Showing posts with label NEWS. Show all posts
Showing posts with label NEWS. Show all posts

Tuesday, 5 May 2026

MISA TANZANIA YAHUDHURIA UWASILISHAJI WA BAJETI YA WIZARA YA HABARI BUNGENI DODOMA

Na Mwandishi wetu - Dodoma

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), leo imehudhuria kikao cha Bunge Jijini Dodoma kilichohusisha uwasilishaji wa mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

MISA Tanzania ilikuwa miongoni mwa taasisi za kihabari zilizoshiriki katika uwasilishaji huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za wadau wa sekta ya habari kufuatilia na kushiriki michakato ya maamuzi yenye athari kwa maendeleo ya tasnia hiyo nchini.

Taasisi hiyo iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Edwin Soko, ambaye alihudhuria kikao hicho kwa lengo la kufuatilia kwa karibu vipaumbele vya wizara hiyo, hususan katika maeneo yanayohusu uhuru wa vyombo vya habari, maendeleo ya wanahabari, na mazingira wezeshi ya utendaji kazi wa sekta ya habari.

Ushiriki wa MISA Tanzania katika kikao hicho unaakisi dhamira ya taasisi hiyo katika kuhakikisha uwajibikaji, uwazi, na ushirikishwaji wa wadau katika masuala muhimu yanayogusa sekta ya habari nchini.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE MEI 5,2026




Magazeti



Share:

Monday, 4 May 2026

MBUNGE MWAKIOJA ATANGAZA NEEMA YA SOKA WILAYA MKINGA





>Agawa vifaa vya michezo kwa timu zote zinazoshiriki Ligi ya wilaya ya Mkinga


Na Oscar Assenga, MKINGA

Mbunge wa Jimbo la Mkinga mkoani Tanga, Twaha Mwakioja, ameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo kuinua kiwango cha soka wilayani humo kwa kuwekeza katika elimu na maendeleo ya waamuzi pamoja na makocha.

Akizungumza wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii uliokwenda sambamba na uzinduzi wa Ligi ya Wilaya ya Mkinga, uliofanyika katika Uwanja wa Chamazi, Kata ya Matamba, Mwakioja alisema lengo lao ni kuwekeza katika michezo kwa vijana ili kuwapatia ajira, kuboresha afya zao, pamoja na kuimarisha amani, mahusiano mema na ushirikiano miongoni mwao.

Alieleza kuwa dhamira yao ni kuwashika mkono vijana ili waweze kupiga hatua kutoka ngazi ya wilaya, kwenda mkoa, kanda na hatimaye ligi za juu, huku yeye akiwa bega kwa bega nao kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Mbunge huyo alibainisha kuwa wamepata taarifa ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa makocha na waamuzi wenye sifa. Hivyo, wamejipanga kuwekeza katika mafunzo ya makocha ili kila kata iwe na angalau kocha mmoja mwenye ujuzi na mafunzo rasmi, pamoja na kuandaa waamuzi wenye vyeti ili kuboresha usimamizi wa michezo.

Alisisitiza kuwa uwekezaji huo utaenda sambamba na ushirikiano na Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga katika kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.

Aidha, alisema mpango wao ni kuhakikisha kila kata na kijiji kinakuwa na timu ya mpira wa miguu inayoshiriki ligi ya wilaya. Aliongeza kuwa watawekeza zaidi ili kuibua timu imara zitakazoweza kushiriki ligi za ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye Ligi Kuu, hatua itakayosaidia kuitangaza Mkinga katika ramani ya soka nchini.

Katika kuonyesha dhamira hiyo, Mwakioja alikabidhi jezi na mipira kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha na kusaidia maendeleo ya michezo wilayani humo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga, Fadhili Habibu, alisema ratiba ya ligi hiyo imeanza Mei 4 katika kituo cha Mkinga, huku kituo cha Maramba kikitarajiwa kuanza Mei 6 (Jumatano), ambapo kutakuwa na vituo vinne vitakavyochezwa katika Kijiji cha Maramba, ikiwa ni pamoja na mechi kati ya Viva Dynamo na Maramba FC.

Habibu alisema lengo la ligi hiyo ni kusimamia na kuibua vipaji vya vijana, pamoja na kuwapa mwelekeo wa maendeleo yao kisoka. Alimshukuru mbunge kwa kujitoa na kushirikiana nao katika kufanikisha malengo hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Mkinga, Hassan Zumo, alimpongeza mbunge kwa juhudi zake za kuendeleza michezo wilayani humo, akieleza kuwa hatua hiyo imeongeza hamasa na matarajio ya ushindani mkubwa katika ligi hiyo, hasa baada ya timu kukabidhiwa vifaa.

Zumo aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2008, wamekuwa wakipeleka vilabu katika mashindano ya ngazi ya mkoa lakini wamekuwa wakikwama kutokana na changamoto za kifedha. Hata hivyo, alisema kupitia uongozi wa Mbunge Mwakioja, wana matumaini ya kupata timu itakayoweza kufika hadi Ligi Kuu.

Aidha, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimeahidi kujituma na kupambana kwa juhudi zote ili kuhakikisha ligi hiyo inaleta mafanikio na tija kwa vijana wa Wilaya ya Mkinga.

Share:

POLISI WATOA ONYO KALI DHIDI YA MATUMIZI MABAYA YA MITANDAO YA KIJAMII



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakati matumizi ya mitandao ya kijamii yakiendelea kukua kwa kasi na kuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kijamii na kiuchumi, changamoto ya matumizi mabaya ya majukwaa hayo imeanza kuibua wasiwasi kwa jamii huku Jeshi la Polisi likionya na kuanza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi, Dodoma,pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kudhibiti uhalifu kupitia ushirikiano na wananchi, bado kuna baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya vitendo vinavyokiuka maadili na sheria, ikiwemo utapeli, matusi, udhalilishaji na uchochezi.

Jeshi hilo limeeleza kuwa hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari, huku matukio machache ya kihalifu yakishughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Msemaji huyo anebainisha kuwa wahusika wa makosa ya mtandaoni wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ambayo imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kudhibiti uhalifu wa kidijitali nchini.

Amefafanua kuwa Katika operesheni za hivi karibuni, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu katika mikoa ya Arusha, Iringa na Mbeya kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii, ikiwemo kutoa lugha za matusi dhidi ya watu mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025.

Aidha, Jeshi hilo limeeleza kuwa msako dhidi ya watuhumiwa wengine unaendelea, hasa wale wanaohusika katika kusambaza maudhui ya kashfa, chuki na upotoshaji wa taarifa, hata kama si waanzilishi wa maudhui hayo.

Katika hatua nyingine,jeshi hilo limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kudhibiti uhalifu huo, huku wakihimizwa kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuzingatia sheria za nchi.

Aidha jeshi la Polisi limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka sheria, bila kujali nafasi au hadhi yake katika jamii.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATATU MEI 4,2026



Magazeti





















Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger