TAFRANI iliyojitokeza bungeni juzi kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema kumuita Mbunge wa Kigoma
Kusini, David Kafulila(NCCR Mageuzi) tumbili, naye kumjibu kwa kumuita
mwizi imeingia katika hatua nyingine ambapo wawili hao wamekataa
kusuluhishwa. Jana asubuhi baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai,
kuahirisha shughuli za Bunge, Mwenyekiti wa Bunge, Mbunge wa Ilala,
Mussa Azzan ‘Zungu’, aliwakuta Werema na Kafulila wakiendeleza mzozo nje
ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Kutokana na hali hiyo, Zungu alijitolea
kuwapatanisha huku akijaribu kukaa katikati awashikishe mikono ili
yaishe, lakini hakufanikiwa. Lawama Wakati Zungu akifanya jitihada hizo,
Werema alilalamika.
“Mimi nina watoto na wajukuu unanitukana… kwani ninyi hamkusikia akinitukana?” Alihoji huku baadhi ya waandishi wakishuhudia.
Wakati Werema akilalamika kutukanwa huku
Zungu akiwa katikati yao, Kafulila naye alilalamika: “Wewe uliniita
mimi mnyama(Tumbili) kumbuka vizuri.”
Werema akijibu malalamiko ya Kafulila,
alisema yeye hakuwa na nia ya kumtukana bali alikuwa akielezea msemo wa
Wanyankole kuwa tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni na kukataa
kushikana mkono na Kafulila akisisitiza aombe radhi.
Kutokana na hali hiyo, Kafulila
aliondoka kutoka nje ya uzio wa ukumbi wa Bunge bila kuomba radhi huku
akimnyooshea kidole Werema, ambaye naye aliingia katika ofisi za Bunge
huku akilalamika kutukanwa na Kafulila.
Chanzo Juzi kabla ya kutoa kauli hiyo,
Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa muongozo ulioombwa na Kafulila kuhusu
fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT),
ambazo zimelipwa kampuni ya PAP, inayomiliki mitambo ya Kampuni ya
Independent Power limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila kwa kuwa fedha za Serikali hazikai katika akaunti hiyo.
Aliendelea kufafanua kuwa taarifa
zinazotolewa zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha kuilipa IPTL,
wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo kutokana
na misuguano baina ya wanahisa wawili waliokuwa wamiliki wa IPTL. Werema
alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe
huku mwingine akipinga juu ya jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na
kumaliza mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo
zipewe kwa mwanahisa mpya, PAP. Werema alisema kuna watu walileta
bungeni vipeperushi wakidai ni ushahidi kuhusu utoaji wa fedha hizo za
akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
“Kafulila ni miongoni wanaoeneza taarifa
potofu…, kama ni tuhuma au kuna rushwa itakuja kujulikana, tusubiri
uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
Tumbili Wakati akizungumza, Werema
alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi
unaosema kwamba tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni. Kabla ya
kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti alikuwa
akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa hivyo atangaze maslahi
yake.
“Naomba nisikilize hata kama ni mtuhumiwa nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali na yeye bila kuwasha kipaza sauti alisema:
“wewe (Werema) ni mwizi tu.” Zungu
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu alimuomba Jaji Werema
kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
(Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu alisema kwa kuwa Bunge lilishaamua
kuwa suala hilo lipelekwe Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ni vyema kama Kafulila ana ushahidi wowote, apeleke huko.
Baada ya kutoa muongozo huo, ambao
ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu alisitisha shughuli za Bunge
mpaka jioni na kuondoka huku akisindikizwa na makatibu wa Bunge na
wapambe kama kawaida.
Tafrani Hatua ya Mwenyekiti wa Bunge
kuondoka katika ukumbi baada ya kusitisha shughuli za Bunge, ilimpa
fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake na kutoka katika kiti
chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa
Mashariki, Sylvester Kasulumbai (Chadema), alihama katika kiti chake na
kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila. Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
baadhi ya mawaziri walimzunguka Jaji Werema kabla hajamfikia Kafulila na
Kasulumbai.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano
na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha- Rose Migiro, Naibu Waziri wa Afrika
Mashariki, Dk Abdullah Juma Saadalla na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene.
Nje ya Bunge, Kafulila na Mnyika
waliitisha mkutano na waandishi wa habari, ambapo walidai kuwa na
ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri kusema uongo bungeni kuhusu
fedha hizo za Escrow.
0 comments:
Post a Comment