KIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
Shina Namba 30, Kigamboni Kisiwani jijini Dar, Bernadetha Shabani (53)
amefariki dunia baada ya kupigwa shoka la kichwa na anayedaiwa kuwa ni
mpangaji wake aliyefahamika kwa jina la Shija Ng’waya (33).
Tukio hilo la kikatili lilijiri Mei 5,
mwaka huu nyumbani kwa marehemu, Kigamboni jijini Dar es Salaam na
marehemu alizikwa Mei 6.
Akizungumza na Uwazi kwa uchungu katika
msiba wa marehemu huyo mwishoni mwa wiki iliyopita, mtoto wa marehemu,
Ester Shija (hakuna undugu na mtuhumiwa) alisema mlalamikiwa huyo
alikuwa mpangaji wao kwa mwaka mmoja akahama.
lisema baada ya muda, mtuhumiwa alirudi kwa marehemu mama yake na kudai kuna vitu vyake aliviacha kwenye chumba.
“Mama alimuuliza ni vitu gani akasema
mwiko, tambi za jiko la Mchina, tochi na redio ndogo. Mama alimwambia
hakuviona pengine watoto walivichezea. Shija akasema yeye anachotaka ni
vitu vyake, akaondoka na kuahidi kurudi siku nyingine.
“Kweli, alirudi tena siku nyingine na kumdai mama vitu vyake na akasema vikikosekana atamuua kisha akaondoka.
“Mama alikwenda kutoa taarifa kwa
mwenyekiti wa serikali ya mtaa (hakumtaja jina). Shija akaitwa na
kuulizwa ni vitu gani? Akavitaja na kusisitiza kama asingevipata
angemfanyia kitu kibaya mama. Mwenyekiti aliripoti polisi kutokana na
vitisho hivyo.
“Awamu nyingine, Shija alikuja nyumbani
akiwa uchi wa mnyama na kudai vitu vyake. Siku hiyo akasema kama
hatavipata lazima aue, mwenyekiti akaenda tena polisi, wakaja kumchukua
lakini haukupita muda alikuja akamwambia mama, ‘nimetoka na ni lazima
nitakuua.’
“Siku nyingine tena Shija akaja. Hii ni
mara ya nne, tena alikuwa uchi. Akasema amefuata vitu vyake, mama
akampigia simu mwenyekiti na kumtaarifu, akaja na wajumbe wengine wa
serikali na kamati ya ulinzi ya kijiji wakamchukua Shija mpaka ofisini
kwao, wakamuuliza kama alikuwa tayari kulipwa fedha akavinunue vitu
hivyo, akasema yuko tayari kama atapewa shilingi milioni 3.
...Mazishi.
“Mama alimwambia kutokana na maisha yake
yalivyo anamuomba amlipe shilingi elfu sabini, Shija akanyanyuka na
kuuambia uongozi, ‘mnaona mama huyu alivyo na dharau, hiyo hela haitoshi
thamani ya vitu hivyo, nitamuua tu,’’ alisema mtoto huyo akimkariri
mtuhumiwa na kulia.
Naye mtoto wa pili wa marehemu, Sofia
Mabula alisema: “Shija alifungwa kifungo cha nje cha miezi sita kutokana
na makosa yake lakini cha ajabu ndani ya mwezi mmoja akatimiza lengo
lake la kumuua mama.
“Sidhani kama mahakama ilistahili
kumfunga kifungo cha nje maana alimtishia mama zaidi ya mara nne mwisho
wa siku akamuua kweli, inauma sana.”
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa
aliyejitambulisha kwa jina moja la Zakaria ‘Waiti’ alisema aliposikia
kwa mara ya kwanza kuhusu madai ya vitu hivyo. Alijiuliza vilikuwa na
nini cha zaidi!
...Waombolezaji.
“Niliwahi kumuuliza mtuhumiwa kwa nini
aling’ang’ania vitu hivyo, akasema alipewa na babu yake ambaye kwa sasa
ni marehemu na vifaa hivyo vilikuwa vinamsaidia katika maisha yake kwani
vina nguvu ya ziada ndani yake,” alisema mwenyekiti huyo.
Akaongeza: “Alisema tochi kazi yake
ilikuwa kuwatibu watoto wadogo wenye mtoto wa jicho, mwiko ulikuwa wa
mti wa Mkula ambapo alikuwa akipikia chakula unampa nguvu za kulima.
Kuhusu redio ilikuwa ikimsaidia kusikiliza matatizo ya watu.
Askari wa JWTZ aliyejitambulisha kwa
jina la Koplo Deus wa Kikosi cha Wanamaji, Kigamboni ndiye aliyemkamata
mtuhumiwa wakati akikimbia kwa kujitumbukiza kwenye Bahari ya Hindi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke,
SACP Alibert Kiondo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema
mtuhumiwa yuko mikononi mwa polisi, uchunguzi unaendelea ili kujua
utimamu wa akili yake.
0 comments:
Post a Comment