Saturday 28 September 2019

Tutahakikisha Malighafi Zinazohitajika Viwandani Zinapatikana

...
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Songwe
Serikali imesema kuwa inaimarisha mikakati yake ili kuwa na uwezekano wa kuwa na malighafi toshelevu katika viwanda vyote nchini.

Ifahamike kuwa malighafi nyingi zinazotumika viwandani asilimia kubwa zinatokana na sekta ya kilimo hivyo moja ya mkakati madhubuti ni kusimamia kwa weledi sekta hiyo ili kuwa na malighafi nyingi na za kutosha.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo  jana tarehe 27 Septemba 2019 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Vwawa Mkoani Songwe.

Alisema kuwa miongoni mwa majukumu muhimu ya Wizara ya kilimo ni kuimarisha Mchango wa sekta ya kilimo ili wakulima waweze kuongeza uzalishaji na tija.

"Ni lazima tuhakikishe kuwa watu wanazalisha kwa ajili ya biashara sio chakula pekee na gharama wanazotumia ni lazima wahakikishe zinarudi ili waone faida ya kilimo" Alikaririwa Mhe Hasunga

Waziri Hasunga ameeleza kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo ina jukumu la kuhakikisha umasikini unapungua kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima ili kilimo kiendelee kuingiza fedha nyingi za kigeni na kuchangia kwa wingi pato la Taifa.

Kadhalika ametaja Mikakati mingine ya wizara ya kilimo kuwa ni pamoja na  Pembejeo (Mbegu bora, Mbolea, na Viuatilifu) kufika kwa wakati kwa wakulima ambapo amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kununua mbegu Bora kwani  zinaweza kukinzana na magonjwa na nyingi zinastahimili ukame.

Kuhusu masoko ya mazao ya wakulima waziri Hasunga amesema kuwa wizara yake imekuja na mkakati maalumu wa kuanzisha kitengo cha masoko kitakachokuwa na majukumu ya kubainisha masoko ya mazao mbalimbali ya wakulima.

"Ni lazima kufanya biashara kisasa kwa kujua mahitaji ya soko kabla ya kuzalisha mazao ya kilimo ili wakulima wanapozalisha tayari wawe wanajua watauza wapi mazao yao" Alisisitiza Mhe Hasunga

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi ambao ni wakazi wa mamlaka ya mji mdogo wa Vwawa na ameneo ya jirani, Waziri Hasunga amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kuimarisha ufanisi wa shughuli za maendeleo katika Jimbo la Vwawa na Taifa kwa ujumla.

MWISHO.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger