Sunday, 23 February 2020

ONGEZEKO LA SANGARA ZIWA VICTORIA LAISHTUA CCM,YATOA MAAGIZO MAZITO

 Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akibeba samaki aina ya sangara mwenye urefu wa  sentimita 90 akiwa na uzito wa kilo 15 baada ya kutembelea Mwalo wa Nyamikoma Busega Simiyu na kushangazwa na mafanikio ya Serikali ya kudhibiti uvuvi haramu
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akikagua zana haramu zilizokamatwa katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM Mkoa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye Sekta ya Uvuvi. Kulia ni Afisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Simiyu na Magu, Samson Mboje.
 Na Mwandishi Wetu, Simiyu


CHAMA cha Mapinduzi kimeshtushwa na ongezeko kubwa la samaki aina ya Sangara ikiwa ni miaka mitatu tu tangu Serikali ya awamu ya tano kuanza operesheni za kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na kutaka Serikali kuchukua hatua za haraka kutafuta masoko ya uhakika ya samaki ndani na nje ya nchi.


Wakizungumza kwenye ziara ya Wajumbe wa Sektetarieti ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Simiyu baadhi ya Wavuvi katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega wamesema awali kabla ya operesheni kuanza walikuwa wakisafirisha wastani wa tani 6 za samaki kwa mwezi lakini tangu Serikali ilipoamua kuchukua hatua za kudhibiti uvuvi haramu samaki wameongezeka na sasa wanasafirisha wastani wa tani 60 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi ‘BMU’ Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu , George James alisema ongezeko hilo kubwa la samaki pia limepunguza bei ya Sangara kutoka wastani wa shilingi 9,000  kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo.


Mbali na mafanikio hayo pia wavuvi hao wameiomba Serikali kuwasaidia kupata mtambo wa kutengeneza barafu katika eneo hilo kwani kwa sasa wanalazimika kusafiri hadi jijini Mwanza umbali wa zaidi ya kilomita 150 kufuata barafu.


Hivyo walimuomba Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu kumfikishia shukrani Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli  kwa uongozi wake imara hasa katika usimamizi wake wa rasilimali za uvuvi na kwamba sasa samaki ni wengi na kwamba ombi lao kubwa ni kusaidiwa kupata soko baada ya ongezeko hilo la samaki.

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega, Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba  aliitaka Serikali kupitia Dawati la Sekta Binafsi lililoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufika katika mwalo huo wa Nyamikoma ili kuwaunganisha wavuvi hao na taasisi za kifedha kuweza kupata mtambo wa kutengeza barafu.


Pia ameitaka Serikali kutanua wigo wa kuwatafutia masoko ya samaki wavuvi hao ili kunufaika na fursa kubwa ya ongezeko hilo la samaki aina ya Sangara kwa kupeleka katika masoko ya mikoa ya mbali na Ziwa Victoria pamoja na nchi za jirani za Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi na Msumbiji.


Kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu, Katibu huyo alisema Ilani ya CCM imeitaka Serikali kudhibiti uvuvi ili kupata uvuvi endelevu na kuongeza kipato cha mwanchi mmoja mmoja na kuiletea fedha za kigeni Serikali kutokana na mauzo ya samaki nje ya nchi na kupongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kusimamia rasilimali hizo za uvuvi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuamua na kusimamia operesheni Sangara ambayo ilisimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi operesheni hii imezaa matunda kama mlivyotoa ushuhuda kwamba operesheni hii mliipinga sana lakini sasa mnaona matokeo yake”alisema.


Aliongeza kuwa CCM inaamini katika kusimamia sheria na kwamba hatua zote zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu zililenga kunufaisha watanzania wengi tofauti na hapo awali ambapo watu wachache ndio waliokuwa wakinufaika kupitia uvuvi haramu.


“Niipongeze sana Serikali yetu kwa kukubali kutukanwa, kuzuliwa maneno mengi kupata kashfa nyingi lakini bado waliendelea kusimamia msimamo wa kulinusuru ziwa letu kwenye ilani yetu tumesema tutahakikisha tunadhibiti uvuvi haramu ili tuweze kupata samaki wa kutosha kwa ajili ya watanzania sisi CCM tunaomba msiishie hapa endeleeni kudhibiti uvuvi haramu ili matunda yazidi kuongezeka siku hadi siku”alisema Katibu wa CCM


Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, David Palanjo aliongoza zoezi la uteketekezaji wa shehena ya nyavu haramu zilizokamatwa kwenye operesheni hiyo katika wilaya za Magu na Busega na kutoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu.
Share:

Tangazo la Nafasi za Kazi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba==>>Kwa Nafasi Zingine Nyingi Zikiwemo za Mabenk, Makampuni Binafsi <<BOFYA HAPA>>


Share:

Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo
Share:

K-lyinn Adai Kuzuiwa Kuingia Kwenye Kaburi La Reginald Mengi

Takriban mwaka mmoja baada ya kifo cha bilionea wa Tanzania Reginald Mangi, tayari kumeibuka mgogoro katika familia yake, baada ya mkewe Jacqueline Mengi kudai kwamba amenyimwa kuona kaburi la mumewe.

Katika chapisho lake la twitter, Klynn kama anavyofahamika anasema kwamba amenyamaza vyakutosha. Na sasa ameshindwa kuvumilia baada ya yeye na wanawe pacha kuzuiwa kuona kaburi hilo na kwamba walihitaji kuomba ruhusa.

Katika chapisho hilo malkia huyo wa urembo wa zamani anaendelea kusema kwamb; "Mmefikia hatua ya kunizuia mimi na wanangu kuingia kwenye kaburi la mume wangu, tunafukuzwa eti mpaka tuombe ruhusa ya kuingia kwenye kaburi la mume na baba wa watoto wangu! Nimechoka , sitakubali kuendelea kuona wanangu wakisononeka na sitakaa kimya", alisema Klynn.

Reginald Mengi alifariki mwaka jana mwezi Mei tarehe 2 huko Dubai akiwa na umri wa miaka 75. Wawili hao walikuwa wamefunga ndoa mwaka 2015 na kupata watoto wawili.

Familia ya bilionea huyo haijatoa tamko lolote.


Share:

Waziri Mkuu Awataka Watumishi wa Umma Watenge Muda wa Kusikiliza Kero za Wananchi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka watumishi wa umma nchini kote kutenga muda wa kusikiliza kero za wananchi.

Alitoa maagizo hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwanga Community Centre, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

“Watumishi mnatakiwa kwenda kwa wananchi na kusikiliza kero na kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi. …hamuendi na kama mngekuwa mnaenda kusingekuwepo na mabango kwani kitendo cha kuwepo mabango ni ishara tosha kuwa hamuendi,” alisema.

Alisema Serikali imepeleka fedha nyingi mkoani Kigoma za kugharamia miradi ya maendeleo zikiwemo sh bilioni 4.6 za ununuzi wa dawa ambapo Manispaa ya Kigoma Ujiji inapata sh milioni 50 kila mwezi hivyo hakuna sababu wananchi kukosa dawa.

Alisema Serikali ya Rais Dk John Magufuli imedhamiria kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya karibu na wananchi zikiwemo za afya ili kuwapunguzia watu, kutembea umbali mrefu hadi hospitali za wilaya au mkoa.

Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Baraza la Madiwani kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili kugharamia miradi ya maendeleo.

Alikemea wananchi katika maeneo mengi ya mkoa wa Kigoma kudai fidia maeneo hata ya mapori na kukwamisha baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya kanda.

Awali, Waziri Mkuu alishiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Mujahidina uliopo eneo la Buzebazeba mijini Kigoma.

Alitumia fursa hiyo kuwausia waumini wa dini ya Kiislam na wananchi kwa ujumla kuendelea kushikamana na kulinda amani. Pia aliwahamasisha walime zao la michikichi


Share:

Katibu Wa UVCMM Kata ya Hananasifu Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela Baada ya Kugundulika Sio Raia wa Tanzania

Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Kata ya Hananasifu, Mohamed Nyandu amehukumiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuishi nchini bila kibali.

Nyandu ambaye imeelezwa kuwa ni raia wa Burundi alikiri kutenda kosa hilo la kuishi nchini kinyume na sheria ya uhamiaji na kutoa taarifa za uongo zikihusisha urai wake.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Kinondoni Vicky Mwaikambo amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yote matatu yanayomkabili hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani na kumtaka kulipa faini ya Sh500,000 kila kosa au kwenda jela miaka mitatu na akitoka jela arudishwe nchini Burundi.

Akisomewa hati ya mashtaka na Wakili wa Serikali Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo amedai kuwa tarehe, mwezi na mwaka usiojulikana mshtakiwa huyo ameingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na alikamatwa Januari 20, 2020 na maofisa wa uhamiaji wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amedai kuwa Januari 20, 2020 katika ofisi za uhamiaji wilaya ya Kinondoni mshtakiwa huyo alikamatwa kwa kosa la kuishi nchini isivyo halali wakati akijua yeye ni raia wa Burundi.

Katika shitaka la tatu mshtakiwa huyo alitoa tarifa za uongo zikihusisha uraia wake kwa maofisa wa uhamiaji ili kujipatia kitambulisho cha Taifa cha Tanzania (Nida) wakati akijua yeye si raia wa Tanzania.

Baada ya kumtia hatiani, wakili wa Serikali alidai kuwa hawana rekodi ya makosa ya nyuma hivyo mshitakiwa anavyoonekana amejihusisha na siasa kwa muda mrefu lengo lake ni kitu gani ukizingatia uhalisia wa nchi aliyotoka katika mambo ya usalama.

“Hivyo naiomba mahakama hii impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,”alidai Shija.

Hata hivyo baada ya Hakimu Mwaikambo kumuhukumu kulipa faini ya Sh1.5 milioni lakini mshtakiwa huyo alishindwa kulipa faini hivyo ameenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Atarudishwa Burundi baada ya kumaliza kifungo.


Share:

UINGEREZA YAPIGA MARUFUKU UHUSIANO WA MAPENZI KATI YA WAFANYAKAZI NA WANAFUNZI

Chuo Kikuu cha London chaanzisha sera ya kupiga marufuku uhusiano wa mapenzi chuoni

Marufuku ya kuwa na uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha London ni mwamko mpya kwa vyuo vikuu, wachambuzi wamesema.

Makundi ya wanafunzi yamesema kwamba ni imani yao kuwa sera sawia na hiyo zitaanza kutekelezwa na vyuo vingine.

Chuo Kikuu cha London kinaaminika kuwa cha tatu nchini Uingereza kuanzisha marufuku hiyo.

Inasemekana kwamba sera hiyo inalenga kuzuia unyanyasaji kwa walio na madaraka na vitendo vya ngono.

Kelsey Paske, maneja wa kitengo kinachoangazia tabia ya utamaduni, amesema sera hiyo pia inalenga kutatua migogoro ambayo huenda ikazuka kutokana na mahusiano "huenda yakawa na athari mbaya katika mazingira ya kwenye taasisi za masomo".

Sera mpya ya mahusiano katika Chuo Kikuu cha London kwa wafanyakazi, kulingana na gazeti la the Guardian, inakataa "mahusiano ya karibu na ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi pale ambapo kuna usimamizi wa moja kwa moja".

Uhusiano wa mapenzi kati ya mfanyakazi na mwanafunzi ambaye hamsimamii kimasomo moja kwa moja ni lazima uwekwe wazi na mfanyakazi.

Sera hiyo pia inakataza mahusiano ya mapenzi na wafanyakazi au wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 au watu wazima ambao wako katika hatari mfano, yule ambaye atahitaji usaidizi maalumu kwasababu ya ulemavu.

Kukiuka sera hiyo kutachunguzwa na kitengo cha kukabiliana na utovu wa nidhamu chuoni, ambao ni pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua kuanzia kupewa onyo rasmi hadi kufutwa kazi au kufukuzwa chuoni.

Dr Anna Bull, wa shirika moja linalopinga vitendo dhidi ya tabia zinazoendeleza ngono katika taassi za shule za juu, amesema kwamba shirika lake linaunga mkono kikamilifu sera hiyo mpya na ni matumaini yao kwamba vyuo vingine vikuu vitafuata mkondo huo.

Alisema kuwa sera hiyo ni moja ya sheria kali Uingereza ambayo pia inatekelezwa na vyuo vikuu vingine viwili vya Greenwich na Roehampton.

Dr Bull ameongeza kuwa vyuo vingi vina sera ambazo zinakemea vikali uhusiano wa mapenzi kati ya wahadhiri na wanafunzi lakini sheria kama hiyo bado huenda ikatoa mwanya kwa wafanyakazi wanaotaka kuwa na uhusiano na wanafunzi ambapo wafanyakazi wanaweza kuitisha vikao nje ya jengo la chuo au hata kuzungumza na mwanafunzi kwa namna inayoashiria kuwa anatafuta uhusiano wa mapenzi.

"Tunaona kwamba huu ni mwito kwa sekta hii kuanza kuwajibika kwa kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya wahadhiri kutumia vibaya madaraka yao," amesema.
Share:

TYSON AMTWANGA DEONTAY WILDER RAUNDI YA 7 NA KUWA BINGWA MPYA WA WBC


Tyson Fury ameshinda pambano lake la leo Februari 23, 2020 la uzito wa juu dhidi ya Deontay Wilder kwa TKO raundi ya 7 na kuwa bingwa mpya wa WBC.Tyson alionyesha umahiri wake katika ulingo baada ya kumaliza ufalme wa Deontay Wilder wa miaka mitano na kuchukuwa mkanda wa WBC katika uzani mzito duniani baada ya kumwangusha binngwa huyo kwa njia ya knockout katika raundi ya saba.

Katika mechi iliochezwa katika Mecca ya ndondi mjini Las Vegas nchini Marekani raia huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 31 alimshinda mpinzani wake katika pigano ambalo ni wachache wangeweza kutabiri..

Mchanganyiko wa ngumi za kulia na kushoto ambazo Wilder amekuwa akizitumia kuwalambisha sakafu wapinzani wake zilitumika dhidi yake na kuangushwa katika raundi ya tatu na tano.

Fury alihakikisha ametimiza aliyoahidi na kubadili mbinu zake kutoka upigaji hadi mwenendo wake na kumzidia nguvu mpinzani wake ambaye hajawahi kushindwa.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Tyson ameandika: “Nataka kusema Deontay Wilder, ameonyesha weledi wake. Amepigana hadi raundi ya saba. Yeye ni shujaa, atarejea tena kuwa bingwa. “Lakini mfalme amerejea katika kiti chake.”

Tyson Fury akizungumza na BT Sport: “Nilimwambia kila mmoja kwamba mfalme anarejea kwenye kiti chake. katika pigano langu la mwisho karibu kila mmoja alinikashifu. Nilikuwa na uzani wa chini na nilifanya mazoezi kupitiza. Mimi ni muharibifu. lakini sio vibaya kwa mwanamasumbwi.

“Natimiza ninachosema. Nilimwarifu Wilder, timu yake, na dunia nzima. Tulifanya mazoezi ya knockout.

“Ninazungumza hivi kwasababu ninaweza kutoa ushahidi wa ninachokizungumzia. Watu walinisema vibaya, waliangalia kitambi changu na upara wangu na kudhania kwamba siwezi kupigana. Alipigana kwa weledi kadiri ya uwezo wake wote Tyson Fury na kila mmoja yuko katika kipindi chake cha juu.

“Namtarajia [Wilder] aombe pigano la tatu. najua kwamba yeye ni shujaa na mimi nitakuwa na msubiri.”

Fury kisha akasema kwamba anataka pambano la tatu dhidi ya Wilder lifanyike uwanja wa Las Vegas ambao kwa sasa unajengwa na utafunguliwa hivi karibuni.

Kulingana na timu yake, Wilder amepelekwa hospitali kushonwa baada ya kujeruhiwa kwenye sikio.

-BBC


Share:

JAJI KUFUNGULIWA MASHITAKA KWA KUDAIWA KUSHIRIKIANA NA MSHUKIWA WA MAUAJI

Jaji mmoja nchini Kenya anayejulikana kwa jina la Sankale Ole Kantai atafunguliwa mashtaka Mahakamani kufuatia madai kwamba alishirikiana na mshukiwa wa mauaji.

Jaji huyo wa Mahakama ya rufaa, Sankale Ole Kantai alikamatwa na maafisa wa jinai siku ya Ijumaa na kuhojiwa kuhusu uhusiano wake wa karibu na Sara Waimu , mshukiwa mkuu wa mauaji ya raia wa Uholanzi Tob Cohen.

Jaji huyo aliachiliwa siku ya Jumamosi mchana kwa dhamana baada ya kulala katika kituo cha polisi cha Muthaiga ambapo alikuwa anazuiliwa. Atawasilishwa mahakamani siku ya Jumanne.

Idara ya Jinai imethibitisha kwamba jaji huyo atafunguliwa mashtaka ya kuwa na njama ya kuilaghai haki na kuingilia mashahidi.

Mwili wa raia huyo tajiri kutoka Uholanzi ulipatikana katika shimo la maji taka nyumbani kwake jijini Nairobi 2019.

Kwa mujibu wa BBC, Maafisa wa polisi wanasema kwamba wana sababu za kuamini kwamba jaji Sankale alikuwa na uhusiano wa karibu na mshukiwa huyo ambaye amedaiwa kumpa ushauri ili kukabiliana na kesi yake mahakamani.


Share:

Mwanajeshi Mwingine wa Uturuki Auawa Kwa Bomu Na Vikosi Vya Syria Vinavyoungwa Mkono na Urusi

Askari mwingine wa Uturuki ameuawa kwenye shambulio la bomu katika mkoa wa Idlib. 

Huyo ni askari wa 16 kuuawa kwenye mashambulio yanayofanywa na vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi. 

Wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema mauaji hayo yametokea wakati ambapo mazungumzo ya kusitisha mapigano baina ya Ankara na Moscow yamekwama. 

Kuongezeka kwa vifo vya wanajeshi wa Uturuki, kunaweza kuondoa uwezekano wa kupatikana suluhu ya kusitisha mapigano katika eneo la Kaskazini magharibi mwa Syria. 

Tangu mapema mwezi Desemba, raia karibu milioni moja wa Syria wengi wao ni wanawake na watoto hawana makaazi na hasa katika kipindi hiki cha baridi kutokana na mapigano. 

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan anatarajia kukutana na viongozi wenzake wa Urusi, Ujerumani na Ufaransa Machi 5 kwa ajili ya kuuzungumzia mkoa wa Idlib.

Baada ya syria kukumbwa na vita kwa miaka tisa sasa, vikosi vya serikali ya Syria vinapambana kulidhibiti eneo hilo la mwisho linaloshikiliwa na waasi.


Share:

Kigwangalla Amuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo Awasamehe Waliosambaza Picha za Uharibifu wa Barabara Hifadhi ya Ngorongoro

Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla amewaombea msamaha waongoza utalii ambao walisambaza video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha uharibifu wa barabara kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Kupitia akaunti yake ya twitter, Dk Kigwangalla ameandika kuwa amemuomba Mkuu wa mkoa wa Arusha Nchini Tanzania, Mrisho Gambo na kamati ya ulinzi kuwasamehe na kuchukulia hilo kama onyo.

Kigwangalla amesema kwa kuwa ni tukio la kwanza, amempongeza Gambo kuingilia kati suala hilo ambalo ameeleza linalinda hadhi ya nchi.
 
Amesema ni vema taarifa kama hizo wawe wanazifikisha mahala husika ili zipatiwe ufumbuzi na ikishindikana afikishiwe Waziri moja kwa moja.

“Ni vema taarifa za changamoto zikafikishwa kwetu kwa njia sahihi. Kama mtu hawapati watu wetu wa huko chini, mimi napatikana kila kona, sijajifungia kwenye selo na sijabadili namba zangu! Nipe taarifa zako na nakuhakikishia nitachukua hatua stahiki na kwa wakati,” ameandika Kigwangalla.

“Huwa sipuuzi taarifa wala ushauri na siangalii umetoka kwa nani. Nafanyia kazi kila kitu. Na ndiyo maana hata majangili tunawakamata kila siku. Kweli tuna uhuru wa kusema na kufanya lolote, lakini tuutumie vizuri kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Hii ni nchi yetu sote, tuilinde, tuipende, tuijenge, tuifaidi,” ameandika.


Share:

Serikali Yajipanga Kutokomeza Magonjwa Ya Mifugo Nchini.

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali itahakikisha inaendelea kutoa dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo nchini ikiwa na lengo la kutokomeza kabisa magonjwa ya mifugo.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo (22.02.2020) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika mnada wa mifugo wa Ndelema uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Handeni Mkoani Tanga ambapo amewataka wafugaji kutoacha kuosha mifugo yao kwani kwa kufanya hivyo mifugo itakuwa na afya njema na hatimaye kupata bei nzuri ya soko.

“Mwaka jana tulipata pesa kutoka kwa mheshimiwa rais zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kununua dawa na kugawa kwa majosho 1,400 nchi nzima, mwaka huu wametuongeza tumepata zaidi ya Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kununua dawa na kusambaza katika majosho 1,700 tutaendelea na zoezi hilo la kutoa dawa za ruzuku bila kuacha ili kuhakikisha tunapiga kabisa vita magonjwa ya mifugo.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha kuhusu wafugaji wa Wilaya ya Handeni kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali Naibu Waziri Ulega akizungumza moja kwa moja kwa njia ya simu katika mkutano huo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amemtaka kuweka alama katika misitu hiyo ili wafugaji waweze kutambua misitu ya serikali na kutoingiza mifugo yao kwa bila kukusudia.

Prof. Silayo amemuahidi Naibu Waziri Ulega katika mkutano huo kuwa atawatuma wataalamu siku ya Jumatatu ili kuanza utekelezaji huo mara moja na kuondoa migogoro ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali.

Katika mkutano huo pia naibu waziri huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni kuhakikisha unatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ikiwemo ya miundombinu katika mnada huo pamoja na barabara ili waweze kusafirisha mifugo yao kwa urahisi zaidi.

Nao baadhi ya wafugaji waliopatiwa nafasi kuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya sekta ya mifugo, wameipongeza serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikihakikisha inawaboreshea mazingira ya shughuli zao huku wakiomba wazidi kupatiwa elimu zaidi ya masuala mbalimbali ili wafanye shughuli zao bila kukiuka sheria za nchi.

Awali akitembelea bwawa la asili katika Kijiji cha Kweingoma kilichopo Wilaya ya Handeni Vijijini Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo lenye urefu wa Kilometa Nne kujiunga katika ushirika ili serikali iweze kuwasaidia katika maeneo mbalimbali huku akiahidi kutoa mashine kwa ajili ya mtumbwi utakaotengenezwa na uongozi wa wilaya hiyo ili kurahisisha shughuli za uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Tanga ambapo amepita pia katika Wilaya za Muheza, Pangani, Mkinga na Halmashauri ya Jiji la Tanga na kuzungumza na wafugaji na wavuvi ili kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo.


Share:

Utatuzi Migogoro Ya Ardhi Dar Es Salaam Wamfikisha Lukuvi Saa Nne Usiku

Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepongezwa na wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa uamuzi wake wa kukutana nao na kutatua migogoro ya ardhi 628 katika mkoa huo katika kipindi cha siku tano kupitia progaramu ya Funguka kwa Waziri hadi saa nne usiku.

Lukuvi alihitimisha programu ya Funguka kwa Waziri kwa kukutana na wananchi wa Manispaa ya Kinondoni jana tarehe 22 Februari kwa kusikiliza na kutatua kero, malalamiko na migogoro mia tatu (300) iliyomfikisha saa 4:22 usiku.

Awali, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikutana na wananchi wa Manispaa za Ilala ambapo alishughulikia migogoro 122, Ubungo 75, Kigamboni migogoro 65 na Manispaa ya Temeke migogoro 66 na kufanya jumla ya migogoro aliyoishughulikia kwa siku zote tano kufikia 628.

Kati ya Wananchi aliokutana nao tangu kuanza kwa program hiyo siku ya jumanne tarehe 18 Februari 2020, Manispaa ya Kinondoni ilioonekana kuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye malalamiko ya ardhi ukilinganisha na Manispaa nyingine za mkoa wa Dar es Salaam.

Baadhi ya Wananchi waliokutana na Waziri Lukuvi walionesha kufurahishwa na utaratibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kukutana na wananchi kwa nia ya kupata suluhu ya migogoro ya ardhi iliyoelezwa kuwa imekuwa ikiwahangaisha kwa muda mrefu bila mafanikio.

Raphael Ngowi mkazi wa Kinondoni ambaye malalamiko yake ni kuhusiana na kiwanja chake kumilikishwa kwa watu wawili alisema, utaratibu wa Waziri wa Ardhi kukutana moja kwa moja na wananchi unamsaidia kupata mambo mengi kutoka kwa mhusika badala ya kusikia kutoka kwa watendaji.

Alisema, utaratibu huo siyo tu unasaidia wananchi wenye matatizo ama kudhulumiwa haki zao katika sekta ya ardhi bali unatoa pia fursa kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi kubainia uzembe wa baadhi ya watendaji wake katika maeneo yenye migogoro.

Kwa mujibu wa Ngowi, kati ya Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano, Lukuvi amevunja rekodi kwa kuweza kutatua matatizo ya wananchi kwa kukutana nao ana kwa ana jambo alilolieleza kuwa limeasisiwa na Mwl. Nyerere kwa kuweka uwazi wa kushugulikia kero.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya wenye Mashamba eneo la Mabwepande katika manispaa ya Kinondoni Seif Maungu anayewakilisha wananchi 258 walio katika mgogoro wa kuvamiwa eneo lao alisema, baada ya kuonana na Waziri Lukuvi sasa wamepata faraja kubwa baada ya mateso ya takriban miaka 13.

‘’Kwa muda mrefu tulikuwa hatupati majibu kuhusiana na mgogoro wa maeneo yetu lakini sasa baada ya kukutana na mhe. Lukuvi tumepata faraja na Rais Magufuli amepata jembe’’ alisema Maungu.

Mkazi mwingine wa Magomeni aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Maulid Kinyogoli aliyewasilisha tatizo lake la kutopata Hati ya Ardhi, aliilezea program ya Funguka kwa Waziri kuwa ni mwarobaini wa matatizo ya ardhi yanayosababishwa na watendaji wa sekta ya ardhi wasiokuwa waaminifu.

‘’Utaratibu wa Funguka kwa Waziri uliaonzishwa na Lukuvi kwa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi ungekuwa ukifanywa na viongozi wengine kupitia sekta zao basi matatizo yangepungua na hivyo kumrahisishia kazi Rais John Pombe Magufuli ya kuleta maendeleo’’ Alisema Kinyogoli.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi wenye malalamiko na kero za ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kwa nia ya kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi ambapo tayari program hiyo imeshafanyika mikoa mbalimbali ikiwemo Kilimanjaro, Tanga, Rukwa, Mbeya, Iringa, Tabora, Kigoma, Kagera, Katavi na Lindi na kuleta mafanikio makubwa.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili February 23

Share:

Saturday, 22 February 2020

Picha : HOTELI YA KISASA 'SAM COMFORT' YAFUNGULIWA RASMI SHINYANGA MJINIHoteli ya Kisasa iitwayo ‘Sam Comfort’ iliyopo katika Mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga imefunguliwa rasmi leo Jumamosi Februari 22,2020.Uzinduzi wa Hoteli hiyo ya Kisasa umehudhuriwa na wadau mbalimbali mjini Shinyanga.

Akizungumza kwa niaba ya Mmiliki wa Hoteli 'Sam Comfort' Samwel Mabala, Humphrey Godfrey Katege amesema Samwel ni mzawa wa Shinyanga amethubutu kuwekeza mkoani Shinyanga na anawaomba wadau wa ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga kumuunga mkono.

“Nawashukuru wote mliofika hapa kutuunga mkono,naamini kuanzishwa kwa Hoteli hii ya kisasa ni sehemu ya kuchangia shughuli za maendeleo katika mkoa wetu wa Shinyanga na taifa kwa ujumla”,amesema Katege.

Naye Mjomba wa mmiliki wa Hoteli, Chief Thomas Ng’ombe amesema miongoni mwa huduma zinazopatikani hotelini hapo ni vyumba vya kulala, chakula na vinywaji mbalimbali.

“Leo tumezindua rasmi Hoteli hii ambayo inapatikana katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi. Tunawakaribisha wateja wote kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga,huduma zetu ni nzuri kwa gharama nafuu ambayo ni rafiki kwa kila mtu”,amesema Chief Ng’ombe.

“Sam Comfort imejengwa na ndugu Samwel Mabala mkazi wa Shinyanga,Kijana huyu kwa muda mrefu amekuwa akipanga kujenga Hoteli na amejisikia faraja kubwa kuwekeza katika mkoa wa Shinyanga. Tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu kabisa,naomba mjisikie mpo nyumbani”,ameongeza Chief Ng’ombe.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa mtaa wa Dome,Solomoni Nalinga Najulwa amempongeza mmiliki wa hoteli ya Sam Comfort kujenga hoteli ya Kisasa katika mtaa wake kwani ameonesha uzalendo wa hali ya juu na ameahidi kumuunga mkono.

Wasiliana na wahusika wa Hoteli ya ‘Sam Comfort’ kwa simu namba 0747874636
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwenyekiti wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Solomoni Nalinga Najulwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Hoteli ya ‘Sam Comfort’  usiku wa Jumamosi Februari 22,2020 ambapo amempongeza mmiliki wa hoteli ya Sam Comfort kujenga hoteli ya Kisasa katika mtaa wake. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mjomba wa mmiliki wa Hoteli, Chief Thomas Ng’ombe akiwakaribisha wateja wote kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga kufika katika hoteli ya Sam Comfort kupata huduma ya vyumba vya kulala,vyakula na vinywaji kwa gharama nafuu ambayo ni rafiki kwa kila mtu.
 Humphrey Godfrey Katege akizungumza kwa niaba ya Mmiliki wa Hoteli ya Sam Comfort Samwel Mabala ambapo amesema Samwel amethubutu kuwekeza mkoani Shinyanga na kuomba wadau ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga kumuunga mkono.
Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa Hoteli 'Sam Comfort'.
Wadau mbalimbali waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa Hoteli 'Sam Comfort'.
Meneja wa Sam Comfort, Jackson Wilson akielezea huduma zinazopatikana katika hoteli yao ambazo ni pamoja na vinywaji,vyakula na vyumba vya kulala vyenye, Tv, maji ya moto na ya baridi.
Muonekano wa sehemu ya Hoteli ‘ Sam Comfort’ iliyopo katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Muonekano wa sehemu ya Hoteli ‘ Sam Comfort’ iliyopo katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Muonekano wa sehemu ya Hoteli ‘ Sam Comfort’ iliyopo katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Bango linaloelekeza ilipo Hoteli ‘ Sam Comfort’.
Muonekano wa sehemu ya mapokezi Sam Comfort.
Muokano wa sehemu ya chumba katika hoteli 'Sam Comfort'
Muonekano wa sehemu ya choo/bafu katika hoteli 'Sam Comfort'.
Muonekano wa sehemu ya chumba katika hoteli ya Sam Comfort.
Muonekano wa sehemu ya Vinywaji katika hoteli 'Sam Comfort'.
Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa Sam Comfort.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Crown Pub,Musa Jonas Ngangala na Mkurugenzi wa La Prince, Athanas William wakijiandaa kufungua Shampen wakati wa ufunguzi wa Sam Comfort'.
Mkurugenzi wa Crown Pub,Musa Jonas Ngangala akigonga Cheers na viongozi wa Sam Comfort na wadau waliojitokeza kwenye uzinduzi wa Hoteli 'Sam Comfort'.
Mkurugenzi wa Crown Pub,Musa Jonas Ngangala akigawa vinywaji.
Zoezi la kugonga Cheers likiendelea.
Zoezi la kugonga Cheers likiendelea.
Zoezi la kugonga Cheers likiendelea.
Kulia ni Mmiliki wa Sam Comfort, Samwel Mabala akiwa ameshikilia kinywaji wakati wa zoezi la kugonga Cheers.
Wadau na viongozi wa Sam Comfort wakifurahia jambo.
Zoezi la kugonga cheers likiendelea.
Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Derick Elias akifuatiwa na Mjomba wa mmiliki wa Hoteli, Chief Thomas Ng’ombe na Mmiliki wa Sam Comfort, Samwel Mabala (kulia) wakicheza muziki wakati wa ufunguzi wa Sam Comfort.
Kulia ni MC Seki akieleza jambo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lulekia, Ansila Benedict akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sam Comfort.
Mkurugenzi wa Hoteli ya Liga, Moris akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sam Comfort.
MC Seki akitoa maelekezo mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa Hoteli ‘Sam Comfort’.
Wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa Sam Comfort.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

TANGAZO LA TOUR MBUGA YA SAADAN

TANGAZO LA TOUR MBUGA YA SAADAN

FUNGUA PAZIA

NDOA ZA UTOTONI

Narudi nyumbani

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger