Thursday, 29 May 2014

MAASKOFU, FREEMASON...

...
BAADHI ya viongozi wa dini nchini wamesema kwamba Watanzania wengi wamekuwa na imani na mambo ya kishirikina wakiamini kuwa wanaweza kubadili maisha kwa njia ya kuwa wanachama wa Imani ya Freemason badala ya kutumia akili huku wakiweka imani kwa Mungu. Akizugumza kupitia Radio Wapo FM, Rais wa WAPO Mission International, Askofu Sylvester Gamanywa amesema Januari 14, mwaka huu alitangaza Oparesheni Milikisha ambaypo watu wanaweza kuwa matajiri lakini cha ajabu alitafsiriwa kuwa ametoka  nje ya imani ya kanisa kwani anahubiri utajiri na kwamba yeye ni Freemason.
Alisema mawazo hayo ya Freemason ni sifa ya kwanza ya ushirikina kwa sababu mtu anayefikiri  na kuamini katika Freemason ni athari za ushirikina.
“Mtu kuwa na mawazo ya Freemason ndiyo sifa ya kwanza ya ushirikina kwa sababu anayeamini na kufikiri katika Freemason ndiyo athari za ushirikina tena ushirikina ulio ndani ya kanisa,” alisema Askofu Gamanywa.
Aliongeza kuwa ushirikina wa Freemason ndani ya kanisa ni mbaya kwa sababu ungekuwa unafanyika Maneremango au Sumbawanga angesema hiyo ni jadi yao.
Alisema ushirikina wa Freemason unapofika kanisani ndipo wanaposema kuwa kunahitajika msaada na akabainisha kuwa kutokana na hilo ameamua kurudi katika falsafa ya ukombozi.
Akifafanua zaidi kiongozi huyo wa kiroho alisema falsafa ya ukombozi imebeba mambo matatu ambayo Yesu aliyafanya akiwa msalabani ambapo alibeba dhambi ili wanadamu wawe huru na dhambi.
Aliongeza kuwa, Yesu aliua magonjwa yote ili wanadamu wawe na afya njema na alifanyika maskini wa kipato kwa mujibu wa Biblia ili watu wasiwe maskini wa kipato kwa njia yake.
Aliongeza kuwa mambo hayo ndiyo yaliyomleta Yesu duniani na ndiyo yaliyosababisha asulubiwe msalabani na yalitakiwa yawe kipaumbele cha fundisho la imani katika jamii ya Kikristo ulimwenguni.
“Lakini watu walewale wanaopinga habari za ukombozi wa Yesu Kristo wanaamini katika shetani zaidi kuliko Mungu na nguvu zake, ndiyo maana nikaona nirudi katika falsafa ya ukombozi.
“Nimegundua kumbe ugonjwa wa Tanzania ni uwezo mdogo wa kufikiri, mtu akiona kuna mpango mzuri wa kuwatoa watu katika dhiki wanasema ni Freemason.
“Kwani hao Freemason wanakaa mtaa gani ambao kama kazi yao ingekuwa kuwasaidia watu naamini wengi wangekuwa wameshabadilika lakini hakuna utafiti au hatua za kutafuta mabadiliko,”alisema.
Akaongeza:
“Watu hawataki kutafuta, wanataka waombewe kisha wapate utajiri lakini kila jambo linahitaji juhudi ili upate na nina uwezo wa kupunguza idadi ya watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri baada ya majini kuondolewa na takataka za pepo na ufumbuzi wa yote upo katika kufikiri.”
Alisema Tanzania imekuwa nchi inayoongoza kwa ushirikina na imeipiku Nigeria kutokana na mauaji ya albino na kikombe cha Babu Mchungaji Ambilikile Masapila ambacho kimeichafua nchi na kuifanya kuongoza Afrika kwa mambo ya kishirika.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakaria Kakobe amekiri kuwa baadhi ya Watanzania wanaamini ushirikina wa Freemason kuliko mambo ya Mungu.
“Uliona kikombe cha Babu kilivyotetemesha nchi, viongozi wakuu wa nchi na watu wa kawaida wote walikuwa wakikimbilia Samunge kwa Babu.
Nilijitahidi kukemea na nyinyi (Gazeti la Uwazi) mlijitahidi kuelimisha, watu wakawa wanazidi kwenda,”alisema Askofu Kakobe.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema aliwaambia watu kikombe kile ni cha shetani lakini hakuna aliyesikia na badala yake viongozi wa kitaifa wakawa wanakwenda na kuhamasisha watu kufuata ushetani.
Askofu Kakobe alisema wakati umefika kwa wanadamu kuachana na mambo ya Freemason na yale yote ya kishirikina na kurejea kwa Mungu na ndivyo maandiko matakatifu yanavyosema.
Alisema haamini kama kuna mtumishi wa Mungu ambaye anaweza kuchanganya mambo ya kishetani na ya Mungu na Mungu akamuacha hivihivi.
“Huwezi kumtania Mungu akakuachia, Mungu ana njia zake za kumfikia na hakuna njia ya mkato, nawahimiza watu wazifuate kwa kuokoka,” alisema.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Nabii George David Geordavie wa Kanisa la Ngurumo za Upako la Arusha, Gaudensia Luila alisema ni vigumu kwa kiongozi wa dini kujihusisha na Freemason.
“Viongozi wengi wa dini hupata utajiri kutokana na sadaka za waumini wao na siyo mambo ya Freemason kama wengi wanavyofikiri.
Ni kweli kwamba siyo vizuri kiongozi wa kidini kuwa na maisha ya kifahari huku waumini wake wakiwa hoi kimaisha. Nampongeza Askofu Gamanywa kwa mikakati yake ya kuinua watu kimaisha,” alisema.
Naye Makamu Askofu Mkuu wa TAG, Magnus Mwiche alisema ni aibu na fedheha kwa kiongozi wa dini kuonekana ana mali nyingi wakati waumini wake wanateseka.
“Sisi kama viongozi wa dini ni kondoo wa Mungu na tupo duniani kwa kuongoza wanadamu wenzetu ili wauone utukufu wa Mungu, kiimani, kiuchumi. Neno la Mungu lisichanganywe na mambo ya kishirikina au Freemason,” alisema.
Mchungaji Imani Mwakyoma wa TAG ameshauri kuwa ni vyema viongozi wa dini wote kuhakikisha wanawainua wafuasi wao  kiimani, kiuchumi na kiroho.
“Ni aibu  na fedheha kwa kiongozi anayemiliki kanisa kuwa milionea wakati wafuasi wake ni mafukara wa kutupa,” alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji Seguye alisema kauli mbiu ya Rais Jakaya Kikwete ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania inawezekana na ni lazima iheshimike na wao viongozi wa dini wanafanya kila njia ili waumini wao wawe na maisha bora.
“Mikakati inayofanywa na baadhi ya viongozi wa dini kuinua maisha ya waumini wao na Watanzania inapaswa kuungwa mkono na kila sekta na isitafsiriwe kuwa ni Ufreemason.”

Hivi karibuni Mzee wa Upako, Mchungaji Antony Lusekelo taulo lake alilokuwa akilibeba madhubahuni liliwahi kuhusishwa na Freemason lakini akafafanua kuwa alikuwa akilitumia kufutia jasho tu na alilazimika kuzivua pete zake kwa kuhusishwa na jamii hiyo ya mambo ya siri.
 
Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger