Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
SEKTA ya Kilimo imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika kipindi hiki tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kilimo kimeendelea kuimarika na hivyo kuchangia asilimia 30.1 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29.2 kwa mwaka 2016 pamoja na kuchangia ajira wananchi kwa asilimia 65.5 na kuchangia malighafi za viwanda kwa asilimia 65.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta zinaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara na kuboresha miundombinu wezeshi ili kuwezesha upatikanaji wa chakula na masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yote.
Huduma za Ugani ni muhimu sana katika kufikisha na kuelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi mbinu bora za kuongeza tija katika uzalishaji, ubora wa mazao kwa usalama wa chakula na lishe pamoja na upatikanaji wa malighafi za viwanda vinavyotegemea kilimo, mifugo na uvuvi.
Aidha, huduma za Ugani hapa nchini zinatolewa kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo ubinafsishaji, mikataba, sekta ya umma na binafsi, ugatuaji wa huduma za ugani na utandawazi wa soko huria. Baada ya ugatuaji wa madaraka (1997) majukumu ya kutekeleza huduma za ugani yalihamishiwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Baada ya ugatuaji wa huduma za ugani kumekuwako na changamoto mbalimbali za kiutendaji ikiwemo Ufuatiliaji na uratibu wa huduma za ugani katika Halmashauri umekuwa na mapungufu kwani hakuna uwajibikaji wa moja kwa moja wa wataalam wa Kilimo walioko Halmashauri na Wizara ya Kilimo pamoja na Halmashauri kutoajiri wataalamu wa kutosha wa ugani, kutotoa motisha kwa kuwaendeleza watumishi wake hivyo kuathiri utoaji wa huduma za ugani.
Ili kufikia malengo iliyoyaweka katika Sekta ya Kilimo nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (2017/2028), ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo ambapo utekelezaji wake utazingatia kuimarisha utafiti, huduma za ugani na mafunzo; upatikanaji wa masoko ya mazao na miundombinu ya uzalishaji.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadiro ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema Serikali imeendelea kuboresha vyuo na vituo vya mafunzo ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya wataalam wa ugani kilimo katika ngazi ya kijiji na kata.
Anasema kuwa Katika mwaka 2018/ 2019, Wizara kupitia vyuo vyake 14 vya kilimo imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389 ambapo wanafunzi 2,051 wamefadhiliwa na Serikali ambapo wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada na 852 ni ngazi ya Stashahada na jumla ya wanafunzi wanafunzi 1,026 wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada wamehitimu masomo yao mwezi Juni, 2019.
“Vyuo hivyo vinatoa Astashahada na Stashahada za Kilimo Mseto, Stashahada ya Umwagiliaji, Matumizi Bora ya Ardhi, Uzalishaji Chakula na Lishe, Matumizi ya Zana za Kilimo, Uzalishaji wa Mazao, Mboga, Maua na Matunda” anasema Waziri Hasunga.
Waziri Hasunga anasema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Lutheran World Relief (LWR) kupitia mradi wa Invest imehuisha mtaala wa Kilimo Mseto na kuzalisha mtaala mpya wa kilimo (Agriculture Production) ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kutimiza masharti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Akifafanua zaidi Hasunga anasema mradi wa Invest umejenga kitalu nyumba katika Chuo cha Taifa cha Sukari Kidatu ili kutoa mafunzo bora kwa wagani tarajali na wakulima na kuwajengea uwezo wakufunzi 20 kutoka vyuo vya Kilimo Ilonga (Kilosa), KATRIN (Ifakara) na Chuo cha Taifa cha Sukari Kidatu ili wafundishe kwa kufuata mwongozo wa mfumo wa moduli.
Anaongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ysa Kilimo imeendelea kuwajengea uwezo wakufunzi wa kilimo 22 ambapo wakufunzi 10 wapo katika mafunzo ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) na 12 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi nchini India na China pamoja na kushirikiana na Taasisi Binafsi kuandaa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi ya kuwajengea uwezo wakulima kuhusu teknolojia mbalimbali za kilimo.
Kwa mujibu wa Hasunga anasema Mafunzo hayo yalihusu Kilimo cha Korosho, Mtwara (wakulima 67), Kilimo cha Mahindi na Maharage, Ukiriguru (wakulima 51), Usindikaji wa mazao- Uyole (wakulima vijana 56), na Kilimo bora cha soya (wakulima 31), Kilimo shadidi cha mpunga (wagani 33), kilimo bora cha alizeti (wakulima 25 na wagani 5), na kilimo bora cha mpunga (wakulima 20), Ilonga.
Hasunga anasema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), kupitia mradi wa TANRICE2 imetoa mafunzo kwa wakulima wa mpunga 1,964. Kati ya hao, wakulima 923 wametoka katika skimu za umwagiliaji za Kimbande Nyasa (Ruvuma), Magoma (Korogwe) Wamiluhindo (Mvomero), Tulokongwa (Morogoro), SololaNkanga (Sumbawanga) na Legezamwendo (Tunduru), Litumbadyosi (Mbinga), Njomulole (Namtumbo), Msanjesi (Namtumbo) na Kyamyorwa (Muleba).
ASDP II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya Taifa, ili kukabiliana na mapungufu na changamoto za sekta ya kilimo na kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la Taifa, kuboresha ukuaji wa pato la wakulima wadogo na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ifikapo 2025.
Ni wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Wilaya kujenga uwezo katika huduma za umma ili kuviwezesha vyama vya wakulima wadogo kulima kibiashara kusaidia kuwaunganisha wafanya biashara wa sekta ya kilimo na mfumo wa uzalishaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa ajili ya soko na kuendeleza mnyororo wa thamani.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment