MBU Aedes au Aedes aegypti ni wadudu wenye mabawa mawili na miguu sita kutoka familia ya Culicidae.
Mbu huyo
asili yake ni Afrika lakini hivi sasa amesambaa sehemu mbalimbali
duniani hasa sehemu za tropiko na anapatikana majira yote ya mwaka hasa
sehemu zenye maji maji. Machapisho mbalimbali ya kimataifa ya utafiti wa
kisayansi kuhusu mbu huyo yanaeleza kuwa amekuwepo kwa zaidi ya miaka
milioni 150 iliyopita na kusabisha maradhi kwa binadamu wa kale.
Utafiti
wa awali uliofanywa na mwanasayansi Fredric Hasselquist mwaka 1757
ulitaja mbu huyo kwa jina la Culex aegypti. Jina la Aedes aegypti
lilianza kutumika mwaka 1920 na lilianzishwa na mwanasayansi Harrison
Gray Dyar, Jr. Aedes ni mbu anayeeneza virusi vinavyosababisha ugonjwa
maarufu kwa jina na chikungunya, homa ya manjano na homa ya dengue
ambayo hivi sasa inaenea kwa kasi katika jiji la Dar es Salaam.
Mbu Aedes
ni miongoni mwa wadudu walioko katika hali ya metamofisisi ambao maisha
yao hupitia hatua nne zinazowafanya kuwa na tabia na maumbo tofauti
ambazo ni yai, lava, pupa na mbu kamili. Unaweza kumtambua mbu huyo kwa
kuwa ana mistari meupe miguuni.
Tofauti
na mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao huuma usiku, mbu wa homa ya
dengue huuma mchana na usiku.Taarifa za kisayansi zinaeleza kuwa mbu
jike ndiye hasa anayeuma na kueneza kirusi cha homa ya dengue wakati
akifyonza damu katika mwili wa binadamu.
Mbu jike
hutumia damu kama lishe kuu ili aweze kurutubisha mayai yake ili
kuendeleza kizazi cha mbu hao. Baada ya kunyonya damu ya kutosha mbu
jike huweza kutaga mayai 100 hadi 200 kwa uzao mmoja. Jike anaweza
kutaga mara tano katika kipindi cha uhai wake.
Mbu
aliyepevuka huishi kwa wastani wa wiki mbili hadi mwenzi moja hivyo mbu
mmoja aweza kutaga mayai kati ya 500 hadi 1,000 kwa kipindi cha wiki
mbili hadi mwenzi mmoja. Wingi wa mayai unategemea kiasi cha damu
aliyopata kwa kuwa kadiri anavyopata damu nyingi ndivyo anavyotaga mayai
mengi zaidi.
Ingawa
mbu huyo anataga mayai 200 katika uzao mmoja, hutaga mayai sehemu
tofauti ili kuzuia kizazi chache kisiangamie kwa urahisi endapo adui
atavamia mayai hayo. Mayai ya mbu aina ya Aedes yana umbo la mviringo
uliochongoka, yana gamba laini na urefu wa milimita moja. Mbu anapotaga
hutoa mayai meupe ila baada ya dakika chache hubadilika na kuwa na rangi
nyeusi.
Mbu hawa
hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au
hata ndani ya nyumba. Mbu huyo anataga kwenye madimbwi ya maji hasa
sehemu yenye mafuriko, kwenye mapango ya miti, sehemu zenye mashimo au
mapango yaliyotengenezwa na binadamu.
Pia
wanataga mayai hao kwenye mapipa, vyungu na makopo ya maua, kweye chupa
na makopo yaliyotupwa ovyo, matairi ya gari, vifuu vya nazi, matambara
katika viambaza vya nyumba na sehemu zozote zile zenye upenyo hasa
katika lundo la uchafu katika viambaza vya nyumba.
Mayai
hayo huanguliwa kwa siku tofauti kulingana na hali ya hewa na mazingira
ya eneo husika. Sehemu yenye joto kama Dar es Salaam mayai huanguliwa
katika siku mbili tu lakini sehemu zenye baridi mayao huchukua hadi siku
saba kabla ya kuanguliwa. Mayai ya mbu wa homa ya dengue hayaanguliwi
yote kwa wakati mmoja, wakati wa kuanguliwa yanaweza kupishana saa
chache au siku nzima kulingana na mazingira ya eneo husika.
Kupishana
huko huwezesha kizazi cha mbu kuwepo wakati wote katika majira ya mwaka
ikiwa eneo husika litakuwa na hali ya maji maji. Mayai ya mbu
anayeeneza ugonjwa wa dengue yanauwezo wa kuhimili hali ya hewa na kukaa
muda mrefu bila kuharibika. Ikiwa mayai hayo yametagwa wakati wa
kiangazi yanaweza kukaa zaidi ya mwaka mzima bila kuanguliwa kisha
huanguliwa kipindi cha mvua ili kiluilui waweza kuishi na kukua vyema.
Kitendo
cha yai kukaa muda mrefu kinasababisha changamoto katika harakati za
kumuangamiza mbu huyo mwenye uwezo wa kudhuru na hata kuua binadamu ili
waweze kuendeleza kizazi chake. Baada ya mayai kuanguliwa viluwiluwi vya
mbu huishi kwa kula chembechembe zinazopatikana kwenye maji.
Baadhi ya
chembechembe ni ndogo sana haziwezi kuonekana kwa macho bila msaada wa
darubini. Viluwiluwi hao huogelea kwenye maji na wakati mwingine huja
juu ya maji. Wanaweza kuishi kwenye kina kifupi cha maji ndio maana
wanaweza kuzaliana kwenye makopo ya maua yanayoruhusu maji kutwama,
kwenye vifuu vya nazi na maeneo mengine yanayohifadhi maji kwa muda
mrefu.
Viluwiluwi
wanakua kulingana na hali ya hewa, endapo kuna hali joto anaweza kukua
kwa muda mfupi katika siku moja ila kama kuna hali ya ubaridi na maji ya
kutisha anaweza kubaki kwenye maji hata kwa zaidi ya mwenzi mzima. Lava
aliyekomaa huwa na urefu wa milimita nane. Mbu dume hukua haraka zaidi
hivyo hubadilika na kuwa mbu kabla ya mbu jike.
Hatua ya
kukua yaani yai, lava na pupa huchukua muda mrefu ikilinganishwa na muda
ambao pupa anapobadilika na kuwa mbu kamili. Mbu aliyepevuka anaweza
kuishi kwa wastani wa wiki mbili hadi mwezi mzima na kusababisha maradhi
mbalimbali yanayotokana na homa ya dengue.
Inaelezwa
kuwa neno dengue linatokana na neno la lugha ya Kihispania
linalomaanisha homa kali pia baadhi ya watafiti wanasema limetoholewa
kutoka na lugha ya Kiswahili “Dinga” ambalo hutumika kuelezea ugonjwa wa
Ka-dinga pepo, unaofanana na dengue ambapo Waafrika waliamini kuwa
husababishwa na pepo mbaya.
Homa ya
dengue Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara wa Afya na Ustawi wa Jamii, homa
hiyo imethibitishwa kuwepo nchini tangu Juni 2013 baada ya sampuli
zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo jijini
Dar es Salaam kuchunguzwa katika maabara ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti
wa Magonjwa ya Binadamu.
Dalili za
ugonjwa ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili
hizo huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu
alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati mwingine dalili za
ugonjwa huo zinaweza kufanana sana na dalili za malaria hivyo wananchi
wanahimizwa kuchukua tahadhari na kupima afya zao mara wanapohisi dalili
za malaria ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua virusi vya
homa ya dengue.
Tabia ya
kunywa dawa bila kupima inaweza kusababisha mtu kupoteza maisha kwa
sababu homa ya dengue haitibiwi kwa dawa za malaria, haina chanjo wala
tiba maalumu. Kwa maneno mengine homa ya dengue sio kama malaria ambayo
kina mtu anaweza kutibiwa na dawa za mseto.
Homa ya
dengue hutibiwa kwa dawa tofauti kulingana na dalili zinakazoambatana na
ugonjwa. Endapo ugonjwa unaambatana na homa kali mgonjwa atatibiwa
homa, kama anapungukiwa na damu au maji mwilini tiba ni kuwekewa damu au
maji.
Pia
mgonjwa wa homa ya dengue anaweza kutokwa na damu kwenye fizi, mdomoni,
puani, kwenye macho na pia njia ya haja kubwa na ndogo na tiba yake
haiwezi kufanana na tiba ya mgonjwa mwenye homa bali atapata tiba sahihi
kulingana na tatizo lake.
Ugonjwa
huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Homa ya dengue
inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa
matibabu ya haraka. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa
anaweza kupoteza maisha.
Wananchi
hawapaswi kuwa na hofu kuhusu tiba kwa sababu serikali imeazimia
kuanzisha vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika hospitali
15 za Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni pamoja Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Hospitali zote tatu za Manispaa katika Jiji la Dar es Salaam
yaani Amana, Mwananyamala na Temeke.
Pia vituo
maalum vitaanzishwa katika Kituo cha Afya Kigamboni, Kituo cha Afya cha
Mbagala Rangi Tatu, Dispensari ya Yombo Vituka, Kituo cha Afya cha
Mnazi Mmoja, Dispensari ya Tabata A, Kituo cha Afya cha Bochi, Kituo cha
Afya cha Mbweni, Hospitali ya Mission Mikocheni, Hospitali ya TMJ,
Hospital ya Regency na Hospital ya Hindu Mandal.
Mbinu za
kupambana dhidi ya mbu wa homa ya dengue Ingawa mbu huyo anaweza
kuangamiza kizazi cha binadamu ni rahisi kupambana naye kama jamii
itaweka dhamira ya dhati ya kuchukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na
kuangamiza mazalio ya mbu hao kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama
au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.
Kufanya
usafi kwa kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama
vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo,
kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu na kuhakikisha maua
yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama.
Pia kuna
ulazima wa kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara na kusafisha
gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama. Pia ni vyema
kunyunyuzia dawa kwenye makaro ya maji machafu na vyoo vya shimo.
Ili
kuepuka ugonjwa wa dengue kila familia inahimizwa kuzingatia usafi,
kuweka wavu kwenye milango na madirisha, kuvaa nguo ndefu na yenye
mikono mirefu ili kuzuia kung’atwa na mtu, kujipaka dawa ya kufukuza mbu
na kutumia neti yenye dawa wakati wote, mchana na usiku.
Makala
haya yameandaliwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari kwa njia ya
mtandao wa kompyuta pamoja na taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii nchini
0 comments:
Post a Comment