Saturday, 17 May 2014

WASSIRA AWATISHA UKAWA

...

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wassira amewatisha wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba wasiporejea bungeni, kanuni zitabadilishwa na Bunge litaendelea.
Wassira alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu hoja za wabunge mbalimbali akiwamo Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuwa majadiliano ndani ya Bunge la Katiba yanakiuka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.(Martha Magessa)
Katika mchango wake, Mdee alisema Ukawa hawako tayari kurejea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba Agosti, mwaka huu endapo majadiliano ya Katiba hiyo hayatajikita kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba.
Hata hivyo, Wassira akijibu kauli hiyo ya Mdee na wabunge wengine waliopaza sauti kuhusu kukiukwa kwa sheria hiyo alisema: "Kama hamrudi tutatumia kanuni zile kutafuta akidi na Bunge litaendelea."
"Tusigeuze Bunge hili kuwa Bunge la Katiba... Bunge la Katiba lipo tena lipo kisheria.... Kuna watu wanageukageuka wanasema sheria ilivunjwa, lakini hawasemi kifungu gani kilivunjwa," alisema Wassira.
Wassira alisema wajumbe wa Bunge la Katiba walitunga Kanuni za Bunge hilo na miongoni mwa waliokuwa walimu wa kanuni hizo alikuwa Ismail Jussa na Tundu Lissu ambao ni wajumbe wa Ukawa.
"Kanuni tuliyotunga ambayo haipingani na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni Bunge hilo kuwa na mamlaka ya kubadili, kurekebisha, kuboresha na kadhalika," alisema Wassira na kuongeza:
"Sasa leo wenzetu baada ya kuamua kutoka wanasema tunavunja sheria eti kwa sababu tunapingana na mawazo ya wananchi. Hiyo siyo sawa. Tunapingana na maoni yapi ya wananchi?
Wassira alisema kama ni hoja ya maoni ya wananchi, upande wa Zanzibar asilimia 60 walitaka Serikali ya mkataba lakini rasimu iliyopo mbele ya Bunge Maalumu la Katiba haina mapendekezo ya mkataba.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliwasihi wajumbe wa Ukawa warejee bungeni, akisisitiza kuwa Katiba Mpya itapatikana kwa maridhiano na si kwa wajumbe kuasi Bunge.
Mabilioni Bunge la Katiba utata
Wabunge wa upinzani wamehoji kiasi cha fedha kilichotumika kugharimia awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba. Kuhoji huko kumetokea wakati, Wizara ya Katiba na Sheria ikisema Sh21 bilioni zimetengwa kwa ajili ya awamu ya pili ya Bunge la Katiba linalotarajia kuanza vikao vyake Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger