo moja linataka isifutwe kwa
madai itawakimbiza wawekezaji na jingine linataka ifutwe ili taifa liwe
na mapato ya kutosha.
Katika
mijadala hiyo, Kamati ya Bajeti ilibainisha kuwa bajeti ya mwaka
2013/2014 ilikuwa na nakisi ya sh trilioni 2, hivyo kushauri kama
serikali itafuta misamaha isiyo na tija itachangia kuimarisha mapato
yake.
Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum, juzi alisema yupo tayari kwa mapambano na
wabunge waliodhamiria kukwamisha muswada huo kwakuwa amesikia kuna
waliojipanga kuuzuia ili kuwanufaisha wafanyabiashara.
Mkuya
alisema anashangazwa na harakati hizo za wabunge ambao kwa muda mrefu
wamekuwa wakiilaumu serikali, kwamba inapoteza fedha nyingi katika
misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa.
"Mimi
nitawashangaa sana wabunge mtakaopinga muswada huu wakati ndio nyinyi
mnaotaka maji, umeme barabara, hospitali katika majimbo yenu...
tumesikia kuna watu wanapita huko, lakini nataka niwahakikishie
nimejipanga kikamilifu," alisema.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana katika viwanja vya Bunge, Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, alisema wabunge wanapaswa kuwa kitu kimoja katika
kuunga mkono muswada huo kwakuwa ndio utakaosaidia serikali kuongeza
mapato yake.
Mwigulu
alisema wanashangazwa na misimamo iliyoanza kuonyeshwa na baadhi ya
wabunge kutaka kukwamisha muswada huo wakati wao ndio waliokuwa vinara
wa kutaka misamaha hiyo ifutwe.
"Kweli
hata sisi tunashangaa wenzetu wamepatwa na kitu gani kiasi cha kuanza
kuonyesha dalili za kutukwamisha, sisi tulidhani wenyewe ndio wangekuwa
mstari wa mbele kushangilia jambo hili, tunawaomba wasikubali ushawishi
wa wafanyabiashara wanaoranda randa hapa Dodoma.
"Tunajua
wafanyabiashara hawataki misamaha hii ifutwe, hivyo watafanya kila jambo
isifutwe, wabunge wawe makini sana na ushawishi wanaopewa na watu
hao..., nchi yetu inahitaji maendeleo, bila kodi hakuna maendeleo,"
alisema.
Spika Makinda azungumza
Akizungumza
na Tanzaia Daima, Spika wa Bunge, Makinda, alisema wabunge kukutana na
wafanyabiashara kuzungumzia muswada huo si dhambi kwakuwa wanapata fursa
ya kuelewa zaidi hatua itakayowasaidia kwenye maamuzi.
Alisema
ushawishi unaofanywa na wafanyabiashara si tatizo kwa sababu jambo
lolote zuri linaanza na ushawishi ambao huwawezesha wahusika kujua baya
na zuri la lile wanalotaka kulifanya.
"Hata
sisi humu bungeni tunashawishiana juu ya jambo fulani, lakini mwisho wa
siku kila mmoja ana uamuzi wake ambao unapaswa uangalie masilahi ya
taifa kuliko binafsi.
"Kila
siku ninapinga wabunge kufanya uamuzi kwa kufuata maslahi ya kundi
fulani la watu, bali ninataka wafanye kwa kuzingatia maslahi ya umma,
sasa kama wafanyabiashara wanawashawishi wabunge waukwamishe muswada na
wao wakafanya hivyo, hilo litakuwa jambo la kusikitisha sana," alisema.
Spika
Makinda, alisema anaikaribisha Takukuru kufanya uchunguzi wa tuhuma za
wabunge kuhongwa na wafanyabiashara ili wakwamishe muswada wa kufuta
misamaha ya kodi.
"Kama
wabunge wenzetu wanapewa rushwa ili wakwamishe muswada huu, naomba
Takukuru waje walifanyie kazi jambo hili, tunahitaji maendeleo kwa taifa
ambayo yanapatikana kutokana na kodi zinazolipwa," alisema.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment