Tuesday, 10 June 2014

HOUSE GIRL ATOBOA SIRI'SAKATA LA KUNG'ATWA NA BOSI WAKE

...


NYUMAya pazia! Yule msichana Yusta Lucas (20) mwenyeji wa Mkoa wa Tabora ambaye alifika jijini Dar kufanya kazi ya u-hausigeli na kufanyiwa ukatili wa kutisha na bosi wake kisha habari zake kuandikwa, ametoa siri nzito, Uwazi limemegewa
.
Yusta Lucas akionyesha majeraha ya meno aliyong'atwa na bosi yake.
Akizungumza kwa uchungu na gazeti hili akiwa wodini kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu Kinondoni, Mwananyamala jijini Dar, Yusta ambaye amefanya kazi kwa tajiri yake huyo kwa miaka mitatu alisema:
“Kwanza nataka watu wajue kuwa mwajiri wangu ni binamu yangu, alinileta hapa Dar kwa ajili  ya kumsaidia kazi za ndani pamoja na kumlelea mwanaye.
“Kipigo hasa kilianza mwanzoni mwa mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuning’ata kwa meno mwili mzima, ndiyo maana mwili wangu wote unaonekana una mabakamabaka.
“Mateso yangu majirani walikuwa wakiyajua kutokana na kilio changu lakini walikuwa wanashindwa kunisaidia kwa sababu ya ushirikiano mdogo.
“Kwanza nashangaa sana kwa adhabu yake ya kuning’ata meno mpaka damu zinabaki kwake. Je, kama nina virusi vya Ukimwi si na yeye anavipata?
“Sijajua alikuwa anapata wapi ujasiri wa kuning’ata meno. Kwa kweli nimeteseka kwa muda mrefu sana. Mungu ndiye anajua, lakini nawashukuru sana majirani walioliona hilo na kuamua kuchukua hatua.”
Yusta Lucas akiwa wodini kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu Kinondoni, Mwananyamala jijini Dar.
KUHUSU MAISHA YA TAJIRI WAKE
Aidha, Yusta alianika mienendo mitano ya bosi wake huyo na kusema imekuwa ikimshangaza sana.
MWENENDO WA KWANZA
“Mimi katika kuishi kwangu pale sijawahi kumwona jirani yeyote amekuja ndani kusalimia wala yeye kwenda kwa jirani kufanya hivyo jambo ambalo si la kawaida.”
MWENENDO WA PILI
“Yeye (bosi wake) hana mume. Lakini tangu nimeishi pale kwa miaka mitatu sijawahi kumwona mwanaume ameingia ndani ya nyumba achilia mbali wanawake wenzake, hata mgeni. Kifupi yeye ni yeye kwa pale nyumbani kama ana marafiki labda wanakutana mbali.”
MWENENDO WA TATU
“Muda wake wa kurudi nyumbani siku zote ni usiku mnene, amewahi sana ni saa mbili usiku. Kwa hiyo, muda mwingi mimi ndiyo huwa nyumbani.”
MWENENDO WA NNE
“Anajiweza, sijui kwa nini aliamua kunifanyia hivi. Maana mtu ana gari, anaendesha mwenyewe na anasema ana hela, ndiyo maana namshangaa kuniadhibu kwa kuning’ata kwa meno.”
MWENENDO WA TANO
“Sikumbuki lini nimewahi kumwona akicheka. Muda mwingi anaonekana amekasirika tu kiasi kwamba nimekuwa nikimwogopa siku zote.”
OMBI KWA SERIKALI
Yusta alisema kufuatia matatizo makubwa yaliyompata ameiomba  serikali imsaidie  aweze  kurudi nyumbani kwao Tabora.
SHUKURANI KWA MAJIRANI
Yusta alitoa shukurani kwa majirani  waliojitokeza kuokoa maisha yake ambapo alisema kama wasingekuwa wao hajui ingekuwaje.
MANENO YA MUUGUZI
Kwa upande wa hospitali hiyo, muuguzi  kiongozi  wa zamu siku hiyo, Mahija Swalehe alikemea tabia za waajiri wa wafanyakazi wa ndani kuwatesa na kuiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho la tatu ili kukomesha vitendo hivyo.
TUJIKUMBUSHE
Yusta alikumbwa na masaibu hayo kwa muda mrefu hadi hivi karibuni majirani wakiwa na polisi walipovamia nyumba hiyo na kumkamata bosi wake kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Oysteraby, Dar ambako anashikiliwa na yeye kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibu baada ya kukutwa na majeraha.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa ametiwa mbaroni.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger