Rais
Jakaya Kikwete akiangua kicheko wakati walimu (juu), walipokuwa wakipita
kwa maandamano, huku wakiimba ‘Shemeji mshahara bado’ wakati wa sherehe
za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika Uwanja wa Uhuru jijini
Dar es Salaam jana. Walimu walimwita shemeji kwa kuwa mkewe, Salma ni
mwalimu kitaaluma. Picha na Silvan Kiwale.
Dar/mikoani. Rais
Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili za kuwafurahisha wafanyakazi. Kwanza
ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao na pili, kupunguza kodi
inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi kutekelezwa
katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi
karibuni.
Akizungumza
kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika
kitaifa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema anatambua kuwa
wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali itasema nini kuhusu masilahi
yao.
Alisema
malalamiko ya wafanyakazi wengi ni kutaka kuona kima cha chini cha
mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye mishahara (Paye), ikipungua.
“Mimi na
wenzangu serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kufanya hivyo,
tumethibitisha miaka iliyopita na tutaendelea kuwa hivyo,” alisema.
Huku
akishangiliwa na wafanyakazi waliofurika katika Uwanja wa Uhuru, Rais
Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama
wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa
nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa Serikali inatumia asilimia
44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua
namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa kuongeza mishahara kwa mwaka huu,
Rais Kikwete alisema kulikuwa na mjadala mkali baina ya wafadhili
waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli
mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa mishahara ni midogo, lazima
tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima ukitoe ili uijenge ile
nafuu, alisema bila kutaja kiwango kitakachoongozwa.
“Hata
sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara ya Utumishi na Hazina
kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi gani, nikaingilia kati
nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa wanataka ipingue kidogo,”
alisema.
Walimu na shemeji yao
Suala la
mshahara lilijitokeza kwa namna nyingine kwenye maandamano ya
wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele ya jukwaa kuu na
kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji yao, kwamba
hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujapata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,” walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo.
Tofauti
na wafanyakazi wengine ambao walipita mbele ya mgeni rasmi bila
kusimama, walimu walisimama kwa dakika moja kuhakikisha ujumbe huo
unamfikia.
Wakati
hayo yakitokea, Rais Kikwete na viongozi wengine walikuwa wakicheka huku
wakiwaangalia walimu hao waliokuwa wakiendelea kuimba wimbo huo.
Ajira kwa wageni
Rais
Kikwete aliagiza yafanyike marekebisho kwenye sheria ya vibali vya ajira
ili kudhibiti ongezeko la wafanyakazi wa kigeni nchini ambao wanafanya
kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Aliagiza
hatua hiyo itekelezwe haraka hata ikibidi kwa kupeleka bungeni hati ya
dharura ili kuhakikisha jambo hilo linaanza mara moja.
Malalamiko ya Tucta
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya
alisema pamoja na ongezeko la mishahara kufanyika kila mwaka, limekuwa
dogo mno kiasi cha kushindwa kufikiwa kima cha chini ya mshahara
kinachotakiwa.
Alisema
kwa upande wa sekta binafsi, Serikali imeongeza mshahara kutoka
Sh100,000 hadi Sh450,000 mwaka jana, huku sekta ya kilimo ikiwa ya
mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini zaidi.
“Hali hii
imesababisha kuwapo kwa upungufu mkubwa wa wafanyakazi mashambani na
hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao,” alisema na kuongeza:
“Tunapenda
kuikumbusha Serikali kwamba kumlipa mfanyakazi mshahara unaokidhi
mahitaji muhimu ya maisha siyo jambo la fadhila, bali ni mojawapo ya
haki za msingi za binadamu zinazosisitizwa na jumuiya za kimataifa.”
Tanga
Mkuu wa
Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtassiwa alisema Serikali inatambua changamoto
zinazowakabili wafanyakazi zikiwamo za kodi ya mishahara kuwa juu na
kwamba inazifanyia kazi.
Mratibu
wa Tucta Mwanza, Evarist Mwalongo ameutaka uongozi wa mkoa kuwachukulia
hatua za kisheria waajiri wasiofuata sheria za kazi huku akiitaka
Serikali kubadilisha sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ili itoe
mafao mazuri kwa wastaafu na kiwango cha kodi kwenye mshahara kipungue
hadi asilimia moja.
Mara
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Henjewelle amewaagiza waajiri kuwalipa
wafanyakazi masilahi yao kwa wakati ili kuepusha migogoro ya mara kwa
mara kazini.
0 comments:
Post a Comment