Thursday 21 December 2023

VIONGOZI MAMLAKA YA MASOKO YA MITAJI BURUNDI WAFANYA ZIARA YA KIMAFUNZO TANZANIA

...
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA CPA. Nicodemus Mkama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kupokea ujumbe kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya mafunzo ya siku tano.
******************

Na Mwandishi Wetu, 

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Tanzania imepokea ujumbe kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya mafunzo ya siku tano.

Ujumbe huo utafanya ziara katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Kampuni za Usimamizi wa uwekezaji na watendaji wengine katika masoko ya mitaji huku ikielezwa ziara hiyo imelenga kujenga uelewa wa namna masoko ya mitaji yanavyoendeshwa.

Pia kuainisha masuala muhimu yatakayoiwezesha nchi ya Burundi kuwa na masoko ya mitaji imara, himilivu, yenye ufanisi na yatayowezesha kuwa na matokeo chanya katika kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi nchini Burundi kama ilivyo nchini Tanzania.

Akizungumza leo Desemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA CPA. Nicodemus Mkama amesema ujio wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, menejimenti na timu ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi umetokana na mafanikio yaliyopatikana katika masoko ya mitaji hivi karibuni nchini Tanzania.

Ameongeza ambapo bidhaa mpya na bunifu zinazowezesha kupata fedha za kutekeleza shughuli za biashara na miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi zimeidhinishwa na kuorodheshwa katika soko la hisa kwa mafanikio makubwa.

Amesema bidhaa hizo ni pamoja na hatifungani za kijani yaani green bond, hatifungani zenye mguso kwa jamii yaani social bonds, na hatifungani zenye kukidhi misingi ya Shariah yaani Sukuk bonds.

"Matokeo hayo yameiweka Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ulimwenguni yanayotoa bidhaa mpya na bunifu, zinazovutia wawekezaji wa ndani ya nchi na kimataifa, " amesema CPA. Mkama.

Ameeleza Masoko ya Mitaji Tanzania ni miongoni mwa masoko yaliyopata mafanikio makubwa kiutendaji barani Afrika, katika kipindi cha hivi karibuni. "CMSA, ambayo ni Mamlaka yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini ...

" Imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza serĂ¡ na mikakati mbalimbali ya serikali ambayo imewezesha kufikia mafanikio hayo.Mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kuongeza thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji.

"Ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 7.6 na kufikia shilingi trilioni 36.13 katika kipindi kilichoishia Novemba 2023, ikilinganishwa na shilingi trilioni 33.59 katika kipindi kilichoishia Novemba 2022."

Akielezea mafanikio yaliyopatikana, CPA. Nicodemus Mkama amesema yametokana na mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na kuwezeshwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, sera za uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa zinazotekelezwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia, zimekuwa chachu yenye matokeo chanya katika kukuza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na wakimataifa na hivyo kuleta mafanikio makubwa zaidi katika masoko ya mitaji nchini Tanzania.

Hivyo kuvutia Mamlaka za masoko ya mitaji kutoka nchni nyingine kuja kupata mafunzo kwa lengo la kuimarisha na kuongeza ufanisi wa Taasisi katika nchi zao, kama ambavyo CMA Burundi wamekuja kujifunza CMSA Tanzania .

CPA. Mkama pia amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu tathmini ya Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani East African Common Market, Tanzania imepanda viwango vya alama za tathmini kwa asilimia 157 kutoka alama 7 hadi alama 18 kati ya 20 na kuwa miongoni mwa nchi zinazotekelezaji vizuri itifaki ya soko la pamoja kwenye masoko ya mitaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki .

Kwa sasa, Tanzania hakuna vikwazo vya ushiriki wa wawekezaji wa kigeni katika soko la hisa, hatifungani za kampuni na mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

CPA. Mkama ameeleza katika kutumia fursa ya masoko ya mitaji ya ndani na ya kimataifa yanayowezesha kupatikana kwa fedha za kugharamia miradi na shughuli zinazochangia Utunzaji wa Mazingira, Maendeleo ya jamii na Utawala Bora CMSA imeidhinisha Kanuni za Soko la Hisa la Dar es Salaam yaani Stock Exchange Rules, ili kuwezesha uorodheshwaji na mauzo ya bidhaa hizo.

Maboresho hayo yameongeza mauzo na kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni na taasisi kupata fedha za kugharamia shughuli za biashara na maendeleo.Aidha maboresho hayo yameongeza matumizi ya bidhaa na huduma, hivyo kuongeza ukwasi kwenye masoko ya mitaji.

CPA. Mkama pia alieleza CMSA imetekeleza mkakati wa kuwezesha utoaji wa Hatifungani za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma ili kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa (Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya) na Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na Mamlaka za Maji na Mazingira kugharamia miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara.

"Jitihada hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi uliozinduliwa na Waziri wa.Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

"Jitihada hizo zimeiwezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga Tanga-UWASA kuwa Taasisi ya kwanza nchini kukidhi vigezo vya awali vitakavyoiwezesha kutoa hatifungani kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira.

Aidha, CPA. Mkama pia alieleza kuwa, Katika kuwezesha matumizi ya teknolojia, CMSA imeidhinisha mifumo ya Sim Invest na Hisa Kiganjani ambayo inawezesha kutoa huduma katika masoko ya mitaji kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuuza na kununua dhamana.

Hatua hiyo imewezesha kuongeza ushiriki wa wananchi mijini na vijijini katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja na soko la hisa.

Aidha, CMSA imeshirikiana na wadau kuandaa miongozo ya kuendesha na kusimamia bidhaa za mitaji halaiki yaani crowdfunding. Bidhaa hizi zitawezesha upatikanaji wa fedha kwa kampuni changa, ndogo na za kati.

Pamoja na hayo amesema CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu, hatifungani Rafiki wa mazingira, hatifungani za bluu na hatifungani za taasisi za Serikali.

Pia CMSA itaendelea kushirikiana na CMA – Burundi ili kufanikisha azma ya kuwa na masoko ya mitaji imara, yenye ufanisi na yanayochochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) Bwa.Allisen Mgenzi ameishukuru Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Tanzania kwa kuwapokea vizuri .

Bwa. Mgenzi amesema amekuja nchini Tanzania akiwa ameongozana na Wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya CMA-Burundi,Menejiment na timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya Mafunzo ya siku tano katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) nchini Tanzania,Soko la Hisa la Dare es Salaam (DSE),kampuni ya Usimamizi wa Uwekezaji na Watendaji wengine katika masoko ya mitaji.

"ziara yetu imelenga kujenga uelewa wa namna masoko ya mitaji yanavyoendeshwa na kuainisha masuala muhimu yatakayoiwezesha nchi ya Burundi kuwa na masoko ya mitaji imara,himilivu,yenye ufanisi na itakayozesha kuwa na matokeo chanya katika kuchochochea ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi nchini Burundi kama ilivyo nchini Tanzani'',amesema Mgenzi.

Mgenzi ameushukuru Uongozi wa CMSA Tanzania kwa kuwapokea vizuri na kuwaonesha namna ambavyo CMSA ilivyofanikiwa katika suala zima la kukuza soko la mitaji nchini Tanzania,lakini pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri na nchi ya Burundi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA CPA. Nicodemus Mkama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kupokea ujumbe kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya mafunzo ya siku tano.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) Bwa.Allisen Mgenzi kuhusu ujio wao kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya nchini Burundi (CMA – Burundi) unaojumuisha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya ziara ya mafunzo ya siku tano nchini Tanzania.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger