Monday 30 September 2019

Waziri Simbachawene Ahimiza Matumizi Ya Nishati Mbadala Kupikia Ili Kuhifadhi Mazingira

...
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amehimiza matumizi ya nishati mbadala kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo wakati akihutubia wanafunzi na wananchi katika mahafali ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pwaga wilayani Mpwapwa.

Aliwataka wananchi kuacha mara moja kukata miti kwa ajili ya kuni au mkaa na kusema kuwa vitendo hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi.

Mhe. Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe alisema kuwa wakati umefika sasa kwa wananchi kuanza kutumia gesi katika shughuli za kupika hivyo kuepuka matumizi ya mkaa au kuni ambayo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na ukaaji wa miti.

“Tukiyachezea mazingira tunachezea uhai wetu na ukataji hovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa unaishia kusababisha kumalizika kwa maeneo yenye miti mikubwa na wengine wanakata miti kwa kiwango kikubwa hata tukae miaka mingi hatutakuja kupata tena miti kama hiyo,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe wilayani humo aliwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao na kuwatia moyo.

Pia alikemea tabia ya baadhi ya wanafunzi wa kike kuanza kushiriki katika vitendo vya ngono kabla ya umri na kuwataka kuzingatia masomo na hivyo kufikia malengo yao na kuwaonya wazazi wanaoficha wahusika wa mimba hizo.

Alionya tabia ya baadhi ya wanaume wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kushiriki nao ngono vitendo vinavyosababisha kuwapa mimba na hivyo kukatisha masomo yao.

Kwa upande wake Afisa Elimu wa Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Nelson Milanzi alitoa mwito kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla kutunza mazingira.

Afisa Elimu huyo aliwataka kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla kutunza mazingira na kupanda miti kwa wingi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger