Na Hudugu Ng'amilo
Waziri wa
Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya
nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo
wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha
kiduchu.
Ilielezwa
bungeni jana kuwa Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga,
Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya
maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa
ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Akichangia
Bajeti ya Wizara ya Maji jana, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu alihoji kile alichokiita upendeleo wa wazi katika ugawaji wa
fedha za maji, unaoipa kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.
Pia
aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi
kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa Sh1.9 bilioni na kusema:
"Upendeleo wa aina hii haufai kwa sababu utaleta matatizo na siyo haki
hata kidogo."
"Profesa
Maghembe atueleze sababu za kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa
isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito ya kudumu na mabwawa ya maana
imepewa bajeti kidogo ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya
maji," alisema Lissu.
Alisema
licha ya Profesa Maghembe katika hotuba yake kutaja mikoa ya Dodoma,
Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa inakabiliwa na upungufu wa maji,
imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku mikoa inayopata mvua za kutosha
na vyanzo vya uhakika vya maji ikitengewa mabilioni ya fedha.
"Dodoma
imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni
na Simiyu Sh2.8 bilioni, wakati mikoa yenye vyanzo vya maji na mvua za
kutosha imetengewa fedha nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni,
Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni na Mtwara Sh7.5 bilioni,"
alisema.
Lissu
alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa mawaziri hao wanatumia
mamlaka yao kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo utaratibu wa Serikali
ya CCM... "Kama utaratibu wa mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi tunaotoka
mikoa yenye ukame tutapataje maji?"
Jana
Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika wakati mgumu, baada ya kuandamwa
na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye alimwita kuwa ni
mzigo kutokana na kutokutolewa kwa fedha za miradi ya maji.
Mnyika
alionyesha kushangazwa na wabunge wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara
hiyo, licha ya kuwa ndogo na fedha za miradi zimekuwa hazitolewi kama
inavyotakiwa.
"Kwa
kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia Profesa Maghembe ambaye ni CCM.
Fedha zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara hii hazijatoka na za
bajeti hii hazitatoka kwa kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna bora
ya kumsaidia ili viongozi wa CCM wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa
bajeti hii ili Serikali irudi mezani na kujiuliza."
Mnyika
alisema kuwa hata ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa Serikali
itaongeza Sh80 bilioni kwa wizara hiyo kabla ya Mei 31 mwaka huu nayo
haijatekelezwa na kusisitiza kuwa wabunge wakiipitisha bajeti hiyo
watakuwa wameuziwa mbuzi kwenye gunia.Alisema kuwa hata miradi ya maji
jijini Dar es Salaam ambayo Profesa Maghembe aliahidi kuwa itakamilika
mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Mbunge wa
Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alisema Profesa Maghembe
amechota mabilioni ya fedha na kuyapeleka katika miradi ya maji kwenye
jimbo lake la uchaguzi wakati maeneo mengine ameyaacha licha ya kuwa
yana kipaumbele na kwamba anatumia miradi ya Serikali kujinufaisha
kisiasa.
"Ukitaka
takwimu zote ninazo hapa, idadi ya watu kwako ni wachache kuliko hata
kwangu lakini kwa vipindi viwili mfululizo umekuwa ukijitengea mabilioni
ya fedha, wewe ni mzigo kabisa," alisema Silinde.
Mwandosya amtetea
Wakati
akijibu hoja za wabunge, Profesa Maghembe hakugusia tuhuma hizo na
badala yake Profesa Mwandosya alimtetea akisema miradi hiyo katika
wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye (Mwandosya) akiwa
Waziri wa Maji... "Si kweli kwamba Profesa Maghembe anapendelea jimbo
lake kwa sababu hakuwa waziri wa wizara hiyo wakati mradi huo
unaanzishwa. Wananchi wa Same, Mwanga, Korogwe na Simanjiro wana haki ya
kupata maji kama wananchi wa sehemu nyingine yoyote. Mwacheni waziri
atekeleze majukumu yake ili watu hawa wapate maji".
Alisema
mradi wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe ni muhimu sana kwa sababu
utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 400,000 ambao hawapati maji
kabisa.
Alisisitiza
kuwa yuko tayari kubeba lawama juu ya mradi huo na si Profesa Maghembe,
kwani waziri huyo anafanya kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo ambao
ulikuwapo hata kabla hajapelekwa katika wizara hiyo.
CHANZO MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment