Mazishi ya mtoto Nasra Rashid (4) aliyefichwa katika boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa, yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya Kola mkoani Morogoro.
Nasra alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni mosi mwaka huu katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu kuanzia Mei
26 mwaka huu akitokea hospitali ya Morogoro.
Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin
Ngungamtitu, ibada na heshima za mwisho zitafanyika katika Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro.
Alisema mwili wa Nasra utawasili katika Uwanja wa Jamhuri saa mbili
asubuhi ambapo ibada na heshima za mwisho zitaanza muda huo hadi saa
sita mchana.
Ngungamtitu alisema shughuli za mazishi zitaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Said Amanji.
Mtoto Nasra alifariki usiku wa kuamkia Juni Mosi baada ya kuzidiwa
kutokana na tatizo la kupumua na utapiamlo uliokuwa ukimsumbua
alipofikishwa Muhimbili.
Safari kutoka Dar
Mwili wa Nasra jana uliondolewa katika hospitali ya Muhimbili majira
ya mchana ukiwa ndani ya Toyota Noah iliyokuwa na askari polisi kitengo
cha Upelelezi Mkoa wa Morogoro pamoja na watu wengine wawili ambao
hawakujulikana nyadhifa zao.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alithibitisha
kuchukuliwa kwa maiti ya mtoto huyo majira ya saa tano asubuhi baada ya
kukabidhiwa kwa mlezi wake, Josephine Joel na maofisa wapelelezi wawili
kutoka Morogoro.
“Maiti ya mtoto Nasra imechukuliwa, tulimkabidhi mama yake mlezi
aliyekuja naye na maofisa upelelezi ambao walikabidhiwa ripoti ya
uchunguzi.
“Siwezi kuzungumza ripoti hiyo ina nini kwa sababu hiyo iko kisheria
zaidi (Medical Legal Report) kutokana na tukio lenyewe lilivyo… pia
siwezi kuwapeleka kwa daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa mtoto
huyo kwa sababu sheria haimruhusu kuzungumza,” alisema Aligaesha.
Mwandishi alimtafuta bila mafanikio daktari aliyeufanya
uchunguzi mwili wa Nasra aliyefahamika kwa jina moja la Mwakyoma, hata
ilipopigwa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
Hata hivyo mmoja wa madaktari waliokuwa wakimtibu Nasra ambaye
hakutaka kutaja jina lake siku hiyo kwa kuwa siyo daktari wa zamu,
alisema mtoto huyo amefariki akiwa kwenye mashine ya oksijeni iliyokuwa
ikimsaidia kupumua.
“Mtoto Nasra alipofikishwa na kufanyiwa vipimo vya awali tulibaini
ana utapiamlo, tukamuanzishia chakula na dawa, tuliendelea na vipimo
akasema anaumia kifuani na kiuno, tukampima na kubaini ana nemonia
wakati huo akashindwa kupumua tukamwekea mashine ya oksijeni,” alisema.
Katika hatua nyingine, baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi,
alisema amekubaliana na uamuzi wa serikali wa kumzika mtoto wake.
Mvungi ambaye jana alionekana katika jengo la kuhifadhia maiti
hospitalini hapo akiwa na ndugu zake wanne, alisema alipewa usafiri
kwenda Dar es Salaam kuchukua maiti ya mtoto wake.
Hata hivyo baada ya gari lililobeba maiti ya mtoto wake kuondoka, nao
waliingia katika gari aina ya Land Cruiser mali ya Halmashauri ya
Manispaa ya Morogoro na kuondoka.
Mtoto Nasra alifichuliwa Mei 21 mwaka huu na majirani ambao
walimweleza Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuwa
alikuwa amefichwa katika boksi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la
Mariamu Said mkazi wa kata hiyo mkoani Morogoro.
Majirani hao walimweleza Zongo kuwa Nasra alifichwa ndani ya boksi
tangu akiwa na miezi tisa mwaka 2009 na kwamba alikuwa hafanyiwi usafi
wala kutolewa nje.
0 comments:
Post a Comment