Mwanamke
aliyetambuliwa kuwa ni Mariamu Said mkazi wa Kiwanja cha Ndege,
Morogoro juzi alishushiwa kipigo na wananchi kutokana na kumficha mtoto
wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne.
Tukio
hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi baada ya majirani zake kutoa
taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo
kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya boksi tangu akiwa na
umri wa miezi tisa.
Zongo alisema majirani hao walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa nje.
Baada
ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu
Mgagala na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo na kumhoji mwanamke
huyo ambaye alikuwa akijibu kwa kubabaika.
Moja
ya maswali aliyoulizwa ni idadi ya watoto wake na akajibu kuwa ana
wawili lakini wakati akiendelea kujibu maswali, ghafla mtoto huyo
alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa wasiwasi na kuamua
kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na kumkuta mtoto Nasra
akiwa ndani ya boksi.
Ofisa
mtendaji huyo alisema wakati wakimtoa mtoto huyo ndani ya nyumba, kundi
kubwa la watu waliokuwa na fimbo na mawe walianza kumshambulia mwanamke
huyo na kumlazimu mtendaji kutoa taarifa polisi.
Alisema
muda mfupi baadaye, polisi waliwasili na kumkamata Mariam na kumpeleka
katika ofisi ya kata ambako aliwekwa chini ya ulinzi.
Baadaye aliwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa Jamii.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema wanaendelea kukusanya
taarifa za tukio hilo ikiwamo matokeo ya vipimo vya madaktari kuhusu
afya ya mtoto huyo kabla ya kuchukua hatua zaidi.
Kamanda Paulo alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa kosa la kumfanyiwa mtoto vitendo vya kikatili.
Hata
hivyo, kamanda huyo alisema polisi wanakadiria kwamba mtoto huyo
alianza kufichwa kwenye boksi hilo akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.
Utetezi wa Mariam
Akijibu
maswali ya polisi, mwanamke huyo alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu
akiwa na umri wa miezi tisa baada ya mama wa mtoto huyo kufariki dunia
mwaka 2010.
Pia mtuhumiwa alikiri kwamba mtoto huyo hajawahi kupewa chanjo yoyote wala kupelekwa kliniki.
Alikuwa
akitoa maelezo hayo huku akiwa amemshikilia mtoto huyo aliyetapakaa
uchafu ikiwamo haja kubwa na ndogo alizokuwa akitoa ndani ya boksi na
kusema kwamba mara ya mwisho alimwogesha Julai mwaka jana.
Pia alisema alikuwa akimwekea chakula na maji ndani ya boksi lililokuwa nyuma ya mlango wa chumba.
Mume
wa mwanamke huyo, Mtonga Ramadhani anayefanya biashara katika Soko la
Mawenzi, Morogoro ambaye pia anashikiliwa na polisi, alidai kuwa hakuona
sababu ya kutoa taarifa za kufichwa kwa mtoto huyo kwa sababu hamhusu
na wajibu wake ni kutafuta chakula.
Alivyonaswa
Baadhi
ya majirani wa mwanamke huyo ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema
Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010 na hawajawahi kumwona
mtoto huyo akitolewa nje wala kufanyiwa usafi.
Walisema
mtoto huyo alibainika baada ya kusikika akikohoa na kulia nyakati za
usiku, jambo lililozua wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina
anayefuga misukule.
Baba wa mtoto
Baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi alisema hakujua kama mwanaye alikuwa analelewa katika mazingira hatarishi.
Akihojiwa
na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu, Mvungi
alisema alimzaa mtoto huyo nje ya ndoa na amekuwa akituma fedha za
matumizi kwa mama yake mkubwa.
Mvungi
ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alisema baada
ya mzazi mwenzake kufariki dunia alishindwa kumchukua mtoto wake kwa
sababu tayari alishakuwa wake.
0 comments:
Post a Comment