Wabunge
wanawake bila kujali itikadi za vyama juzi usiku waliungana kuibana
Serikali wakishinikiza iongeze fedha za Bajeti ya Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ya mwaka 2014/15 ili kukabiliana na vifo vya kina mama
na watoto.
Kibano
hicho kilianza mapema asubuhi lakini moto zaidi uliwaka jioni wakati
Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo iliyotengewa Sh622
bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo
mwaka 2013/14 ambayo ilitengewa Sh753 bilioni. Wabunge wanawake 10 na
wanaume wawili walichangia ikiwamo kutoa shilingi.
Kambi ya
Upinzani ilianza kuibana Serikali ikisema imeweka rehani wananchi wake
kutokana na kitendo chake cha kuchangia kiasi kidogo cha fedha za
maendeleo za wizara hiyo.
Akiwasilisha
taarifa ya kambi, Waziri Kivuli wa Afya, Dk Anthony Mbassa alisema
Bajeti ya Sh622 bilioni na fedha za maendeleo ni Sh305 bilioni ambazo
kati ya hizo, Serikali itatoa Sh54 bilioni tu, wakati washirika wa
maendeleo watatoa Sh251 bilioni.
"Hii
inaonyesha wazi kuwa Serikali imeendelea kuweka rehani wananchi wake
kutokana na bajeti kuendelea kuwa tegemezi kwa wahisani," alisema.
Kibano cha wanawake
Licha ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri
wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na
Adam Malima kutoa ufafanuzi, walishindwa kuwashawishi wabunge hao
waliokuwa wakililia nyongeza ya bajeti.
Hoja
hiyo, iliibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso
baada ya kuondoa shilingi akiitaka Serikali itoe majibu ya sababu za
kutoa Sh387 bilioni pekee kati ya Sh753 bilioni za bajeti ya mwaka
2013/14, jambo ambalo limekwamisha utendaji kazi wa wizara hiyo, ikiwa
ni pamoja ya kushindwa kutekeleza Azimio la Abuja kuwa kila nchi itenge
asilimia 15 ya bajeti kuu kwa ajili ya Wizara ya Afya ili kunusuru vifo
vya kina mama na watoto.
Baada ya
kauli hiyo wabunge kadhaa walisimama na kuunga mkono hoja hiyo licha ya
Mwigulu kulieleza Bunge kuwa Serikali imepanga kuongeza kiasi cha fedha
kilichobaki kabla ya Juni 31, mwaka huu.
Hoja hiyo
ilifafanuliwa na Malima ambaye alisema Serikali imetoa Sh12 bilioni na
kwamba tayari fedha hizo zimeshaingizwa katika akaunti ya Wizara ya
Fedha kwa ajili ya kulipia deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambalo ni
Sh89 bilioni na deni la matibabu nje ya nchi ambalo ni Sh21 bilioni.
"Kwa nini
Bunge lilipitisha Sh753 bilioni wakati likijua wazi kuwa haziwezi
kupatikana, Watanzania watapataje huduma za afya?" alihoji Paresso.
Jaji
Werema alijibu akisema Azimio la Abuja ni la hiari na hata kama nchi
husika ikishindwa kulitekeleza haitapata adhabu yoyote, huku akisisitiza
kuwa Serikali haikupata fedha za kufikia malengo ya azimio hilo na
kuahidi kuwa kiwango cha fedha kilichobaki kitaongezwa kabla ya mwisho
wa mwezi huu.
0 comments:
Post a Comment