Tuesday, 10 June 2014

'MZEE SMALL' AZIKWA AACHA LAANA-SOMA HAPA NI NINI

...

HATIMAYE aliyekuwa nguli wa sanaa za maigizo Bongo, Said Ngamba ‘Mzee Small’ amezikwa jana katika Makaburi ya Tabata-Segerea jijini Dar es Salaam huku akiacha laana kwa tasnia ya maigizo.

Mzee Small alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili  (MNH) ambako alilazwa akisumbuliwa na…

Ustadhi akimuombea marehemu dua ya mwisho baada ya kuuhifadhi mwili wake kaburini.

Stori: MWANDISHI WETU
HATIMAYE aliyekuwa nguli wa sanaa za maigizo Bongo, Said Ngamba ‘Mzee Small’ amezikwa jana katika Makaburi ya Tabata-Segerea jijini Dar es Salaam huku akiacha laana kwa tasnia ya maigizo.
Mzee Small alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili  (MNH) ambako alilazwa akisumbuliwa na maradhi ya kiharusi yaliyomuanza miaka takriban miwili iliyopita.
Mwili wa Mzee Small ukiwa kaburini.
Wakati wa kuugua kwake, marehemu aliwahi kulalamikia kitendo cha sehemu kubwa wa wasanii wa Bongo Movies kumtenga kiasi cha kuwa ombaomba hali iliyomfanya awe akisema: “Mungu yupo, iko siku.”
“Mzee Small amezikwa sasa, lakini kichwani lile neno lake kwamba Mungu yupo kwa sababu tulikuwa hatumsaidii kwa lolote naliogopa sana,” alisema mmoja wa mastaa wa Bongo Muvi ambaye hakupenda jina lake litoke gazetini.
Mdogo wa marehemu mzee Small akiwa chini baada ya kuzidiwa na kuishiwa nguvu muda mfupi baada ya shughuli za kuhifadhi mwili wa kaka yake kumalizika.
Aliendelea: “Unajua yale maneno ya kutulalamikia ambayo yalikuwa ya kweli kabisa, ni laana kwetu wasanii kwani tumekuwa tukibagua watu. Akiumwa fulani mwenye jina kubwa kwa sasa tunakimbilia, akifa fulani mwenye jina kubwa kwa sasa tunakimbilia, lakini wakongwe kama marehemu Mzee Small ameondoka akiwa hana msaada kutoka kwenye tasnia.
“Leo hii ameondoka, nini katuachia kama si laana. Maana hajaacha faida kwetu ambayo tunaweza kusema tutarithi.”
Rais Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo pembeni (kulia) ni Mahmoud, mtoto wa marehemu
Wakati wa uhai wake, marehemu Mzee Small alipotembelewa na waandishi wetu, aliwalalamikia wasanii wa filamu nchini akisema: “Mimi nimewafundisha vijana wengi maigizo.
“Pia ni mmoja wa waliohangaikia sanaa mpaka leo hii unaona vijana wana mafanikio, wanaendesha magari nk.
Ni kwa sababu ya sisi tuliotangulia. Leo hii nina matatizo wananikimbia, Mungu yupo.”
Naye mtoto wa marehemu, Mohmud Ngamba alisema mzee wake kabla hajafa alimuonya kutofuata mambo ya dunia na kushika sana njia za Mungu na wawe na upendo kwa watu.
Pia alimwambia ajitahidi kufanya sanaa ili aje kuwa kama yeye baba yake.
Mahmoud Said Ngamba akisoma wasifu wa baba yake.
Nje ya familia ya marehemu anapatikana msanii mwenzake, Chausiku Salum ‘Bi Chau’ ambaye kilio chake baada ya kupokea kifo cha msanii huyo kilikuwa kikubwa kupita watu wengi wa karibu na marehemu.
Bi. Chau alikipokea kifo cha mkongwe huyo wa maigizo akiwa jijini Tanga.
Bi. Chau alianza kuigiza na marehemu miaka ya tisini akiwa kama mke wa kwenye sanaa hali iliyowafanya wengi kuamini ni mke halali wa marehemu hata nje ya jukwaa la sanaa.
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini (Taff) Simon  Mwakifwamba akisalimiana na Rais Kikwete.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Marehemu Mzee Small alizaliwa mwaka 1955. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mingumbi, Kilwa mkoani Lindi. Mbali na ukongwe, Mzee Small kila alipozungumza na watu hakuona sababu ya kuficha kusema yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha runingani.?Mzee Small alianza sanaa hiyo miaka ya sabini akifundishwa na mwigizaji Said Seif ‘Unono’ ambaye ni marehemu kwa sasa.
Meneja wa Global Publishers Abdallah Mrisho (mwenye tai na miwani katikati) akiwa na baadhi ya wasanii waliofika kwenye maombolezo.
Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, Mzee Small ametumika katika vikundi vya mashirika mbalimbali nchini.
Marehemu kila alipotajiwa Bi. Chau alisema ni mkewe wa ndoa wa kwenye maigizo kauli ambayo wengi hawakuiamini wakijua anakwepa kumtambulisha moja kwa moja.
Kuna wakati mke wake, Fatuma Ngamba aliwahi kusema kwamba, hana wivu na Bi. Chau kwa vile anajua anaigiza na marehemu na ndiyo kazi inayowafanya waishi.

Jeneza likipelekwa makaburini.
Katika kipindi cha mateso ya ugonjwa wake, wadau mbalimbali walijitokeza kumsaidia kwa hali na mali huku wito mkubwa ukitolewa kwamba, watu zaidi wajitokeze badala ya kusubiri kutoa rambirambi.
Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu Mzee Small. Amina.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger