Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Ireland wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini na kuwataka kuangalia zaidi mnyororo wa thamani wa namna ya kuyaongezea thamani maziwa ili kupanua zaidi soko la maziwa kutoka Tanzania kwenda nchi za nje.
Akizungumza na wawekezaji hao leo (Jumatatu 30.09.2019) kutoka shirika la Sustainable Food Systems Ireland (SFSI) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Prof. Gabriel amesema maziwa yatakapoongezewa thamani yataiwezesha Tanzania kuingia zaidi katika masoko ya nje ya nchi yakiwemo ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ushirikiano na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
“Waangalie pia zaidi mnyororo wa thamani namna ya kuyaongezea maziwa thamani ili tuingie zaidi katika solo la Afrika Mashariki, SADC na nje ya SADC. Lengo kubwa la wizara kwa wadau kama hawa wakija kutuona inakuwa faraja kwa kuwa inagusa maisha ya mfugaji wa kawaida, pale ambapo maziwa yatachakatwa na kuongezewa thamani soko litakuwepo tungependa wafugaji wazalishe maziwa ambayo wataweza kuuza.” Amesema Prof. Gabriel
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili soko la maziwa liendelee kuwepo kwa kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo yanapaswa kuongezewa thamani ili kukuza zaidi soko la maziwa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la SFSI ambalo lipo chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Bahari ya Jamhuri ya Ireland Bw. David Butler, amesema shirika hilo ilimekuwa likifanya kazi katika nchini mbalimbali, ambapo limekuwa likifanya vizuri katika sekta ya nyama na maziwa kwa zaidi ya miaka 40 na kuendesha programu mbalimbali za kilimo na mifugo ili kuyaongezea thamani mazao.
Bw. Butler ameambatana na Dkt. Seamus Crosse kutoka Shirika la Greenfield International la Jamhuri ya Ireland, ambapo wawekezaji hao watakutana na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ili kuangalia namna ya bora ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano serikalini
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
0 comments:
Post a Comment