NAIBU
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni amesema askari
wa usalama barabarani watakaobainika kupokea rushwa watashughulikiwa kwa
kuwa wataweka mitego kwa ajili ya kuwakamata.
Alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia askari hao kuwa wanapenda rushwa na ndio chanzo cha ajali barabarani na kwamba wanachafua taswira ya jeshi hilo.
Akizungumza
na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam jana jijini humo, Masauni alisema mtego watakaouweka ndilo kaburi
lao na kwamba watafungwa kwa sababu ya tamaa ya Sh 10,000, hivyo
wajihadhari.
Alisema
Taifa linakabiliwa na changamoto ya ajali za barabarani na kwamba wana
wajibu wa kuwalinda raia wa nchi hii, badala ya kushiriki kuwaangamiza
kwa tamaa ya fedha. Alisisitiza kuwa hawataweza kufikia uchumi wa kati
endapo nguvu kazi zitaendelea kupotea kutokana na ajali za barabarani.
“Kuondoa
ajali inawezekana na watu watakaoleta sababu za ajabu ajabu hiki sio
kipindi chake ni lazima tuzitekeleze kama tulivyopanga kwenye mkakati
wetu kwamba ndani ya miezi sita tuwe tumepunguza ajali kwa asilimia 10,” alisema akisisitiza askari kubadilika, kwani ndio wasimamizi wakubwa wa usalama barabarani.
Akizungumzia
changamoto zinazowakabili askari hao, alisema kuwa wapo baadhi ya
askari ambao wanafanya kazi katika mazingira hatarishi na magumu kama
vile kupigwa risasi, kugongwa na magari na kwamba jitihada zao
zinatakiwa zitambulike kwa kupandishwa vyeo na mishahara kwa kazi nzuri
wanazofanya.
Kamanda
wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema
mkutano huo ni sehemu ya kutoa elimu kwa askari watakaosimamia mkakati
huo kuhakikisha ajali zinapungua.
Naibu
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Abdulrahman Kaniki alisema ajali za
barabarani ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili Taifa.
Alisema
ni wakati wa askari kuongeza chachu, ari na mbinu katika kutekeleza
majukumu yao kwa wananchi na kwamba wapo imara kutekeleza maagizo halali
kutoka kwa viongozi wao.
0 comments:
Post a Comment