HOTUBA YA MHE DKT. SHUKURU JUMANNE KAWAMBWA (MB), WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI |
Ndugu Dkt. Siston Masanja
Mgullah, Mtendaji Mkuu wa ADEM,
Ndugu Mwenyekiti wa Wanamafunzo,
Ndugu Viongozi wa Elimu WEMU NA OWM-TAMISEMI,
Ndugu Wawezeshaji wa Mafunzo na Wafanyakazi wa ADEM,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
1.
Utangulizi
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Kwanza napenda kutumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai hadi leo hii tunapokutana katika kufunga mafunzo kuhusu namna ya kukabiliana na majanga shuleni na katika ofisi za elimu nchini. Pili, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mtendaji Mkuu wa ADEM kwa kunishirikisha na kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika ufungaji wa mafunzo haya muhimu kwa Maafisa Elimu Taaluma na Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu yaliyoanza Jumatatu terehe 19/05/2014
na kumalizika leo Ijumaa 06/06/2014.
Nimejulishwa kuwa washiriki wa mafunzo haya wanatoka Mikoa yote Tanzania Bara na waligawanywa katika makundi makuu matatu ili kufanya mafunzo kuwa fanisi; na kundi hili ni la tatu. Ninawapongeza sana washiriki wote wa mafunzo haya katika awamu zote tatu. Hongereni sana.
2. Shukrani kwa Wadau waliochangia kufanikisha mafunzo.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa OWM-TAMISEMI kwa kugharamia mafunzo haya muhimu ya namna ya kukabiliana na majanga na maafa katika taasisi za elimu nchini. Nawashukuru pia wadau wote waliochangiakufanikisha mafunzo haya kwa njia moja au nyingine, hususan wakufunzi na wafanyakazi wa ADEM, maafisa kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Kukabiliana na Maafa, Maafisa kutoka Hospitali ya Amana Manispaa ya Ilala, RED-CROSS-Dares Salaam na Kikosi cha Zima Moto Wilaya ya Bagamoyo. Asanteni sana kwa ushiriki wenu wenye ufanisi.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Nimeambiwa kwamba mafunzo haya yalishirikisha jumla ya Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Taaluma (Msingi na Sekondari) wapatao 636 kutoka Tanzania Bara. Hili ni kundi muhimu sana ambalo linahusika moja kwa moja katika kusimamia utekelezaji wa utoaji Elimu bora
nchini katika ngazi ya halmashauri chini ya mkakati mpya wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika sekta ya elimu.
3. Madhumuni ya Kutoa Mafunzo haya
Ndugu Washiriki wa Mafunzo,
Sisi viongozi wa WEMU, OWM-TAMISEMI na ADEM,tunaamini kuwa mafunzo mliyoyapata yatawawezesha kusimamia utoaji wa elimu bora shuleni na pia kutumia mbinu mbalimbali mlizo jifunza katika kuzuia na kukabiliana na majanga yanapotokea katika maeneo yenu. Tunaamini pia
kuwa mtaweza kutoa elimu kuhusu majanga kwa walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wote wa elimu katika halmashauri zenu. Aidha, Elimu mliyoipata itawawezesha pia kuwa na uwezo wa kusimamia, kufuatilia na kuimarisha miundombinu shuleni. Aidha, kuchukua hatua na tahadhari zitakayowezesha kukabiliana na majanga, mbalimbali kama vile umuhimu wa milango ya majengo ya shule kufungukia nje, kuwa na vifaa vya kuzima moto na kuwa na visanduku vya huduma ya kwanza.
4. Athari zinazotokakana na majanga kwa ujumla.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Katika kipindi kisichopungua miongo mitatu, dunia imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali ambayo yamesababisha hasara kubwa ya upotevu wa mali na maisha ya watu. Kila mwaka, watu zaidi ya milioni 200 duniani wanaathirika kwa ukame, mafuriko, vimbunga, matetemeko, moto, milipuko ya mabomu na majanga mengine. Aidha, kuongezeka kwa majanga kumeongeza kasi ya
watu kuathirika kiuchumi na kuongeza idadi ya watu maskini duniani. Majanga haya yanagusa kila mtu na yako kila mahali. Tumesikia kuhusu tsunami ya Bahari ya Hindi; matetemeko ya ardhi Kusini
mwa Asia, vimbunga kule Marekani, Visiwa vya Caribbean na Pasifiki, na kuhusu mafuriko makubwa bara la Ulaya na Asia, ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Kuwepo kwa majanga duniani kunatokana na sababu kuu tatu ambazo ni;
i. Majanga
yanyotokana na kuongezeka kwa shughuli za wanadamu zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa na mazingira. Baadhi ya shughuli hizo ni ukataji wa miti ovyo, uchimbaji wa madini katika migodi mikubwa, uvuvi mkubwa baharini usiozingatia utaalamu, uanzishwaji wa viwanda vikubwa vya kemikali na madini, matumizi mabaya ya ardhĂ na ugaidi;
ii. Majanga yanayosababishwa na nguvu ya asili mfano Volkano, vimbunga,
mafuriko na matetemeko ya ardĂ; na
iii. Majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu pamoja na nguvu za asili kwa pamoja (complex disasters), kwa mfano moto, magonjwa na ukame.
Ninaamini wawezeshaji wamewafundisha masuala haya kwa undani zaidi.
5. Athari za Majanga hapa nchini.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji na milipuko ya mabomu. Majanga yote haya yameleta maafa na kusababisha athari kwa wananchi na mali zao. Katika mwaka 2013/14, ukame umesababisha upungufu wa
chakula kwa watu 828,063 katika Wilaya 54 za Mikoa 14 nchini. Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya shilingi bilioni 15.2 pamoja na shilingi bilioni 2.2 kwa ajili
ya kukisafirisha hadi kwa walengwa. Mafuriko makubwa pia yametokea katika maeneo mengi hususan, mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Tanga, Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu. Katika kukabiliana na athari zilizojitokeza, Serikali na wadau mbalimbali wametoa misaada ya dharura ya kibinadamu kwa waathirika na kuchukua hatua za kurejesha miundombinu ya maji, elimu, afya, barabara na madaraja na umeme.
6. Athari za Majanga katika Shule
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Shule zetu zimekuwa zikikumbwa na majanga mbalimbali kwa mfano moto, mafuriko na vimbunga. Majanga haya yameleta athari kubwa kwa maisha ya walimu na wanafunzi, katika majengo yakiwemo madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo. Samani za shule, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, barabara, huduma za maji na umeme, viwanja vya michezo na mazingira yote ya shule yamekuwa yakiharibiwa na majanga. Tumeshuhudia moto ukiteketeza shule za Sekondari za
Shauritanga, Idodi, Morogoro n.k na kusababisha vifo kwa wanafunzi na kuharibika kwa miundo mbinu ya shule. Pia tumeshuhudia mafuriko yakisababisha kutoendelea kwa masomo katika Wilaya za Kilosa, Kyela, Ilala, Mvomero n.k mafuriko haya yalisababisha shughuli za shule kukwama.
7. Umuhimu wa Elimu ya Majanga kwa Wasimamizi wa Elimu.
Ndugu Wanamafunzo na Wageni waalikwa,
Wakati majanga yanapotokea, watoto wetu na wanajumuiya wote katika shule huwa hawako
salama. Kwa kawaida wakati wa majanga watoto ndio huwa wanapata madhara makubwa kwa sababu uwezo wao wa kujitetea huwa ni mdogo. Hivyo wengi huathirika vibaya na hata kupoteza maisha. Ikiwa wasimamizi wa watoto hawa watapata elimu ya kukabiliana na majanga upo uwezekano mkubwa wa kupunguza hasara zinazotokana na Majanga katika taasisi za elimu nchini. Kwa hiyo mafunzo haya ni muhimu sana kwa Viongozi wanaosimmia Shule na taasisi za Elimu. Mafunzo haya hayanabudi kuwa endelevu kwa viongozi wote katika ngazi mbalimbali za elimu. Ninaamini kuwa mafunzo haya yatakapokuwa yametolewa kwa wasimamizi wote wa elimu, shule zetu zitaendelea kuwa mahali salama pa kutolea elimu bora.
8. Mikakati ya Kitaifa ya kukabiliana na Majanga nchini
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Wakati majanga haya makubwa yanatokea, Serikali zote duniani zimekuwa na mikakati ya kuchukua hatua za tahadhari ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa majanga haya na athari zake kijamii. Tanzania kwa mfano tunayo Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo inatupa mwongozo wa jinsi ya kukabiliana na majanga mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea nchini kwa
kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa. Aidha, Tanzania imekuwa ikishiriki katika kuandaa mikakati ya kimataifa inayohusu kuchukua tahadhari katika kupunguza majanga haya. Moja ya mikakati hiyo ni Hyogo Framework of Action (2005 -2015) uliotokana na mkutano wa kimataifa katika jimbo la Kobe, nchini Japan (2005) ambao madhumuni yake ni kupambana na majanga yanayoathiri maendeleo ya nchi kwa njia ya elimu na kuweka miundombinu sahihi inayoweza kusaidia kukabiliana na majanga.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Serikali kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa, imeendesha mafunzo ya kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na maafa ikiwemo kupokea na kugawa misaada wakati wa maafa katika ngazi za Mkoa na Wilaya kwa mikoa ya Mara, Geita, Singida, Simiyu, Shinyanga, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora na Arusha. Aidha, Mipango ya kujiandaa kukabiliana na maafa katika Halmashauri za Wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu, Mwanga na Same imeandaliwa. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 serikali itafanya tathmini ya maafa yanayoweza kutokea na uwezo wa kukabiliana nayo pamoja na mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika Halmashauri za Wilaya za Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Masasi, Mvomero na Kilosa. Vilevile, itaanza Ujenzi wa Kituo cha Dharura cha Utendaji na Mawasiliano (Emergency Operation and Communication Centre) katika eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni.
9.Mikakati ya kukabiliana na Majanga Sekta ya Elimu.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Kwa upande wa sekta ya elimu, mchakato wa kuwezesha wasimamizi wa elimu kuhusu elimu ya kukabiliana na majanga ngazi ya Halmashauri umeanza na maafisa hawa na baadae mafunzo yatafanyika kwa Maafisa Elimu Wilaya, Maafisa elimu Mkoa Wakuu wa Wilaya na wadau wengine kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Ni mategemeo ya Serikali kuwa baada ya mafunzo haya, washiriki wataweza kutimiza majukumu haya mapya kama ifuatavyo:
· kuunda Kamati za kukabiliana na Majanga Shuleni;
· kuandaa mipango kazi ya kukabiliana na majanga katika ngazi ya halmashauri na shule;
· kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo milango kufungikia nje, kuweka vizima moto (fire extinguishers), ndoo za michanga na kuboresha mazingira ya shule;
· kujenga uelewa wa pamoja wa namna ya kukabiliana na majanga miongoni mwa walimu, wanafunzi na jumuiya inayozunguka shule;
· kujenga mtandao (network) wa kukabiliana na majanga kati ya shule na jumuiya inayozunguka shule;
· kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu majanga shuleni;na
· kuandika taarifa sahihi kuhusu uwezekano wa kutokea majanga na madhara ya majanga shuleni mara yanapotokea.
Ndugu Mtendaji Mkuu;
Ni azma ya Serikali, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuendelea kusimamia na kuwezesha Wakala kutoa mafunzo fanisi ya Uongozi na Uendeshaji wa Elimu pamoja na masuala mtambuka yakiwemo kukabiliana na majanga kwa maafisa walio katika ngazi mbalimbali za usimamizi wa elimu nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila kiongozi katika taasisi ya elimu anapata mafunzo haya ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa watoto waliosheheni maarifa, stadi na ujuzi stahiki unaowawezesha kuhimili ushindani katika soko la ajira na ulimwengu wa kazi.
9. Masuala Mtambuka yanayo athiri Utoaji wa Elimu bora.
Ndugu Mtendaji Mkuu,
Naomba nitumie nafasi hii pia kuwakumbusha washiriki wa mafunzo na jamii yote ya ADEM kuhusu masuala mtambuka kama Virus vinavyosababisha UKIMWI, Rushwa sehemu za kazi, masuala ya Kijinsi na Jinsia, Madawa ya kulevya na uharibifu wa mazingira. Masuala yote haya yanaathari katika mchakato mzima wa utoaji elimu nchini. Nawaomba wahitimu wetu muongeze nguvu katika kupambana na masuala mtambuka sehemu za kazi na katika jamii. Kumbukeni kuwa nchi yoyote duniani huendelea kutokana na kuwepo kwa watu wenye Afya njema, Utawala Bora pamoja na nguvu kazi yenye weledi katika nyanja za Sayansi na Teknolojia, kiuchumi, kisiasa na kijamii.
10. Hitimisho
Ndugu Mtendaji Mkuu na Washiriki wa Mafunzo,
Kwa kumalizia, napenda kuwakumbusha wahitimu wa mafunzo kuwa elimu waliyopata hapa ADEM iwafikie maafisa wengine wa elimu ngazi ya halmashauri, kata na shule. Walimu na wanafunzi ni walengwa wakuu wa elimu hii ya kukabiliana na majanga kwa kuwa shule zimekuwa zikikumbwa na majanga mbalimbali mfano moto na mafuriko kwa kiasi kikubwa. Ni mategemeo ya Serikali kuwa taasisi zote za elimu nchini zitakuwa na mipango mikakati ya namna ya kukabiliana na majanga kwa kuelimisha wadau wote namna ya kuzuia na kupambana na majanga. Kwa kufanya hivyo, shule zitakuwa na uwezo wa kuendelea kutoa elimu bora hata wakati wa majanga na baada ya majanga kutokea.
Ndugu Mtendaji Mkuu na Washiriki wa Mafunzo.
Baada ya kusema haya, sasa napenda kutamka kuwa mafunzo kwa Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Taaluma wa elimu ya Msingi na Sekondari yanayohusu elimu katika majanga yamefungwa rasmi.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
0 comments:
Post a Comment