Kijana Ndaki Samola akiwa amepandishwa ndani ya gari la polisi kwa ajili ya kupelekwa kwa wataalamu ili kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya akili. |
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida mamia ya wananchi wa kijiji cha Ilebelebe
kata ya Itilima wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamefurika kushuhudia
tukio la kijana mmoja anayesadikiwa kuwa ni msukule aliyeibuka siku
moja baada ya kikongwe kuuawa kwa kucharangwa mapanga kwa imani za
kishrikina kijijini hapo.
Imeelezwa
kuwa siku ya mazishi ya Kikongwe huyo Mei 27 mwaka huu ndipo kijana
huyo anayedaiwa kuhifadhiwa na kikongwe huyo alikutwa na wananchi nyuma
ya nyumba ya kikongwe huyo saa tatu usiku akizunguka na kusikika akisema
kaamua kutoka nje baada ya kukosa chakula.
Walioshuhudia
tukio hilo walisema Kijana Ndaki Samola anayedaiwa kuwa ni msukule
akizungumza kwa shida alisema anatoka kijiji cha Bubale kata ya Samuye
wilaya ya Shinyanga na alifika kijijini hapo kwa ajili ya kuoa.
Kijana
huyo akizungumza bila ya kufafanua ni kipindi gani amekaa katika kijiji
hicho alidai alikuwa akiishi kwenye nyumba ya bati ya kikongwe huyo na
wenzake wawili na kwamba kutokana na njaa yake ndiyo kaamua kutoka.
Mwenyekiti wa
kijiji cha Ilebelebe Thomas Nkindo alisema tukio hilo limewashangaza
kwani kijana huyo hajawahi kuonekana kijijini hapo hata siku moja ,hali
ambayo imewapa wasiwasi wananchi kutokana na maneno aliyoeleza kwamba
alikuwa kwenye nyumba ya kikongwe huyo ambayo ilikuwa imefungwa kwa muda
mrefu na haitumiki.
“Baada
ya kuhojiwa na jeshi la jadi sungusungu kijana, alidai kilichomtoa
ndani ni njaa na kawaacha wenzake wawili mmoja akiwa ni mwanamke,na
alikuja kwa ajili ya kuoa na kufikishiwa kwenye nyumba hiyo ya tope
ambayo imeezekwa kwa bati iliyokuwa ikimilikiwa na marehemu”,alieeleza
Nkindo.
Akifafanua
zaidi kuhusu tukio hilo afisa mtendaji wa kijiji cha Ilebelebe Emmanuel
Asili alisema marehemu Nyanzala Basu kabla ya kufikwa na mauti siku
hiyo ya tukio asubuhi alikuwa amealika wanawake, ambao walifanya kazi ya
kumsaidia kukata viazi maarufu kama michembe ndipo usiku huo huo
alivamiwa na kuuawa majira ya saa 1.30 wakati akimpatia mbwa wake
chakula.
“Kilichotushtua
zaidi huyo kijana Ndaki alikuwa ananukia harufu ya nyama wakati
tunamuona na ukizingatia mchana kwenye mji huo ulipokuwa msiba walikuwa
wamechinja mbuzi,moja kwa moja wananchi walimtilia mashaka inawezekana
akawa ni msukule kwa kulinganisha na maelezo yake “alisema Asili.
“Kutokana
na mashaka hayo tulitoa taarifa kwa jeshi la polisi huku tukimhifadhi
kijana kwa muda katika ofisi yangu uangalizi zaidi na polisi walipofika
walizungumza na wananchi na kuamuru mlango wa nyumba hiyo uvunjwe ili
kuona kilichomo ndani wakakuta beseni,ndoo na bati
lililochakaa”,alieeleza afisa mtendaji wa kijiji.
Akizungumza
na wananchi mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Kishapu ASP Samwel
Kijenga aliwataka kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu waliosababisha
mauaji hayo ya kinyama huku akiwataka kuondoa wasiwasi kuhusu nyumba
waliyokuwa wakihofia kwani wameangalia hawajaona kitu hivyo waendelee na
shughuli za maendeleo.
Hata
hivyo wakati kijana huyo akiwa tayari amepandishwa ndani ya gari la
polisi kwa ajili ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi kama ana matatizo ya
akili,alitokea mwanamme aliyejitambulisha kwa jina la Nyalali Chaba
mkazi wa kijiji cha Ikoma wilayani Kishapu na kudai kuwa anamfahamu ni
mdogo wake anasumbuliwa na tatizo la akili ndipo polisi wakamkabidhi kwa
maandishi.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga SACP Evarist Mangalla amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo la mauaji ya kikongwe na tayari watu wanne
wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi wakati wakiendelea na
upelelezi
0 comments:
Post a Comment