atimaye picha halisi ya gharama ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) awamu ya kwanza, imeonesha nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo na Posta, itapanda kutoka nauli ya chini ya Sh 400 ya sasa mpaka Sh 700 na Sh 800 kwa ruti moja.
Kwa
wanafunzi, nauli kwa ruti moja kwenda katika vituo hivyo vikubwa katika
mradi huo ambao utaanza kwa majaribio mwishoni mwa mwaka huu, zitapanda
kutoka Sh 200 mpaka nusu ya nauli ya mtu mzima kwa ruti husika.
Aidha,
mfumo wa uendeshaji wa mradi huo na nauli, umewekwa katika sehemu
mbili; sehemu ya kwanza ni usafirishaji wa abiria kutoka maeneo ya ndani
ya makazi ya watu mpaka katika vituo vidogo na vikubwa vilivyopo
barabara kuu za Dart, za Morogoro na Kawawa kwa sasa na sehemu ya pili
ni usafirishaji wa abiria kutoka katika vituo vilivyopo katika barabara
kuu ya Dart za Morogoro na Kawawa, kwenda vituo vikuu vikiwemo Kariakoo
na Posta.
Hayo
yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam, katika taarifa ya mwisho ya
Makubaliano ya Dart, iliyotolewa katika mkutano wa Mashauriano ya
Uwekezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo wa Dart.
Taarifa
hiyo imebainisha kuwa, abiria atakayelazimika kusafiri na mabasi ya
Dart kwa safari fupi ndani ya barabara zilizo katika makazi ya watu, kwa
mfano wa barabara inayopita Sinza; kutoka Bamaga mpaka Shekilango,
atalipa Sh 500, tofauti na sasa ambapo analipa Sh 400.
Kwa
atakayetumia mabasi ya Dart kutoka katika barabara ndogo zilizopo
katika makazi ya watu, kwenda katika vituo vikubwa vya Dart vilivyopo
njia kuu za Morogoro na Kawawa ili kwenda Kariakoo, Posta au Kimara,
atalazimika kukata tiketi ya Sh 800, atakayoitumia kupata usafiri kutoka
barabara ndogo na katika barabara kubwa.
Mfano
wa nauli hiyo, ni abiria anayetoka maeneo hayo ya Sinza kwenda Kimara,
Kariakoo au Posta, ambaye atalazimika kukata tiketi ya Sh 800,
itakayomwezesha kupakia basi la Dart kutoka maeneo hayo mpaka
Shekilango, ambako atabadilisha basi kwa tiketi hiyo hiyo, kwenda
Kariakoo, Posta au Kimara.
Aidha
kwa abiria watakaolazimika kutumia mabasi matatu ya Dart, kutoka katika
barabara ndogo zilizopo katika makazi ya watu, kupitia barabara kuu za
Dart na kwenda katika eneo lililopo katika barabara ndogo za makazi ya
watu, watalazimika kulipa Sh 900 kwa mabasi yote matatu.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, mabasi yatakayotumika kubeba abiria kwenye njia
kuu, yatachukua watu zaidi ya 150 kwa basi moja, ambapo abiria
watakaopata viti vya kuketi ni 52 na wengine wamewekewa eneo nadhifu la
kusimama.
Kwa
mabasi yatakayobeba abiria kutoka njia ndogo zilizopo katika makazi ya
watu, yatachukua watu zaidi ya 80, kati ya hao abiria 42 ndio
watakaopata nafasi ya kukaa na waliobakia wamewekewa nafasi nadhifu ya
kusimama.
Kuhusu
muda utakaotumika kwenye ruti moja ya mabasi hayo ya Dart, abiria
atatumia muda wa dakika zisizozidi 30 kufika anakokwenda, akitumia
mabasi kwenye njia kuu, tofauti na sasa ambapo kwa kutumia daladala
abiria hutumia zaidi ya saa mbili kufika waendako.
Akizungumza
katika mkutano huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, utaratibu wa ulipaji
nauli kwenye mabasi ya Dart, utakuwa ni wa kutumia mfumo wa kadi ambapo
abiria anatakiwa anunue tiketi kabla ya safari.
Alisema
utaratibu huo, utapunguza au kuondoa kero kwa abiria na katika mabasi
madogo yanayobeba abiria kuwaunganisha kwenye njia kuu, yatakuwa na
vifaa vya mawasiliano baina ya dereva aliye barabara ndogo na dereva
aliye barabara kuu za Dart.
Kwa
mujibu wa Sagini, mradi huo ukianza, abiria watanunua tiketi kwa
kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu kama vile M-pesa, Tigo-pesa,
Pesa Fasta na Airtel Money.
Alisema
ili kuzuia wizi na udanganyifu kwenye vituo vya mauzo ya tiketi na
kwenye vituo vya mabasi, zinafungwa kamera na video ili kuimarisha
ulinzi, na kuhakikisha mapato halali kwa ruti zinazofanywa.
“Hii itasaidia kuondoa wizi na uhujumu unaoweza kufanywa katika vituo vya abiria,” alisema Sagini.
Alisema
kwa hatua hiyo, dalaldala za sasa zitaondolewa katika zaidi ya njia 43
ambazo ziko kwenye barabara ya Morogoro na barabara ya Kawawa na katika
ruti nyingine, daladala hizo zitaendelea kuondolewa hadi hapo ujenzi wa
barabara zote za Dart utakapokamilika.
Katika
mabasi hayo ya kubeba abiria kwenye njia kuu za Dart, mabasi
yanayoruhusiwa ni yale yatakayokidhi vigezo, ambavyo ni pamoja na kuwa
na upana wa meta 18 na uwezo wa kubeba abiria 150, ambayo yanahitajika
mabasi 145.
Kwa
mabasi yatakayosogeza abiria hadi njia kuu, yatatakiwa yawe na uwezo wa
kubeba abiria zaidi ya 80 na upana wa meta 12 na yatatakiwa mabasi 90.
Akitoa
mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia,
alisema ni vyema katika sekta binafsi, wadau wa usafiri na watu
mbalimbali wachangamkie fursa hiyo.
Alisema
Serikali kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi, umeona ni vyema
kushirikisha wadau hao kwenye mradi huo mkubwa Afrika Mashariki, ambao
ukitumika vizuri ni chachu ya maendeleo na ukuaji uchumi.
0 comments:
Post a Comment