Monday, 30 September 2019

Waziri Lugola Aagiza Askari Wote Kituo Cha Polisi Wahamishwe

Na Felix Mwagara, MOHA-Katavi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Katavi, kuwahamisha askari wote wa Kituo cha Polisi Majimoto kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili askari hao.

Waziri Lugola alitoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Mji wa Majimoto, Wilaya ya Mlele wakati akijibu kero mbalimbali za wananchi.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Lugola alisema kero zilizowasilishwa na wananchi hao, zinaonyesha askari wa kituo hicho wanajihusisha na vitendo mbalimbali vya rushwa, kupiga wananchi ovyo, kushindwa kudhibiti ulinzi na usalama pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi.

“Natoa agizo hili liwe fundisho kwa askari wote wasiowaaminifu kote nchini, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huu natoa siku saba askari wote wa kituo hiki wahamishwe na waletwe wengine ili wajifunze,” alisema Lugola.

Baada ya agizo hilo, waendesha bodaboda na wananchi wengineo, walishangilia na kusema kuwa mji huo sasa utatulia kutokana na uwepo wa amani bila kuwa na manyanyaso.

Mmoja wa wananchi aliyetoa malalamiko dhidi ya polisi katika kituo hicho ni Malewe Maswe, alilalamikia kuwa baadhi ya askari hao walimpiga na kumsababishia maumivu makali ya miguu kutokana na kuhoji kosa lake la kuletwa kituoni hapo baada ya kugombana na mwalimu mmoja katika mji huo.

“Tulikuwepo na Mwalimu niliyegombana naye kituoni hapo, askari wakaniambia nendeni mkaelewane na mwalimu huyo, nikawaambia hatuwezi elewana maana zoezi hilo lilishindikana, askari wakasema unatufundisha kazi, yule pale dogo (askari ambaye alikuwa katika mkutano huo) simjui jina lake alinipiga kipigo sana, na askari mwingine bonge anachochea hii ndiyo Serikali ya Magufuli,” alisema Maswe.

Aidha, Waziri Lugola alijibu kero mbalimbali, ikiwemo ya Mkazi wa Mji huo, Malugu Mayombi ambaye ni mkulima maarufu wa mpunga wa eneo hilo, aliangua kilio kwa waziri akidai polisi wameshindwa kushughulikia kesi yake ya madai ya shilingi milioni sitini (6000,000/-) anazomdai mfanyabiashara Sali Kulwa maarufu TBS aliyemuuzia gunia 623 za mpunga.

“Waziri wangu, naomba unisaidie mimi maskini, ujiowako utaniokoa, nakuomba Waziri unisaidie nadai shilingi milioni 33 na laki 5 kati ya shilingi milioni 60 nimelipwa shilingi milioni 26 na laki 5 pekee, nimeshindwa kuendeleza kilimo naishi kwa shida, nilikuwa nalima ekari 100 kwasasa nalima ekari 30 tu nisaidie jamani, nateseka mimi,” alisema Mayombi.

Waziri Lugola alimuagiza Kamanda wa Polisi kushirikiana na Mkuu wa Polisi Wilaya kulitatua suala hilo kwa muda wa wiki moja wamkamate mtuhumiwa na aweze kumlipa fedha za Mayombi.

Waziri Lugola amemaliza ziara ya siku tano Mkoani Katavi, na ameelekea Mkoani Rukwa kuendelera na ziara ya kikazi akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika mikutano mbalimbali ya hadhara mkoani humo.


Share:

WAMILIKI WA MAKANISA,BAA NA KUMBI ZA STAREHE WANAOPIGA 'MUZIKI MNENE' WAPEWA ONYO KAHAMA


Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imetoa onyo kwa wamiliki wa baa na kumbi za starehe za usiku ambazo zipo katikati ya makazi ya watu ambazo zinapiga muziki kwa sauti ya juu sambamba na kuzifungia kwa kukiuka sheria na kusababisha kero kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana Septemba 29,2019 na Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na namna wanavyotekeza suala hilo la uchafuzi wa mazingira unaofanywa na upigaji kelele katika vilabu vya usiku.

Amesema wamebaini wengi wao wan aleseni ambazo haziwaruhusu kuendesha biashara ya usiku katika maeneo yao kutokana na kutokidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na kumbi ambazo hazitoi kelele ya muziki nyakati za usiku.

“Zipo baa na klabu ambazo zinajinasibu kwa ni night club lakini hazina sifa hizo na zipo zimejengwa katikakati ya makazi ya watu nab ado zinaendelea kupiga muziki kwa sauti ya juu,hatutakubali kuona uchafuzi huu wa mazingira ukiendelea”alisema Macha.

Katika hatua nyingine Macha alisema serikali inaheshimu sana madhehebu ya dini lakini katika wilaya yake yapo baadhi ya makanisa yamejengwa katikakati ya makazi hali ambayo imekuwa ikisababisha malalamiko kwa baadhi ya wapangaji ambao sio waumini wa madhehebu hayo.

Alisema baadhi ya makanisa hayo yamekuwa yakifungua muziki wa sauti ya juu katika makanisa hayo nyakati za usiku na kusababisha usumbufu kwa watu wengine hususani wagonjwa.

“Kuna sehemu tumetembelea na kukuta vifaa vipo tu pekee na vikiendelea kupiga muziki tuu bila ya kuwepo kwa waumini wa madhehebu hayo katika nyumba hizo”,alisema Macha.

"Tunawashauri viongozi wa dini kujenga makanisa yao katika maeneo ambayo yametengwa na Halmashauri ili kuondoa migogoro kwa wananchi",alisema.
Share:

LUGOLA AAGIZA ASKARI WOTE WA KITUO CHA MAJIMOTO WAHAMISHWE.... WANANCHI WATAKA MKUU WA KITUO ABAKI

Na Adelina Ernest - Malunde 1 blog
Waziri wa mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola ametoa siku saba kwa Polisi Mkoa wa Katavi kuwahamisha askari wote wa kituo cha Polisi Majimoto kwa madai kushindwa kushugulikia kutatua kero za wananchi pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Lugola alitoa agizo hilo jana jioni Jumapili Septemba 29, 2019 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Majimoto Halmashauri ya Mlele mkoani Katavi wakati akijibu kero za wananchi ambao walieleza kuwepo kwa kero lukuki katika kituo cha polisi Majimoto hali iliyomlazimu kuagiza askari wote 15 wa kituo hicho kuondolewa.

Waziri Lugola alisema kupitia kero zilizowasilishwa na wananchi, zinaonyesha wazi askari hao 15 wanajihusisha na rushwa, kupiga wananchi ovyo wakiwemo bodaboda, kushindwa kudhibiti ulinzi na usalama na kutoshughulikia malalamiko ya wananchi.

"Nataka niseme haya kutoa mfano, ili iwe fundisho kwa wengine kote nchini, Kaimu kamanda, natoa siku saba askari wote wa kituo hiki wahamishwe na waletwe wengine ili wajifunze," alisema Lugola.

Baada ya agizo hilo, Waziri Lugola aliwauliza wananchi askari wote wanatakiwa kuhamishwa? ambapo walipinga mkuu wa kituo hicho Iddy Kombo asihamishwe badala yake wahamishwe askari wengine wote.

"Asihamishwe, asihamishwe, asihamishwe," walisema wananchi.

Awali mmoja wa wananchi wa Majimoto Malugu Mayombi ambaye ni mkulima wa zao la Mpunga alieleza kero yake ya kutapeliwa Mpunga gunia 600 zenye thamani ya Sh.Milioni 60 na Mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Sali Kulwa maarufu kama TBS lakini jeshi la Polisi limeshindwa kumpa msaada.

Hata hivyo amewataka kutimiza wajibu wao kama Jeshi la Polisi na kuhakikisha hali ya usalama unaimarika katika kata hiyo kwani maendeleo huambatana na ulinzi na usalama wa kutosha.
Share:

TMDA YAENDESHA MAFUNZO YA SIKU TANO KWA WAKAGUZI WA DAWA WA MKOA WA PWANI
Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) inaendesha mafunzo maalum ya siku tano kwa wakaguzi  wa dawa wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani yanayoendana na kuzingatia maadili, uweledi pamoja na uelewa wa kanuni na sheria ikiwemo suala la usimamizi wa  dawa zenye asili ya kulevya  ili kuhakikisha kuwa zinatumika  kwa matumizi yanayotarajiwa na si vinginevyo katika kulinda Afya za Jamii.


Awali akifungua mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Baraza la Wauguzi na Ukunga (TNMC) Kibaha Mkoani Pwani,   mgeni rasmi ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba amewapongeza TMDA kwa hatua hiyo kwani imekuja kipindi muafaka kwa watalaam hao  kwani mkoa huo umejipanga kuwa kitovu cha viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na viwanda vingine.

“Mkoa wa Pwani unaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vikiwemo vya kawaida na vya dawa. Wataalam wetu wekitoka hapa watakuwa msaada na kuongeza chachu ya kuwezesha ukaguzi na ufuatiliaji  na kutimiza wajibu wao.

"Pia naamini  mtajifunza mbinu za kukabiliana na dawa na vifaa tiba duni na bandia  na utoaji wa taarifa kuhusiana na madhara yatokanayo na madhara ya matumizi ya bidhaa za dawa.” Alieleza Dk.Kamba

Aidha, Dk. Kamba alisema kuwa, katika dhana ya viwanda, Mkoa wa Pwani umekuwa mstari wa mbele katika kuvutia wawekezaji wa viwanda hususani vya dawa na vifaa tiba.

“Mpaka sasa tuna viwanda sita ambavyo vimeanza kujengwa tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani. Viwanda hivi vitaongeza ajira kwa wananchi wa Mkoa wetu lakini pia kuzuia fedha zetu kwenda nje kufuata dawa ..naamini tutapiga hatua na tutaendelea kutimiza wajibu wetu” alimalizia Dk. Gunini.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki  wa TMDA,  Adonis Bitegeko ameeleza kuwa mafunzo hayo yatalenga kwenye utendaji sahihi na uelewa kama taratibu za Mamlaka zinavyolenga.

“Katika uzoefu wa kufanya ukaguzi imeonekana mapungufu kwa baadhi ya wakaguzi wetu hivyo katika mafunzo haya tutajitahidi wakaguzi waelewe na watambue namna ya kubaini dawa duni na  bandia pia washiriki watapatiwa mafunzo ya kuzingatia miongozo katika ukaguzi wa viwanda vinavyozalisha na dawa na vifaatiba ili kuwezesha uzalishaji wa dawa bora, salama na fanisi alisema Adonis Bitegeko.

Nae Mratibu wa ofisi za Kanda  na Halmashauri za TMDA, Dkt. Henry Irunde akisoma taarifa ya utangulizi ya mafunzo hayo, akimwakilisha Mkurugenzi wa TMDA, alibainisha kuwa, jukumu kubwa la watalaam hao kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi zao katika kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi katika dawa na vifaa tiba nchini.

“ufanisi wa dawa na vifaa tiba ni jambo muhimu sana  katika kuboresha afya ya jamii. Hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya dawa zinazotumika nchini zinatoka nje ya nchi. Pamoja na kwamba udhibiti katika vituo vya forodha na katika soko umeimarishwa, bado kuna changamoto ya uwepo wa dawa duni, bandia na ambazo hazijasajiliwa hivyo dawa hizi hazina  budi kufuatiliwa na kuondolewa  kwenye soko hivyo mafunzo haya tutapata wakaguzi wenye weledi katika kutambua dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi pamoja na kuhamasisha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini” Alisema Dkt. Irunde.


 Mafunzo hayo ya siku tano  yaliyoanza Septemba 30, yanatarajiwa kufikia tamati Oktoba 4, mwaka huu huku yakizingatia masuala muhimu  kwa wakaguzi hao ni pamoja na kuwakumbusha maadili na taratibu za kazi katika kutumiza majukumu yao. Pia uwelewa wa kanuni za uzalishaji pamoja na miongozo ya usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.
Share:

RAIS MAGUFULI : NIMEONGEZA SIKU 7 TENA ZA KUOMBA MSAMAHA KWA WAHUJUMU UCHUMI..SIFANYI KAZI YA KITOTO WASIDANGANYWERais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, ameongeza siku 7 zingine kwa watuhumiwa wa makosa ya Uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha, kuendelea kuwasilisha maombi ya kuomba radhi kwa Mkurugenzi wa mashtaka (DPP),ili waweze kusamehewa na kuachiwa huru.

Maamuzi hayo ameyatoa leo Septemba 30, 2019, Ikulu jijini Dar es salaam, wakati akipokea taarifa ya maombi ya Watuhumiwa wa Uhujumu Uchumi kutoka kwa DPP,ambapo hadi sasa jumla ya maombi 467 yamekwishawasilishwa.

"Najua una barua nyingine zimekwama kwenye Ofisi za Mkoa, na kama kweli wapo waliokwamishwa kwa sababu ya umbali, nimeongeza tena siku 7 ili usije ukaniomba tena, katika siku 7 wapo ambao walizuiliwa na Maofisa na Magereza akitaka hongo kidogo, Kamishina wa Magereza upo hapo mkafuatilie walioomba msamaha kwa DPP ili msiwakwamishe'' amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa "natoa wito kwa Watanzania wenye tuhuma za uhujumu uchumi, wasiwe na wasiwasi ukishakiri basi kesho ndiyo ushahidi huo, siwezi nikafanya kazi ya kitoto ya namna hiyo nimeshasema nimetoa msamaha ni msamaha kweli, kwa hiyo wasidanganywe''

Mapema wiki iliyopita wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Magufuli alishauri na kutoa siku 7 kwa DPP, kukutana na watuhumiwa wa uhujumu uchumi na kwa wale ambao watakuwa tayari kukiri makosa yao na kukubali kuzirudisha fedha hizo basi waachiwe huru.

TAZAMA HOTUBA YA RAIS MAGUFULI HAPA

Share:

Waziri Mkuu Kuanza Ziara Ya Kikazi Ya Siku Tatu Mkoani Singida

Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Singida na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi alisema ziara hiyo ataianza Oktoba 4, 2019 na Oktoba 7 atafungua rasmi maonesho ya pili ya viwanda vidogo vidogo (SIDO) yatakayofanyika kitaifa mkoani humo.

NCHI sita za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinatarajiwa kushiriki maonesho hayo ambazo ni Kenya, Burundi, Ruanda, Uganda, China, India na Afrika kusini.

Dkt.Nchimbi alisema maonesho hayo yataanza kufanyika Oktoba 4 hadi 9 mwaka huu,na yatafunguliwa rasmi oktoba 7 na waziri mkuu Kassimu Majaliwa.

” Maonesho haya yatafanyika sanjari na maadhimisho ya wiki ya chakula duniani ambayo yatafanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 16 mwaka huu katika Viwanja vya Bombadier zamani Peoples” alisema Nchimbi.

Alisema kufanyika maonesho hayo mkoani Singida ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo ambao unakuwa kiuchumi kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na viwanda.

Pia alisema mkoa wa Singida wanajivunia kuchaguliwa kufanyika kwa maonesho hayo kitaifa na hii itawapa hamasa kubwa wananchi katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji kutokana na mazao yanayolimwa mkoani hapa.

Dkt. Nchimbi alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kupokea ugeni huo na kushiriki katika maonesho hayo.

Aidha mkuu wa mkoa alisema kabla ya kufungua maonesho hayo waziri mkuu Kassim Majaliwa atafanya ziara ya kikazi kila wilaya na halmashauri zote za mkoa huo na kuzungumza na wananchi pamoja na watumishi katika mkutano wa hadhara.

Katika ziara hiyo Majaliwa atatembelea miradi mbalimbali ya kimkoa na miradi mikubwa ya kitaifa, ambapo miradi ya kitaifa ni mradi wa kupokea na kupozea umeme uliopo katika halmashauri ya manispaa ya Singida pamoja na mradi wa daraja Sibiti linalounganisha mkoa wa Singida na Simiyu lililopo wilayani
Mkalama.


Share:

HOTUBA YA DPP BISWALO MGANGA ALIPOKABIDHI KWA MHE RAIS UTEKELEZAJI WA MSAMAHA WAHUJUMU UCHUMI NCHINI

Share:

HOTUBA YA RAIS DKT. MAGUFULI MARA BAADA YA KUKABIDHIWA UTEKELEZAJI WA MSAMAHA WA WAHUJUMU UCHUM

Share:

SCHOLARSHIP TENABLE IN KOREA AT THE ACADEMY OF KOREAN STUDIES STARTING FROM MARCH 2020

1.0 Call for Application The General Public is hereby informed that, the Academy of Korean Studies has granted a Scholarship programme to eligible Tanzanian Nationals to pursue Masters and Doctoral Degree programs at the Academy of Korean in the Republic of South Korea in the academic year 2019/2020. For further information visit the following link htt://intl.aks.ac.kr/english (AKS in… Read More »

The post SCHOLARSHIP TENABLE IN KOREA AT THE ACADEMY OF KOREAN STUDIES STARTING FROM MARCH 2020 appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

WIZARA YA ELIMU: SCHOLARSHIP FOR 2020 GLOBAL KOREA SCHOLARSHIP (GKS) FOR UNDERGRADUATE DEGREE

WIZARA YA ELIMU: SCHOLARSHIP FOR 2020 GLOBAL KOREA SCHOLARSHIP (GKS) FOR UNDERGRADUATE DEGREE 1.0 Call for Application The general public is hereby informed that, the National Institute for International Education (NIIED) under the Ministry of Education of the Republic of Korea is offering undergraduate study opportunity to a Tanzanian citizen for 2020 Undergraduate Global Korea Scholarship (GKS). 2.0… Read More »

The post WIZARA YA ELIMU: SCHOLARSHIP FOR 2020 GLOBAL KOREA SCHOLARSHIP (GKS) FOR UNDERGRADUATE DEGREE appeared first on Udahiliportal.com.

Share:

Taarifa Kwa Umma Kutoka Wizara Ya Maji
Share:

Rais Magufuli Atoa Tahadhari Kwa Watuhumiwa Wa Uhujumu Uchumi

Rais John Magufuli amewataka watuhumiwa wa kesi ya uhujumu uchumi walioagizwa kuwasilisha barua zao za kuomba msamaha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuepukana na dhana ya kuwa msamaha huo ni wa uongo kwakuwa yeye ameutoa kwa dhati na kwamba hawezi kufanya hivyo kwa lengo la kuwatega.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 30, alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa wa kusamehe watuhumiwa hao wa uhujumu uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha na mali.

“Hizi siku saba ni kwaajili ya wale ambao wamekwama inawezekana mwingine akawa amejifikiria zaidi katika siku ya leo hadi ya saba akatoa maamuzi yake ninafahamu wapo wanaodanganywa huu msamaha ni wa uongo,”

“Huwa hakuna msamaha wa uongo hauwezi ukatoa msamaha wa majaribio au wa kumtega mtu, msamaha ukishautoa ni msamaha la sivyo wewe uliyetoa utaibeba hiyo dhambi kwa Mungu.

"Ninafahamu wapo wanaodanganywa na mawakili wao ili waendelee kuwachomoa pesa wanaawambia ukiomba msamaha maana yake unakuwa umeshajishtaki mwenyewe sasa hiyo ni shauri yao waamue wanamsikiliza nani,” amesema Magufuli.


Share:

Ziara Ya Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Dkt John Joseph Pombe Magufuli Mkoa Wa Songwe
Share:

Wawekezaji Watakiwa Kuyaongezea Thamani Maziwa Kufikia Soko La Nje Ya Nchi

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ireland wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini na kuwataka kuangalia zaidi mnyororo wa thamani wa namna ya kuyaongezea thamani maziwa ili kupanua zaidi soko la maziwa kutoka Tanzania kwenda nchi za nje.

Akizungumza na wawekezaji hao leo (Jumatatu 30.09.2019) kutoka shirika la Sustainable Food Systems Ireland (SFSI) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Prof. Gabriel amesema maziwa yatakapoongezewa thamani yataiwezesha Tanzania kuingia zaidi katika masoko ya nje ya nchi yakiwemo ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)

“Waangalie pia zaidi mnyororo wa thamani namna ya kuyaongezea maziwa thamani ili tuingie zaidi katika solo la Afrika Mashariki, SADC na nje ya SADC. Lengo kubwa la wizara kwa wadau kama hawa wakija kutuona inakuwa faraja kwa kuwa inagusa maisha ya mfugaji wa kawaida, pale ambapo maziwa yatachakatwa na kuongezewa thamani soko litakuwepo tungependa wafugaji wazalishe maziwa ambayo wataweza kuuza.” Amesema Prof. Gabriel

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili soko la maziwa liendelee kuwepo kwa kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo yanapaswa kuongezewa thamani ili kukuza zaidi soko la maziwa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la SFSI ambalo lipo chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Bahari ya Jamhuri ya Ireland Bw. David Butler, amesema shirika hilo ilimekuwa likifanya kazi katika nchini mbalimbali, ambapo limekuwa likifanya vizuri katika sekta ya nyama na maziwa kwa zaidi ya miaka 40 na kuendesha programu mbalimbali za kilimo na mifugo ili kuyaongezea thamani mazao.

Bw. Butler ameambatana na Dkt. Seamus Crosse kutoka Shirika la Greenfield International la Jamhuri ya Ireland, ambapo wawekezaji hao watakutana na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kuangalia namna ya bora ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini.

Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano serikalini
   Wizara ya Mifugo na Uvuvi


Share:

Mafunzo Ya Wataalamu Wa Kilimo Kufanikisha Malengo Ya ASDP II

Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
SEKTA ya Kilimo imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika kipindi hiki tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kilimo kimeendelea kuimarika na hivyo kuchangia asilimia 30.1 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29.2 kwa mwaka 2016 pamoja na kuchangia ajira wananchi kwa asilimia 65.5 na kuchangia malighafi za viwanda kwa asilimia 65.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta zinaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara na kuboresha miundombinu wezeshi  ili kuwezesha upatikanaji wa chakula na masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yote.

Huduma za Ugani ni muhimu sana katika kufikisha na kuelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi mbinu bora za kuongeza tija katika uzalishaji, ubora wa mazao kwa usalama wa chakula na lishe pamoja na upatikanaji wa malighafi za viwanda vinavyotegemea kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha, huduma za Ugani hapa nchini zinatolewa kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo ubinafsishaji, mikataba, sekta ya umma na binafsi, ugatuaji wa huduma za ugani na utandawazi wa soko huria. Baada ya ugatuaji wa madaraka (1997) majukumu ya kutekeleza huduma za ugani yalihamishiwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Baada ya ugatuaji wa huduma za ugani kumekuwako na changamoto mbalimbali za kiutendaji ikiwemo Ufuatiliaji na uratibu wa huduma za ugani katika Halmashauri umekuwa na mapungufu kwani hakuna uwajibikaji wa moja kwa moja wa wataalam wa Kilimo walioko Halmashauri na Wizara ya Kilimo pamoja na Halmashauri kutoajiri wataalamu wa kutosha wa ugani, kutotoa motisha kwa kuwaendeleza  watumishi wake hivyo kuathiri utoaji wa huduma za ugani.

Ili kufikia malengo iliyoyaweka katika Sekta ya Kilimo nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (2017/2028), ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo ambapo utekelezaji wake utazingatia kuimarisha utafiti, huduma za ugani na mafunzo; upatikanaji wa masoko ya mazao na miundombinu ya uzalishaji.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadiro ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema Serikali imeendelea kuboresha vyuo na vituo vya mafunzo ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya wataalam wa ugani kilimo katika ngazi ya kijiji na kata.

Anasema kuwa Katika mwaka 2018/ 2019, Wizara kupitia vyuo vyake 14 vya kilimo imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389 ambapo wanafunzi 2,051 wamefadhiliwa na Serikali ambapo wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada na 852 ni ngazi ya Stashahada na jumla ya wanafunzi wanafunzi 1,026 wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada wamehitimu masomo yao mwezi Juni, 2019.

“Vyuo hivyo vinatoa Astashahada na Stashahada za Kilimo Mseto, Stashahada ya Umwagiliaji, Matumizi Bora ya Ardhi, Uzalishaji Chakula na Lishe, Matumizi ya Zana za Kilimo, Uzalishaji wa Mazao, Mboga, Maua na Matunda” anasema Waziri Hasunga.

Waziri Hasunga anasema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Lutheran World Relief (LWR) kupitia mradi wa Invest imehuisha mtaala wa Kilimo Mseto na kuzalisha mtaala mpya wa kilimo (Agriculture Production) ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kutimiza masharti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Akifafanua zaidi Hasunga anasema mradi wa Invest umejenga kitalu nyumba katika Chuo cha Taifa cha Sukari Kidatu ili kutoa mafunzo bora kwa wagani tarajali na wakulima na kuwajengea uwezo wakufunzi 20 kutoka vyuo vya Kilimo Ilonga (Kilosa), KATRIN (Ifakara) na Chuo cha Taifa cha Sukari Kidatu ili wafundishe kwa kufuata mwongozo wa mfumo wa moduli.

Anaongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ysa Kilimo imeendelea kuwajengea uwezo wakufunzi wa kilimo 22 ambapo wakufunzi 10 wapo katika mafunzo ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na 12 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini India na China pamoja na kushirikiana na Taasisi Binafsi kuandaa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi ya kuwajengea uwezo wakulima kuhusu teknolojia mbalimbali za kilimo.

Kwa mujibu wa Hasunga anasema Mafunzo hayo yalihusu Kilimo cha Korosho, Mtwara (wakulima 67), Kilimo cha Mahindi na Maharage, Ukiriguru (wakulima 51), Usindikaji wa mazao- Uyole (wakulima vijana 56), na Kilimo bora cha soya (wakulima 31), Kilimo shadidi cha mpunga (wagani 33), kilimo bora cha alizeti (wakulima 25 na wagani 5), na kilimo bora cha mpunga (wakulima 20), Ilonga.

Hasunga anasema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), kupitia mradi wa TANRICE2 imetoa mafunzo kwa wakulima wa mpunga 1,964. Kati ya hao, wakulima 923 wametoka katika skimu za umwagiliaji za Kimbande Nyasa (Ruvuma), Magoma (Korogwe) Wamiluhindo (Mvomero), Tulokongwa (Morogoro), SololaNkanga (Sumbawanga) na Legezamwendo (Tunduru), Litumbadyosi (Mbinga), Njomulole (Namtumbo), Msanjesi (Namtumbo) na Kyamyorwa (Muleba).

ASDP II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya Taifa, ili kukabiliana na mapungufu na changamoto za sekta ya kilimo na kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la Taifa, kuboresha ukuaji wa pato la wakulima wadogo na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ifikapo 2025.

Ni wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Wilaya kujenga uwezo katika  huduma za umma ili kuviwezesha vyama vya wakulima wadogo kulima kibiashara kusaidia kuwaunganisha wafanya biashara wa sekta ya kilimo na mfumo wa uzalishaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa ajili ya soko na kuendeleza mnyororo wa thamani.

MWISHO


Share:

Rais Magufuli aongeza siku saba watuhumiwa uhujumu uchumi kutubu

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga amesema ofisi yake imepokea barua za watuhumiwa 467 wanaoomba kukiri makosa ya uhujumu uchumi na wapo tayari kurudisha fedha jumla ya Shilingi 107.8 Bilioni.

Akiwasilisha taarifa yake leo Jumatatu Septemba 30, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, Mganga amesema watuhumiwa wameitikia wito alioutoa Rais John Magufuli

DPP amemuomba Rais Magufuli kuongeza siku tatu kwaajili ya kuwapa nafasi watuhumiwa wa uhujumu uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha na mali ambao barua zao zimechelewa kufika ofisini kwake.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli ametoa siku saba kuanzia leo Jumatatu Septemba 30, 2019 hadi Oktoba 6, 2019.

“Kama kweli wapo walikwamishwa na DPP umeniomba siku tatu mimi naona nikupe siku saba ili usije ukaniomba tena siku nyingine, nilitoa siku sita kwamba watuhumiwa wote wanaotaka kupata huu masamaha kwa kupitia taratibu za kisheria na wameitikia zaidi ya watu 467 na fedha Sh.  bilioni 107.842 zitaokolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao lakini nitoe tahadhari baada ya siku hizi saba kuisha wale wote watakaoshikwa kwenye makosa haya ya uhujumu uchumi sheria ichukue mkondo wake

“Nimetoa hizi siku saba na sitatoa nyingine lakini niwapongeze hawa 467 na mimi ningeomba ofisi ya DPP muharakishe ili watu waanze kutoka wakajumuike na familia zao kwasababu waliingia kwa njia ya mahaka watatoka kwa njia ya mahakama kwahiyo muwafikishe kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuachiwa isije tena mtakapochambua mkakuta wamebaki 300,” amesema Magufuli.

Aidha amesema msamaha huo hautawahusu watuhumiwa wenye kesi mpya na kwamba wachukuliwe sheria kwakua msamaha huo ni kwa wale waliokwama tu.

“Watakaoshikwa na kesi za uhujumu uchumi leo, kesho na kuendelea wao waendelee na kesi zao za uhujumu uchumu maana huu msamaha hauwahusu hata kidogo kwani kuna wale ambao wana kesi mpya wao wapelekwe tu kwenye kesi,” amesema.


Share:

Live: Rais Magufuli Anapokea Taarifa Ya Wahujumu Uchumi Waliotubu

Live: Rais Magufuli Anapokea Taarifa Ya Wahujumu Uchumi Waliotubu


Share:

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Amkalia Kooni Mkandarasi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Chunya -Makongolosi kwa kiwango cha lami kuhakikisha anamaliza mradi huo ndani ya muda wa mkataba na si vinginevyo.

Aidha, ameongeza kuwa hatamuongezea mkandarasi huyo muda wa kumaliza kwani muda aliopewa ulikuwa unamtosha kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Hayo ameyasema mkoani Mbeya alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amemuelekeza mkandarasi huyo kuongeza vitendea kazi na wataalamu ili kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliobakia.

“Natarajia utaongeza vifaa na wataalamu ili kuhakikisha kazi hii inakamilika kwa wakati, pia ukumbuke kuwa sitakupa muda wa nyongeza hivyo fanya juhudi ili umalize mradi huu ndani ya muda”, amesisitiza Arch. Mwakalinga.

Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 unajengwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 59 ambazo zote ni fedha za Serikali na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2020.

Arch. Mwakalinga amemuelekeza pia mkandarasi kutumia muda wake wote kuwa katika eneo la mradi hata ikiwezekana kuongeza masaa ya kufanya kazi usiku na mchana.

“Fanyeni kazi usiku na mchana ili kuepukana na changamoto za vipindi vya mvua na hakikisheni barabara hii inajengwa kwa viwango vya ubora zaidi”, amesema Arch. Mwakalinga.

Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mbeya Eng. Mwita Magesa, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 53 ukilinganisha na muda wa mkataba uliotumika ambao ni miezi 23 sawa na asilimia 85.19 ya muda wa mkataba.

Eng. Mwita ameeleza kuwa mkandarasi mpaka sasa ameshakamilisha kujenga tabaka la juu la barabara kwa mawe yaliyosagwa KM 9.18, lami ya prime KM 6.78 na kazi zingine za ujenzi wa makalvati madogo na madaraja makubwa matatu zikiendelea.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Chunya-Makongolosi yenye urefu wa KM 39 ni sehemu ya barabara ya Mbeya-Rungwa yenye urefu wa KM 293 inayounganisha mkoa wa Mbeya na mikoa jirani ya Singida na Tabora ambapo barabara hii ikikamilika itaongeza zaidi fursa za kimaendeleo kwa wananchi kiuchumi na usafirishaji.


Share:

Waziri Simbachawene Ahimiza Matumizi Ya Nishati Mbadala Kupikia Ili Kuhifadhi Mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amehimiza matumizi ya nishati mbadala kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati akihutubia wanafunzi na wananchi katika mahafali ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pwaga wilayani Mpwapwa.

Aliwataka wananchi kuacha mara moja kukata miti kwa ajili ya kuni au mkaa na kusema kuwa vitendo hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi.

Mhe. Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe alisema kuwa wakati umefika sasa kwa wananchi kuanza kutumia gesi katika shughuli za kupika hivyo kuepuka matumizi ya mkaa au kuni ambayo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na ukaaji wa miti.

“Tukiyachezea mazingira tunachezea uhai wetu na ukataji hovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa unaishia kusababisha kumalizika kwa maeneo yenye miti mikubwa na wengine wanakata miti kwa kiwango kikubwa hata tukae miaka mingi hatutakuja kupata tena miti kama hiyo,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe wilayani humo aliwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao na kuwatia moyo.

Pia alikemea tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike kuanza kushiriki katika vitendo vya ngono kabla ya umri na kuwataka kuzingatia masomo na hivyo kufikia malengo yao na kuwaonya wazazi wanaoficha wahusika wa mimba hizo.

Alionya tabia ya baadhi ya wanaume wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kushiriki nao ngono vitendo vinavyosababisha kuwapa mimba na hivyo kukatisha masomo yao.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Nelson Milanzi alitoa mwito kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla kutunza mazingira.

Afisa Elimu huyo aliwataka kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla kutunza mazingira na kupanda miti kwa wingi.


Share:

NAIBU WAZIRI MGUMBA AWATAKA WALIMU NCHINI WAACHE KUTUMIA KILIMO KAMA ADHABU YA KUWAPA WANAFUNZI

NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba akizungumza na watumishi wa Halamashauri ya wilaya ya Pangani wakati wa ziara yake kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah
Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji kulia akimueleza jambo Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba wakati wa ziara yake wialayani humo
MKUU wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani Mwalimu Hassani Nyange 
 NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba kushoto akisalimiana na Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Pangani Seif
 NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba kushoto akisialimiana na Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani Mwalim Hassani Nyange wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo
 NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba kushoto akisalimiana na Afisa Tawala wa wilaya ya Pangani Gibson George wakati wa ziara yake kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah
NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba kushoto akisalimiana na Mkuu wa Polisi wilaya ya Pangani (OCD) Georgina Matagi 
NAIBU Waziri wa Kilimo Omari Mgumba amewataka walimu wa shule za Msingi na Sekondari waache kutumia kilimo kama adhabu ya kuwapa wanafunzi wakati wanapokosea kwani inawajengea tafsiri mbaya kwa jamii na baadae wanapokuwa wanachukia kilimo.
Mgumba alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake wilayani Pangani ambapo alisema kwamba kuna tabia ambayo imejengeka kwa walimu hao kwamba mtoto anapokosea anaambiwa leo utakwenda kilima siku nzima, utakwenda kumwagilia hali ambayo inapelekea baadae wakikua wanakuwa hawahitaji kilimo kwa sababu awali waliona kama adhabu.

Alisema kwamba hapana suala hilo sio jema na ndio maana wao wanasema kilimo ni ute wa mgongo lakini watafungamanisha kilimo na elimu ili watoto tokea anakuwa ajue kwamba nchi hii uchumi wake unategemea kilimo.

“Hivyo ninapoambiwa niwe na tuta la mchicha sio adhabu bali ni sehemu ya kuniandaa kielimu nije kujitegemea au nije kuajiri wengine kwenye mashamba yao kwani bila kufanya hivyo tutakuwa tunaimba kitu kingine wakati uchumi wetu unategemea kilimo”Alisema Naibu Waziri huyo.

Naibu Waziri huyo alisema kwamba mkakati wa serikali ni kuimarisha kilimo hivyo wataendelea kufungamanisha elimu yao na kilimo chao.

Akizungumzia Kilimo cha Minazi wilayani humo Naibu Waziri huyo alisema kwamba kilimo cha minazi ni kweli mpaka sasa hawaapata ufumbuzi wa magonjwa yake kwa miaka zaidi ya 30 mpaka leo ambayo yanasababsihwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Alisema pia hilo linatokana na kukubali kuletewe mbegu ya kisasa ambayo haiendani na mazingira ya nchi hivyo kama Taifa  wameendelea kuimarisha vituo vyao vya utafiti hasa cha utafiti wa minazi mikocheni lengo ni kuanza kurudi kwenye kuzalisha miche kutumia minazi ya asili inayokabiliana na hali ya hewa na ikolojia ya ya nchi yetu .

“Na sasa tumeanza kuzalisha kitalu cha miche asili Bagamoyo na itasambazwa nchi nzima kwa lengo la kupanda na hatimaye kuweza kurejesha minazi hiyo”Alisema

Akizungumzia udogo wa bei ya nazi nchini Naibu Waziri huyo alisema kwamba nazi zinauzwa bei ndogo na imeendelea kuwa ndogo ni kutokana na ushindani uliopo kwenye soko la ndani, kanda na kimataifa kwa sababu ya bidhaa mbadala.

 “Hivyo kila nazi ikipanda bei watu wanakwenda kutumia mafuta lakini kila tunapoacha kutumia nazi na kutumia mafuta na kwenda kwenye chukuchuku wanapunguza mahitaji ya nazi”Alisema.

Hata hivyo alisema kwamba wanakuja na mkakati wa kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza thamani bidhaa hiyo ili kupanua soko la nazi hapa nchini na mbegu za nazi ambazo zinaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi huku akieleza kwamba wakienda kuongeza thamai tatizo hilo litakwisha.

Katika hatua nyengine Naibu Waziri huyo aliwataka watanzania tuendelee kutumia nazi kwani wanapoendelea kuitumia zaidi wanatongeza mahitaji na soko la nazi litakuwa kubwa huku akisistiza kwamba watakaendelea kutumia mafuta bei ya nazi itashuka.

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso alisema kwambazao la nazi limeathiriwa namaradhi kwa muda mrefu mpaka yamepatikana bado tiba yake haijapatikana miaka 30.

Alimwambia Naibu Waziri Mgumba kwamba ugonjwa huo umekuwa haupati ufumbuzi kama lilivyokuwa gonjwa la ukimwi hiyo walimuomba watafiti na watalamu wafanye utafiti ambao utafika mwisho na wenye manufaa na kuweza kurudisha uchumi wake.

“Kwa sababu nazi zinakazi nyingi unaweza kusingwa na machicha yake ukabaki hapa Pangani….lakini pia inaleta heshima kwenye ndoa na hivyo kuweza kurejesha furaha”Alisema.

Mwisho
Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya Septemba 30
Share:

Sunday, 29 September 2019

Makonda Awaomba Mawaziri Wamvumilie....Awataka Wasitishe Ziara Zao Dar es Salaam Kwa Muda

Mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewaomba Mawaziri wanaotaka kufanya ziara za miradi katika mkoa huo, kusitisha kwa muda ili kupisha utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa.
Amesema mwezi huu na Octoba watamalizia pia utekelezaji wa mikakati waliyopeana na kuanzia hapo mawaziri wataweza kufika na kuendelea na ziara zao za kikazi.

Makonda ameyasema hayo ni leo wakati akikagua mradi wa ujenzi machinjio  ya kisasa ya Vingunguti ambao ujenzi wake umefika asilimia 25.

"Nawaomba mawaziri ambao wanataka kufanya ziara katika mkoa huu, tutekeleze miradi ambayo tumepewa maelekezo na Rais Magufuli alipofanya ziara na baada ya hapo waendelee kama walivyopanga," Makonda alisema.

Kuhusu ujenzi wa machinjio hayo alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutekeleza mradi huo kwa haraka.

Makonda alimuagiza Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto, kukaa na baraza la madiwani kwa ajili ya kutenga fedha za kujenga barabara ya kuelekea katika machinjia hayo yenye urefu wa Kilometa moja.

"Baraza la madiwani likae litenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya kuingia katika machinjio haya ya kisasa ili wafanyabishara wanaokuja wasikwame kwa sababu ya ubovu wa barabara," Makonda alisema.

Alisema pia kuwapo kwa machinjio hayo ni fursa kwa Manispa kujenga reli ya kuingia eneo hilo ili mizigo isafirishwe kwa treni.

Aidha, aliwataka kuangalia namna ya kuwalipa fidia wakazi wa maeneo hayo ili kuandaa eneo kwa ajili ya kupanua machinjio hayo kwa miaka ijayo.

Makonda alisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu na kuukabidhi kwa ajili ya kuanza shughuli za kuchinja ng'ombe.

Naye Mhandisi Elisante Ulomi, alisema wanamalizia kazi ya kushindilia kifusi kwa ajili ya kuanza kusuka nondo na kumwaga zege.

Alisema mwishoni mwa mwezi Novemba wataanza kupaua, wakati kazi za kufunga umeme na kumalizia kazi za ndani zikiendelea.

Naye Meya wa Ilala, Omary Kumbilamoto, alisema wanatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Makonda na kwamba lengo ni kuhakikisha mradi huo unakamilika Disemba na unakuwa kivutio.

Mbali na mradi huo, Makonda alitembelea mradi wa ujenzi wa soko la Kisutu na kuagiza mradi huo kukamilika mwezi Mei mwakani.


Share:

BONANZA LA MIAKA MITATU YA MISENYI JOGGING CLUB LAFANA..DC MWILA ATAKA WANANCHI WAFANYE MAZOEZI


Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Kanali Denice Mwila amewataka wananchi wilayani humo kuepuka kutumia gharama nyingi katika matibabu badala yake wajikinge na maradhi kwa kufanya mazoezi.

Kanali Mwila ametoa wito huo Septemba 28,2019 wakati wa Bonanza la kwanza la kuadhimisha miaka 3 ya Misenyi Jogging Club lililofanyika katika uwanja wa mashujaa Bunazi wilayani humo likiwa na lengo la kuwahamasisha wananchi kuipenda michezo ili kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi.

Kanali Denice Mwila amesema kuwa kupitia Bonanza hilo wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kupima afya zao na kufanya mazoezi kwani michezo ni afya.

"Naomba tushirikiane kuhamasisha jamii kuwa na mwamuko wa kufanya mazoezi ili kufukuza magonjwa nyemelezi",amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Tamasha la Misenyi Jogging Respicius John amewapongeza wadau wote walioshiriki kikamilifu vikiwemo vyombo vya habari mkoani Kagera vilivyotangaza tamasha hilo bure kuanzia mwanzo mpaka linamalizika kuwaomba wananchi wilayani Misenyi kujitokeza kwa wingi katika kufanya mazoezi.

Respicius amesema malengo ya baadae ni kuhakikisha jamii inakuwa na nguvu kubwa katika mazoezi na kuwataka wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki mazoezi ili kukuza na kuimalisha miili yao.

Bonanza hilo limeenda sanjari na utoaji wa huduma za upimaji afya ikiwemo upimaji wa VVU na kuchangia damu pamoja na michezo mbali mbali ikiwemo kuvuta kamba, kukimbia kwenye magunia kucheza Draft, pete, mpira, kumenya ndizi kwa wanaume mchezo ambao ulienda kiushindani kati ya timu zilizopewa majina ya Simba na Yanga.
Wanafunzi wa shule ya msingi Bunazi wilayani Misenyi wakionesha vipaji vyao wakati wa Bonanza la kwanza la kuadhimisha miaka 3 ya Misenyi Jogging Club lililofanyika katika uwanja wa mashujaa Bunazi wilayani humo.

 Mwanafunzi wa shule ya msingi Bunazi wilayani Misenyi akionesha kipaji chake.

Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Denice Mwila akiwa katika michezo pete

Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Denice Mwila akihamasisha wananchi kuipenda michezo.
Mratibu wa bonanza hilo Respicius John akizungumza wakati wa  bonanza.
Mchezo wa  kuvuta kamba ukiendelea

Mchezo  wa kushindana kumenya ndizi ukiendelea.
Mbio za magunia zikiendelea.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

TANGAZO LA TOUR MBUGA YA SAADAN

TANGAZO LA TOUR MBUGA YA SAADAN

FUNGUA PAZIA

NDOA ZA UTOTONI

Narudi nyumbani

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger