Wednesday, 25 September 2019

Waziri Mkuu: Tutaendelea Kulinda Viwanda Vya Ndani

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 25, 2019) alipotembelea kiwanda cha maziwa cha Asas, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa. Amesema Serikali imedhamiria kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia sekta ya viwanda.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini kuwa uchumi wa viwanda ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Serikali imefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo ili kuhakikisha inaleta tija kwa wafugaji na taifa kwa ujumla, hivyo wafugaji endeleeni kuimarisha ushirika wenu. Wizara ya Mifugo iendelee kuwaelimisha wafugaji ili wafuge kitaalamu.”

Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya Asas kwa sababu ni miongoni mwa kampuni chache ambayo imeanza kutoa elimu kwa wafugaji juu ya namna bora ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni bora za ufugaji wa kisasa pamoja na kuwapa uhakika wa soko.

Amesema Serikali inathamini sana uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Asas kwa sababu wameitikia wito wa Serikali wa ujenzi wa uchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo itahakikisha wawekezaji wote wananufaika na uwekezaji wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Maziwa cha Asas, Fuad Abri amesema kiwanda chao kinampango wa kupanua uzalishaji kwa kujenga kiwanda kingine cha kusindika maziwa katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Awali,Waziri Mkuu alizindua kiwanda cha maji cha Mkwawa cha mjini Iringa na kusema kuwa ujenzi huo ni njia ya uhakika ya kupunguza tatizo la ajira na kwamba itaendelea kushawishi wawekezaji wa ndani na nje ili wananchi wengi wapate ajira.

“Serikali imetoa wito kwa wawekezaji wawekeze katika viwanda mbalimbali nchini, hivyo ni muhimu wawekezaji hao wakalindwa na wasibugudhiwe ili waweze kuendelea na uzalishaji wa bidhaa zao. Watumishi mlioajiriwa fanyeni kazi kwa uaminifu.”

Naye,Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda cha Maji cha Mkwawa,Ahmed Huwel alisema kiwanda chao kilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kuzalisha na kufanya biashara ya maji safi na salama pamoja na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Alisema kiwanda chao kimeajiri watumishi158 kati yao wanaotoka nje ya nchi ni watatu tu na kwa upande wa ajira zisizo rasmi ni zaidi ya 3,000 na kwamba wanatarajia kuongeza ajira kwa wananchi wengi zaidi baada ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda kingine cha kutengeneza vinywaji baridi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazokikabili kiwanda hicho alisema ni pamoja na ukatikaji wa umeme wa mara kwa mara hali inayosababisha kuharibika kwa baadhi ya mitambo hivyo ameiomba Serikali iwasaidie.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger