Sunday 31 December 2023

MWAKA 2024 PUNGUZA MAZOEA NA WATU ULINDE HESHIMA YAKO

 
Mwaka 2024 Punguza Mazowea na Watu Ulinde Heshima Yako!


Denis Mpagaze
_______________________

Usiruhusu watu wakuzoee sana, wakikuzoea watakuona wa kawaida, wakikuona wa kawaida watakudharau, wakikudharau, watakuharibia.

Siku zote anayekuharibia ni aliyekuzowea, anayekujua sana, anakuona wa kawaida sanaa, hakuogopi! Anakumudu!

Asipokuogopa hataona uzuri wako, akiukosa uzuri wako atashughulika na madhaifu yao, atayasambaza kwa watu wakuone mtu wa hovyo!

Akifanya hivyo umekwisha; wengi wameumia sana kwa sababu walikubali kuzoeleka, walikubali kuwa cheap.

Usiwe hivyo. Jitahidi kuwa adimu, siyo kila mtu anakuita ita kama mafungu ya nyanya na viazi sokoni na wewe unaitika na kwenda. Utaharibu!

Be adimuπŸ˜„πŸ˜„. Vitu vya thamani viko adimu. Havionekani kirahisi. Vimejificha! Vinavyoonekana kirahisi ni vile cheap!

Mungu ameendelea kutukuzwa na kuheshimika kwa sababu haonekani. Amejikalia zake Mbinguni. Hakuna anayejua hata sura yake. 

Angekuwa anatembea mitaani, tunakutana naye kila siku, anapanda na daladala kabisa tusingempa hiyo heshima. 

Alituletea Yesu tukamzowea, tukamuona wa kawaida, tukamdharau mpaka tukamuua. Binadamu ni wema wasipokuzowea. Ni hatari wakikuzowea.

Hata Mungu nakwambia siku akija hapa duniani tukamzowea kuna watu watafanya majaribio ya kumuua!πŸ˜„πŸ˜„ Hakuna kiumbe hatari kama binadamu. 

Kitu chochote kinachopatikana kwa nadra kinathamani kubwa. Madini yanapatikana kwa nadra sana na yapo ardhini.

Kaa mbali na nguru mbili. Ukikaa mbali heshima inakuja. Jitahidi kuwa mtu wa kutopatikana kirahisi.

Ikitokea mtu amekutana na wewe basi iwe ni kwa mambo ya msingi sana. Siyo unaitwa oi, umeishaitika na kuondokaπŸ˜„πŸ˜„πŸ˜„.

Wazungu wanasema keep distance. Jitahidi kutopatikana popote wakati wote na kwa watu wote. 

Distance ndiyo inatengeneza hadhi ya mtu, usiwe mtu wa kujumuika na watu hovyo hovyo. Angalia kama kuna tija ya kujumuika. Kama ipo nenda, haipo acha! 

Ukiwa mbali na mtu ni rahisi kumpenda na kumfurahia na kuwa na kiu naye zaidi, hata dharau na machukizo hutaviona.

Mama yetu alipenda kusema mkitaka kupendana na kuheshimiana msiishi kwa ndugu zenu, na mkienda kutembea kaeni siku chache, ondokeni.

Ukiwa mtu wa kukeep distance watu watakwambia una nyodo, lakini  ndo ukweli. 

Katika kitabu cha Robert Green "The 48 Laws of Power" by Robert Greene, sheria ya 16 inasema use absence to increase respect and honour.

_"Too much circulation makes the price go down: The more you are seen and heard from, the more common you appear. Create value through scarcity._"

Hata bidhaa zikiwa nyingi sokoni zinashuka bei. Zikiadimika bei inapanda. Bora kujiweka mbali kidogo. Acha wakuone unaringa kikubwa wakuheshimu. 

Kuna watu mahusiano yenu yaishie kwenye salamu tu, mengine kuhusu wewe wasijue. 

Ikiwezekana wasijue unakoishi, wasijue familia yako, wasijue elimu yako, wasijue kazi yako, wasijue miradi yako, wasijue mkeo, wasijue mume wako.

Wakijua watakuzowea, wakikuzowea siku ukanunua hata gari watakununia na wakati gari lenyewe la mkopo, hawajui kama una maumivu ya kulipa mkopo.

Watakununia kisa umehamia kwenye nyumba yako, watakuchukia kisa umepanda cheo, ukizubaa wanakuua kabisa. Waulize wapanda vyeo mazonge wanayokutana nao!

Usiwaonyeshe watu ng'ombe anayekupa maziwa, watampa mifuko ya plastiki afe ukose maziwa, uteseke!πŸ˜„πŸ˜„πŸ˜„

Kutokuwa na mazoea mazoea na watu kunaeshimisha sana. Lazima ujiwekee mipaka. Mazoea husababisha kukoseana heshima.

Mtu akizoea biashara yako hatakulipa. Atakuwa mtu wa kukopa na kuchelewa kulipa. Wakati mwingine atataka umpe bure.

Hizi lugha za huyu ni mtu wangu hapana. Heshima kwanza.

Usipende kila mtu ajue unaishije hapa mjini ndo maana wahenga wakasema siri ya mtungi aijuae kata.

Mazoea ni mazuri kwa watu yanaleta ukaribu ila ni mabaya kuliko unavyoyafikiria. Hii ni ngumu kumeza ila ndo umeze tu.

Watu wakikuzoea sana wataanza kukuomba hela bila adabu. Wasipokuzowea hawakuombi. Wataishia kusema siwezi kumuomba yule baba kwa sababu sijamzoea. Good!

Watu wakikuzoea sana wataingia ndani kwako bila kupiga hodi na kwenda kula vitu kwenye friji. Hapo wanakusababishia mtikisiko wa bajeti hasa kama unatoka katika jamii zetu za kula kwa manati! 

Mazoea ni chanzo cha migogoro mingi. Waliozoeana ndiyo wagombanao. Mazoea ni fimbo ya maangamizi yako. Jaribu kuyakacha.

Kijana mmoja alikuwa mtaani na mama yake, rafiki yake akamwambi, oya bado hujaacha tabia yako ya kula wamama! Ayiii! Mazowea ni hovyo sana!

Ofa ya Sikukuu inaisha. Changamka. Ni vitabu 10 kwa Sh 20,000. Ni softcopy. Mpesa 0753665484.

Cheers
Mwl. Denis Mpagaze
Muhenga wa Karne ya 21!


Share:

WAKAZI KAWE WALIA NA UKABAJI NYAKATI ZA JIONI

 

......................

Na Mwandishi Wetu

Wakazi wa mtaa wa Kawe Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam, wameliomba Jeshi la Polisi nchini kuongeza ulinzi hasa nyakati za jioni eneo la Tanganyika pekazi kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukabaji na unyanganyi kwa kutumia silaha husani za jadi unafanywa na vijana wanajitambulisha kama Ulinzi Shirikishi kabla ya kumuibia mhusika.

Wamedai kuwa ukikutana nao hujitambusha kama watu wa usalama na baada ya hapo hutekeleza uovu huo kwa kukutolea mapanga,Visu,Nondo, na kumuibia muhusika.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa mtaa huo ambao wawili walikataa kutotajwa kwa majina, wamedai kuwa kumekuwepo kwa vitendo hivyo katika eneo hilo ambalo ni karibu zaidi na kituo Cha Polisi Kawe.

Wamedai hivi karibuni mmoja wa Askari wa Jeshi anadaiwa kukabwa akiwa na mpenzi wake katika eneo hilo jambo ambalo linaongeza wasiwasi miongoni mwao.

Williams Nashoni ni mmoja wa mkazi wa mtaa huo amesema kuwa kumekuwepo kwa vitendo hivyo kwa kiasi kubwa japo hivi karibuni vimepungua kutokana na baadhi ya walinzi wa mchungaji Mwamposa kuongeza walinzi hata hivyo akidai bado jitihada zinatakiwa kuongezwa kutokana na walinzi hao kutokuthi mahitaji .

Nashoni amesema kinachowaumiza ni vitendo hivyo kutokea eneo ambalo si mbali na kituo cha Polisi Kawe huku akiwaomba wahusika kujitathimini.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Acp, Mtatiro Kitinkwi amesema kuwa wamejipanga kuendeleza kudumisha ulinzi na usalama eneo nzima la mkoa wa kipolisi ikiwemo Kawe na Tanganyika Pekazi.

Amedai kuwa kuelekea Mwisho wa mwaka Kuna tukio la mkesha Tanganyika pekazi na wao kama Jeshi wamejipanga kuongeza ulinzi na usalama ili kuhakikisha hakuna vitendo viovu havijitokezi hata kwa bahati mbaya.

Amesema kuwa taarifa zote za uhalifu wanazipokea na watahakikisha wanazifanyia kazi ili kuhakikisha ulinzi na usalama kwa raia unaimarika zaidi.

Amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa zote za uhalifu katika mkoa huo ili kuwarahisishia kazi na kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.

Share:

SHUWASA YATOA CHAKULA KWA WENYE UHITAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imewakumbuka watu wasiojiweza katika Manispaa ya Shinyanga kwa kuwapa zawadi za mwaka mpya ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Zawadi hizo zimejumuisha mchele, mafuta ya kupikia, sukari na sabuni ambapo jumla ya watu 13 wamepatiwa msaada huo ambapo zawadi hizo ni mchele kilo tano, sukari kilo mbili, mafuta ya kula lita tatu na sabuni miche miwili.

Aidha SHUWASA imekuwa ikiwasaidia watu hao wenye uhitaji ikiwa ni pamoja na kuwalipia bili za maji za kila mwezi.









Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI DESEMBA 31,2023. .... FUNGA MWAKA

 


Magazeti ya kufungia mwaka 2023

Share:

Saturday 30 December 2023

KC HALMASHAURI YA WILAYA YA UBUNGO WACHAMBUA BAJETI YENYE MLENGO WA JINSIA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) Kupitia vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Ubungo wamekutana kuichambua bajeti ya 2023/2024 yenye mlengo wa Jinsia ambapo wameangalia katika upande wa miundombinu ya Elimu,  Afya, Maji,Kilimo na Miundombinu ya barabara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 30,2023 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kituo Cha Taarifa na Maarifa  kata ya Manzese Bi. Theresia Lehanjara amesema kuwa kwenye maeneo ya elimu wameangalia miundombinu ya shule, kupatikana kwa vyumba vya kujisitiri kwa wasichana, uwiano wa matundu ya vyoo pamoja na uwepo wa vyoo kwa wenye ulemavu.

Aidha wameipongeza halmashauri ya Wilaya hiyo kwani imekuwa ikileta matumaini mazuri hasa kwenye eneo la elimu, wamewekeza fedha za kutosha katika kuimarisha miundombinu ya shule kwenye maeneo mbalimbali.

“Licha yakuwa kuna maeneo ambayo bado kuna changamoto, tunaamini mpaka kufikia mwezi wa sita matarajio mengi yatakuwa yamefikiwa kama watakuwa wamewekeza nguvu kwa wale watendaji”. Amesema

Amesema kuwa katika Wilaya yao hakuna uwiano sawa wa walimu wakuu wakike na wakiume ambapo imechangia changamoto kubwa ya kutatua mahitaji ya mtoto wa kike anapokuwa shuleni,ambapo wamebainisha pia kuhusiana na Miundombinu ya madarasa kubadilishwa kuwa maabara ingawa madarasa hayajitoshelezi.

"Tunaomba basi kama Wizara inawaamini wanawake, inapaswa kuwawezesha hawa wanawake wanapochaguliwa kuwa wakuu wa shule, tusisikie habari ya kwamba mwanamke amechaguliwa amekataa kuitumikia ile nafasi, kwanini wanaume wakipata nafasi wanapata uhamisho wao na wenzi wao. Jambo jingine ni madawati na majengo wanataka kuboresha maktaba kwenye mashule yetu tulipokua tukiangalia bajeti tunaomba wasipunguze madarasa kuwa maktaba maana majengo yaliyopo hayajitoshelezi". Amesema 

Vilevile amesema kuwa  bado wanakabiliwa na changamoto ya wodi ya wakinamama wajawazito kwa ajili ya kujifungua wanapohitaji huduma hiyo ambapo serikali inatakiwa kushughulikia changamo hiyo kwa haraka.

Kwa upande wake Mwalimu wa Chuo Kikuu Cha Mzumbe Bi.Lihoya Chamwali amesema kuwa Bajeti yenye mlengo wa kijinsia ni muhimu ili kuhakikisha maendeleo yanamfikia kila mtu ambapo amesema wamebaini kuhusiana na suala la taulo za kike kuwa zimepungua kutoka Milioni mbili hadi kufikia Milioni Moja.

"Tulipewa ufafanuzi kuwa kuna pesa nyingine imetengwa na  hiyo ni kwaajili ya mapato ya halmashauri ya ndani, kuna pesa nyingine ambayo imetengwa kutoka vyanzo vingine hadi kufikia Milioni Kumi". Amesema Bi. Lihoya.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kituo Cha Taarifa na Maarifa Kata ya Mabibo Bw.Msafiri Mwajuma ameeleza kuwa bila miundombinu rafiki kwa mwanamke, haitawezekana kumuinua kiuchumi hivyo kunahitajika kutengeneza mazingira wezeshi.

Share:

KONDOA DC NA TGNP WAJADILI MAFANIKIO YA BAJETI YENYE MTAZAMO WA KIJINSIA


Na Mwandishi Wetu, Kondoa

Halmashauri ya wilaya ya kondoa, mkoani Dodoma, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, imeandaa bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia kwa kujenga miundombinu ya vyoo vya shule vyenye kukidhi mahitaji ya wasichana wanapokuwa kwenye hedhi.

Hayo yalibainishwa na Afisa Mipango wa Halmashauri, Joshua Mnyang’ali, alipokuwa akijibu taarifa ya uchambuzi wa Bajeti ya Halmashauri kwa mtazamo wa Kijinsia iliyofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa Kata ya Haubi.

“Choo tulichojenga shule ya Msingi Mwisanga na shule mpya ya sekondari ya Ntomoko, vina vyumba maalumu ya kujisitiri wasichana wanapokuwa kwenye hedhi, kichomea taka kwaajili ya kuteketeza taulo za kike ambazo zimetumika. Pia katika vyoo tunavojenga sasa, tunaweka sehemu ya haja ndogo kwa wavulana, lengo ni kupunguza msongamano kwenye vyoo, ili wanafunzi wafurahie kuwepo shuleni. Kwa kufanya hivyo tunapunguza pia utoro na kuongeza ufaulu”, alisema Mnang’ali.

Aidha naye mganga mkuu wa halmashauri, Dkt. Nelson Kimolo, amesema kwamba, Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24, imedhamiria kupunguza kabisa au ikiwezekana kutokomeza vifo vya mama na mtoto, kwa kutenga bajeti Zaidi ya shilingi Milioni 44 kwaajili ya kuwalipa madereva wa ngazi ya jamii watakaotumika kuwasafirisha Mama wajawazito kutoka zahanati kwenda Hospitali kubwa ili kurahisisha mfumo wa rufaa.

“Huu ni mradi unaojulikana kama M-MAMA ambao umeleta mabadiliko makubwa, unasaidia sana kuondoa tatizo la usafiri, magari tuliyo nayo ya kubeba wagonjwa hayatoshelezi, tumeona afadhal kuwa na utaratibu huu mpya wa kuingia mikataba na madereva waliko kwenye jamii, wahudumu wa Hospitali wawasilane nao muda wowote ili kuhakikisha Mama mjamzito anapata huduma ya haraka na kukokoa maisha yake”, alisema Dkt. Kimolo.

Awali akiwasilisha mapendekezo ya Jumla mwezeshaji wa Uchambuzi wa Bajaeti kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, pamoja na halmashauri kuwa na vyanzo vichache vya mapato ya ndani, bado wamejitahidi kuangalia eneo la afya na elimu.

Temba, ameongeza kwamba, bado kuna mapengo ya kijinsia kwenye Bajeti ya Halmashauri hasa katka eneo la ustawi wa Jamii ambapo Bajeti ya kuzuia na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia imetengwa kidogo, sambamba na Idara ya Maendeleo ya Jamii inayotakiwa kuwajibika katika uhamasishaji wa jamii kushiriki katika shughuli na maendeleo kutengewa fedha kidogo sana.

“Eneo la Ukatili wa Kijinsia, ni muhimu kuliangalia,tukiwekeza kwenye miundombinu ya elimu, alafu tusipoweka mikakati ya kuwalinda watoto wa kike na kiume wasifanyiwe ukatili wa Kijinsia na udhalilishaji wakingono, hatutapata matokeo mazuri”,alisema Temba.

Pia, eneo lingine lenye mapungufu ambalo Halmashauri imeshauriwa kuboresha na kuongeza msisistizo kwa viongozi wa vijiji na kata kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ili waweze kuibua fursa na vikwazo katika maendeleo (O&OD) ili waweze kushiriki vizuri katika kuisimamia na kuitekeleza miradi ya maendeleo.

Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutumia kiasi cha shs.milion 440 kuboresha vyanzo vya maji, sh. Milion 3, kujenga vichomea taka katika zahanati, sh. Million 23 kujenga mashimo ya taka mbichi (placenta pit) katika zahanati na vituo vya afya, ambapo Kituo cha afya mnenia kimetengewa bajeti ya sh. Milion 35 kwa ajili ya kujenga kichomea taka na vyoo.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), unatekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri ya Kondoa, inayolenga kujenga uwezo wa kwa jamii kupitia Kituo cha taarifa na Maarifa, kupata uwezo wa kuchambua masuala ya Kijinsia na kushawishi kuingzwa kwa masuala ya Kijinsia katika sera, mipango na miongozo.

 Sambamba na kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa Halmashauri kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uongozi bora na ushiriki wa wanawake katika uongozi.







Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger