Aidha, wakati vyuo hivyo vikirudisha fedha hizo, ukaguzi wa kutafuta wanafunzi hewa uliofanywa ulibaini Sh. bilioni 3.85 zililipwa kwa wanafunzi hewa 2,192 kwa kipindi cha mwaka 2015/16, Prof. Ndalichako aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi.
Kiasi hicho cha fedha kiligundulika kulipwa wanafunzi hewa katika vyuo 29 kati ya 31 vilivyokaguliwa, alisema.
Akizungumza na Nipashe baada ya mkutano huo, Prof. Ndalichako alisema katika vyuo vilivyorudisha fedha hizo kabla ya ukaguzi, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kiliongoza kwa kusalimisha fedha nyingi zaidi - zaidi ya Sh. milioni 400.
Licha ya kurudisha fedha hizo, wakati wa ukaguzi ilibainika chuo hicho kina wanafunzi hewa 364 ambao kwa mwaka wa fedha uliopita, walilipwa Sh. milioni 460.96.
Katika orodha ya vyuo 31 vilivyokaguliwa, ni Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut-Mbeya) na Chuo Kikuu cha Biashara (CBE-Dodoma) tu ambavyo havikuwa na wanafunzi hewa.
Chuo ambacho kimebainika kutafuna kiasi kikubwa cha fedha baada ya ukaguzi, alisema Prof. Ndalichako, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) chenye wanafunzi 13,972 wanaopata mikopo, lakini kati yao, 350 ni hewa na walilipwa Sh. milioni 703.43.
Akifafanua juu ya fedha zilizorudishwa baada ya kutoka kwa tangazo la uhakiki wa wanafunzi, Waziri Ndalichako alisema sheria inataka fedha zikikaa siku 30 bila kuchukuliwa, zirudishwe Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
“Lakini hilo lilikuwa halifanyiki, ila tulivyosema tunakagua, fedha hizo zilirudishwa ndani ya muda mfupi,” alisema.
MAREHEMU, WALIOFUKUZWA
Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alisema fedha za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zimeshatolewa.
Alisema awali aliagiza utoaji fedha hizo usimame baada ya kubaini takribani wanafunzi 600 kati ya waliokuwa wanaombewa fedha hizo walikuwa ama marehemu, waliofukuzwa vyuo na walioacha.
“Mwanzo nilitaka vyuo viniletee orodha ya wanafunzi wao waliopo chuoni na ambao hawapo kwa sababu mbalimbali, zile taarifa nikazipeleka Bodi ya Mikopo,” alisema.
“Baadaye (vyuo) vikaleta orodha ya wanaotakiwa wapewe fedha za mafunzo kwa vitendo, kwa haraka haraka tu mimi nikaona kama (wanafunzi) 600 ambao baadhi yao ni marehemu, wengine wamefukuzwa chuo na wengine wameacha.
“Ndipo nikasema zoezi lile lisimame kwanza na uhakiki ufanywe na vyuo na wakuu wa vyuo wasaini kabisa.
” Waziri huyo alieleza kuwa ‘madudu’ hayo yamebainika kwenye ukaguzi uliofanywa na kitengo cha ukaguzi wa ndani cha HESLB kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Baada ya hatua ya kwanza ya ukaguzi, sasa sehemu ya pili itaendelea ili kumaliza vyuo vyote 81 vilivyopo nchini,” alisema.
Alisema wanaohusika na mtandao huo watakabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi, na kwamba baadhi ya maofisa mikopo wa vyuo mbalimbali na wahasibu wamepewa barua za kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua.
Alisema hatua zaidi zitaendelea kwa kuwa ‘ulaji’ huo una mtandao mpana, kuanzia wanaotengeneza majina ya wanafunzi waliomaliza vyuo, kujumuisha waliofariki, kuacha ama kufukuzwa na kuyapeleka bodi ya mikopo. Prof. Ndalichako pia alisema wamebaini benki zina urasimu mkubwa katika kutoa fursa kwa wakaguzi wa kazi hiyo.
0 comments:
Post a Comment