WABUNGE
wamesema hali ya elimu nchini ni mbaya na kumshauri Rais Jakaya Kikwete,
kuunda Tume ya Kudumu ya Elimu ili kuangalia ubora na kudhibiti sekta
hiyo muhimu.
Katika
michango yao kwenye mjadala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
uliotarajiwa kuhitimishwa jana jioni, wabunge wamesema suala la elimu
halina siasa, na nchi isipochukua hatua sasa, itakuwa hatari kwa vizazi
vijavyo.
Mbunge wa
Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alieleza matatizo kadhaa katika
mitihani ya Darasa la Saba pamoja na ule wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)
na kudai kuwa “kuna madudu makubwa.”(Martha Magessa)
Mbatia
aliyekuwa ameshika nakala za mitihani hiyo na baadaye kuiwasilisha kwa
Naibu Spika, Job Ndugai, alidai baadhi ya mitihani hiyo ni migumu na
imewashinda maprofesa wa vyuo vikuu.
Profesa,
dau “Mimi niliwapatia mitihani hii maprofesa wa vyuo vikuu, imewashinda.
Niliwapa huu wa Hisabati, akanirudishia akisema mtihani wenyewe
haufanyiki. “Sasa kama yupo mtu humu atamudu kuufanya na kupata alama
mia moja, nampa milioni kumi,” alisema Mbatia, huku Naibu Spika akieleza
kuwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo yuko tayari kuufanya. “Profesa
Muhongo ni profesa wa miamba, kama ataweza huu hapa aje achukue,”
alitamba Mbatia.
Mbatia alisema elimu ya Tanzania ni dhaifu na nchi imeshindwa katika elimu na kuwa suala hilo si la chama cha siasa.
Akitoa
majawabu ya hoja zake, Mbatia alimshauri Rais kuunda Tume ya Kudumu ya
Elimu, ambayo pamoja na mambo mengine, alisema itaangalia ubora na
kudhibiti elimu nchini.
Msomi
huyo alitaka pia Tume hiyo ifanye kazi ya kuandaa mitaala, kuhariri
vitabu akisema Tanzania haina wahariri wa vitabu kama ilivyo kwa vyombo
vya habari vyenye wahariri wa aina mbalimbali.
Alizitaja
kazi nyingine kuwa ni kufanya utafiti wa kisayansi, kuamua lugha ya
kufundishia na kuangalia kwa ujumla tatizo la kushuka kwa elimu.
Alisema
elimu siyo bidhaa ya kuuzwa sokoni, bali iwe huduma na kukerwa na kodi
nyingi katika elimu na gharama za ada kwa shule binafsi.
“Ni
lazima tuukubali ukweli na kukabiliana nao. Elimu yetu imeshuka. Watoto
wa walalahoi watapata tabu, kama hatukuisimamia hili, tutapata tabu
katika miaka 20 au mia ijayo hasa wakati huu wa sayansi na teknolojia,”
alisema Mbatia.
Mbunge wa
Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), aliyesema kuwa elimu iko katika
chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalumu (ICU). Kama Mbatia,
Serukamba alishauri kuanzishwa kwa Tume ya kujichunguza kuhusu
kuporomoka kwa elimu nchini, akisema “tukubali waseme, tujisahihishe.”
Alisema
suala hilo si la mtu mmoja, na kuacha siasa na kuongeza kuwa kama kuna
jambo “tunacheza nalo, basi ni elimu, tunaua kizazi kijacho.”
Alisema
si vyema kutatua tatizo la elimu kwa kuangalia leo tu, bali uwepo
mkakati wa dhati wa muda mrefu, na kutolea mfano Marekani ilivyopitia
mfumo wake wa elimu mwaka 1981.
Ada kubwa
Kwa upande wake, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza (CCM),
ambaye anamiliki shule kadhaa nchini, alisema kuna tatizo la shule
binafsi kulundikiwa kodi nyingi, na ndio manaa zinatoza ada kubwa.
“Kuna
sijui kodi ya mapato, PAYE, majengo, SDL, yaani ni michango, michango,
kodi. Kwa staili hii, ada inapanda, baadaye shule inakufa,” alisema
Rweikiza.
Aidha,
kama walivyopendekeza wabunge wengine waliochangia jana, mbunge huyo
alitaka ukaguzi utiliwe mkazo, akitoa mfano kuwa shule zake
hazijakaguliwa tangu mwaka 2005.
Mbunge wa
Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM), alisema kwa sasa hakuna Wizara ya
Elimu baada ya kuondolewa kwa shule za msingi na sekondari.
Badala
yake, akashauri wizara hiyo ibaki kuwa kitovu cha mawazo bora ya elimu
kama ilivyo Tume ya Mipango kuhusu masuala ya mipango.
Said Arfi
wa Mpanda Mjini (Chadema), licha ya kuzungumzia ukaguzi, alisema bajeti
ya elimu imezidi kutegemea wahisani ambao hawatekelezi ahadi zao.
Nyambari
Nyangwine wa Tarime (CCM), ambaye ni mtunzi wa vitabu, alipendekeza
kuanzishwa kwa Shirika la Uchapaji, kwani vitabu ni moja ya maeneo
yanayochangia mporomoko wa elimu nchini.
Mbunge wa
Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) alisema mazingira mabovu, ukaguzi
kuachwa, shule kukosa maabara na kushuka kwa morali ya walimu,
kumechangia kushuka kwa elimu nchini.
Muundo
Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msolla (CCM), alitaka masuala ya shule
za msingi na sekondari yabaki katika wizara hiyo na irejeshwe wizara ya
kusimamia elimu ya juu, huku akisisitiza kuwa upangaji madaraja ni
angamizo katika elimu nchini.
Naibu
Spika Ndugai naye alipendekeza masuala ya elimu yaondolewe Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na
kurejeshwa kwa wizara hiyo ili yasimamiwe vyema.
Kambi
Rasmi ya Upinzani ilisema kuwa malengo na mikakati yote iliyoainishwa ni
mizuri, lakini “tunadhani mikakati hiyo imekuwepo muda mrefu,
kilichokosekana ni utekelezaji na ufuatiliaji wake.”
Msemaji
wake, Susan Lyimo alishauri mikataba ya utendaji kazi katika kila ngazi
ya elimu iwekwe wazi ili atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ijulikane
atawajibika vipi. LIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPA
0 comments:
Post a Comment