Idara ya
Uhamiaji nchini Tanzania imegundua maficho ya wasichana waliosafirishwa
kutoka nchi za India na Nepal mjini Dar es Salaam ambao wanatumikishwa
katika biashara zisizo halali katika maeneo mbalimbali jijini humo.
Katika
siku tano zilizopita, idara ya uhamiaji jijini Dar es salaam inasema
imewaokoa wasichana 51 raia wa India na Nepal waliohifadhiwa katika
nyumba kadhaa na kutumikishwa katika biashara ya ngono na nyinginezo na
kuwakamata wafanyabiashara wenye asili ya kiasia wanaotuhumiwa
kusafirisha wasichana hao na kuwatumikisha hapa nchini
Mwishoni
mwa mwezi uliopita wasichana wengine 17 walikutwa wamehifadhiwa katika
nyumba moja eneo la Msasani jijini Dar es salaam kwa zaidi ya miezi
mitatu huku wakidaiwa kutumika kwenye biashara ya ngono huku wengine 34
wakikamatwa jana eneo la Mwananyamala jijini humo.
Wafanyabiashara
waliotiwa nguvuni wanadai kuwa waliwaleta nchini humo wasichana hao
kushiriki kucheza ngoma za asili kutoka mataifa yao katika club mbali
mbali za usiku maarufu-Mujra na walikuwa wamehifadhiwa katika jengo moja
huku pasi zao za kusafiria zikiwa zimechukuliwa na aliyetambuliwa kama
meneja wao
Afisa
Uhamiaji Mkaguzi wa mipaka Doto Selasini amesema wasichana hao wenye
umri wa chini ya miaka 26 waliingizwa nchini kwa njia halali kwa ahadi
ya meneja wao kukaa nchini kwa siku 14 kwa ajili ya kushiriki ngoma za
utamaduni wa mataifa yao, lakini wamekuwa wakitafutiwa wateja na baadae
kulazimishwa kufanya vitendo vya ngono na kwamba wamefanikiwa kupata
taarifa zao kupitia raia wema
Meneja wa
wasichana hao Savio Menes ambaye naye ametiwa mbaroni na maafisa wa
uhamiaji amesema wasichana hao aliwaingiza nchini kupitia wakala aliyeko
nchini India na kudai kuwa walikuja kushiriki ngoma za utamaduni za
bara la Asia
Hata
hivyo wasichana wenyewe walipohojiwa na maafisa wa uhamiaji walikiri
kuishi katika mazingira magumu na kufanya biashara isiyo halali na
kwamba wako tayari kurejeshwa makwao India na Nepal. Wamedai kuwa
wamekuwa chini ya ulinzi mkali huku wakitolewa usiku na kupelekwa katika
mahoteli na kurejeshwa alfajiri na hawakuruhusiwa kuwa na mawasiliano
na mtu yeyote.
Taarifa
zilizopatikana baadaye zilieleza kwamba wasichana 17 waliokamatwa Mei 30
wamesafirishwa na kurejeshwa makwao India na Nepal huku wafanyabiashara
waliowaleta wakisubiri taratibu za kufunguliwa mashtaka.
0 comments:
Post a Comment