Sunday, 1 November 2026

SERIKALI KUZINDUA SERA MPYA YA VIWANDA NA JASIRIAMALI NDOGO NA ZA KATI JIJINI DODOMA - MHE. KAPINGA



📌 Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa sera hizo;

📌 Waziri Kapinga afanya mkutano na waandishi wa habari kueleza hatua ya maandalizi iliyofikiwa;

📌Asema Serikali  inalenga kuongeza mchango wa sekta ya viwanda hadi kufikia asilimia 15  kwenye pato la Taifa;

📌 Asema Sera ya maendeleo endelevu ya viwanda na Sera ya maendeleo ya jasirimali dogo na kati kuinua biashara bunifu la makundi yote.

DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inatarajia kuzindua sera mbili mpya zinazolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya viwanda na jasiriamali ndogo na za kati nchini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza uzalishaji, ajira, uongezaji thamani wa malighafi za ndani na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 31, 2026, katika Ukumbi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), jijini Dar es Salaam, Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Sera hizo ni Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya jasiriamali ndogo na za Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025). 

Amesema Sera hizo zimefanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kuweka mazingira wezeshi ya biashara, uwekezaji na uzalishaji nchini na kuongeza kuwa zitaimarisha pia  mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

Mhe Kapinga aliongeza kuwa Serikali inalenga kuongeza mchango wa sekta hiyo hadi kufikia asilimia 15 ya Pato la Taifa, sambamba na kuongeza uzalishaji, uongezaji thamani wa malighafi za ndani na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Waziri Kapinga amesema Wizara imejipanga vizuri kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha kila sekta inajipanga na kujiratibu upya ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea kuimarisha na kuitangaza nembo ya Made in Tanzania kwa lengo la kuongeza utambuzi na kuaminika kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, kukuza matumizi ya bidhaa za ndani na kupanua fursa za masoko kwa wazalishaji wa Kitanzania. 

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhamasisha wananchi kuthamini bidhaa za ndani na kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wa maendeleo ya wajasiriamali wadogo na wa kati, Waziri Kapinga amesema Sera husika inalenga kuboresha miundombinu wezeshi, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kukuza matumizi ya teknolojia na ubunifu pamoja na kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na wajasiriamali hao ma hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao, kuongeza tija na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa upande wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda, amesema inalenga kuongeza thamani ya mazao na rasilimali zinazozalishwa nchini kupitia uimarishaji wa mnyororo wa thamani, kuendeleza viwanda vya kimkakati, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kuimarisha uwezo wa viwanda vya ndani kushindana katika masoko. 

Aidha, sera hiyo inalenga kuchochea uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Kuelekea uzinduzi huo, Wizara ya Viwanda na Biashara imeandaa maonesho na kliniki za biashara Novemba 2 na kongamano la wadau wa sekta ya Viwanda na Biashara wanatarajia kukutana Novemba 3, 2026, kwa lengo la kuwapa wadau wa sekta ya viwanda na biashara fursa ya kujifunza kuhusu sera hizo, kujadili masuala ya utekelezaji na kuelewa mchango wao katika kuimarisha maendeleo ya viwanda na ujasiriamali nchini.

Uzinduzi rasmi wa Sera hizo utafanyika Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.
Share:

DC BAGAMOYO AWATAKA WADAU KUONGEZA USHIRIKIANO KUFANIKISHA TAMASHA LA SANAA NA UTAMADUNI


NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo amewataka wadau mbalimbali kuongeza ushirikiano katika kufanikisha Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ili liendelee kudumu na kukuza sekta ya sanaa nchini.

Akizungumza katika kilele cha Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni lililofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Mkuu huyo wa Wilaya amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za maandalizi na uendeshaji wa matamasha makubwa.

Amesema TaSUBa imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kufanyika kwa miaka 44 mfululizo, hatua inayopaswa kupongezwa kutokana na mchango wake katika kuhifadhi, kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Tanzania.

Ametoa pongezi kwa Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo, uongozi, wafanyakazi, wanachuo na kamati zote za tamasha kwa juhudi wanazozifanya kila mwaka kuhakikisha tukio hilo linaendelea kufanyika.

Aidha, amewataka waandaaji wa tamasha hilo na matamasha mengine nchini kuendelea kufungua milango kwa wadau wengi zaidi ili washirikiane katika kugharamia na kuendesha matukio hayo muhimu kwa Taifa.

Katika hatua nyingine, amewapongeza wasanii wote walioshiriki tamasha hilo, akieleza kuwa baadhi yao walijigharamia wenyewe ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya tukio hilo.

Amesema kujitolea kwa wasanii hao ni ishara ya uthubutu na mshikamano katika kudumisha na kuendeleza sanaa na utamaduni wa Taifa.

Vilevile, aliwahamasisha wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kuhudhuria na kushiriki matamasha yajayo ili kuwapa moyo wasanii na kuthamini kazi zao.

Amewashukuru wadhamini na taasisi mbalimbali zilizojitokeza kusaidia kufanikisha tamasha hilo kwa namna tofauti.

Wadhamini hao ni Azam Media Limited, ITV na Radio One, EGA, Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi Tanzania (TPFCS), SUMA JKT, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Malkia Events Management and Tents Limited na Coca-Cola.

Wengine ni Bagamoyo Friendship Society, Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), BRELA, TwiBhok Bagamoyo, Shule ya Sekondari Baobab, Bonge Hardware, Klimario Hardware, Salehe Mguu Hardware, Stella Maris Hotel, TANLAPIA, Ofisi ya Ardhi Bagamoyo, DAWASA Bagamoyo na Travellers Lodge, pamoja na vikundi mbalimbali vilivyojigharamia kushiriki tamasha hilo.
Share:

TANROADS MBEYA YATEKELEZA MAAGIZO YA MAKAMU WA RAIS, NJIA 106 ZAFUNGULIWA


Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya umeanza kutekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kufungua maeneo na njia 106 za pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi, hatua inayolenga kupunguza adha kwa wananchi na wafanyabiashara wakati ujenzi ukiendelea.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais jijini Mbeya Oktoba 16 na 17, 2026, ambapo alitoa maelekezo kwa TANROADS kuhakikisha njia zinazotumiwa na wananchi zinafunguliwa ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kupunguza usumbufu unaotokana na utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha wananchi wanaendelea kutumia njia hizo wakati kazi za ujenzi zikiendelea.

Amesema pamoja na kufunguliwa kwa njia hizo, mkandarasi ameagizwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa na tayari kilomita 3 zilizopo Mbeya mjini TANROADS imeshaanza zoezi la kumwaga lami.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 29 kuanzia Nsalaga (Uyole) hadi Ifisi, eneo la Kiwanja cha Ndege cha Songwe, ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 138.

Utekelezaji wa maelekezo hayo unalenga kuhakikisha wananchi, wafanyabiashara na watumiaji wengine wa barabara wanaendelea na shughuli zao za kila siku huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

TANROADS Mkoa wa Mbeya inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia ubora wa kazi, usalama wa watumiaji wa barabara na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza wakati wa ujenzi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Wananchi waliozungumza wameeleza kufurahishwa na hatua ya TANROADS kufungua njia 106 za pembezoni mwa mradi huo, wakisema hatua hiyo imeanza kupunguza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo wakati wa shughuli za ujenzi.

Gladis Mjabili, mkazi wa Ileje, pamoja na Selina Leonard na Leonard Charles ambaye ni dereva bodaboda, wakazi wa Mbeya, wamesema upatikanaji wa njia hizo ni muhimu katika kurahisisha shughuli za kila siku na kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara.

Kwa upande wake, Salim Ngaola, dereva wa lori anayesafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Congo, amesema hali ya barabara na upatikanaji wa njia za kupita ni mambo muhimu kwa madereva wanaosafirisha mizigo masafa marefu.

Naye Leobinus Leonard, dereva wa bajaji jijini Mbeya, amesema hatua hiyo itarahisisha shughuli za usafiri wa ndani na kuwasaidia madereva kuendelea kutoa huduma kwa wananchi bila usumbufu mkubwa.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger