Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro, amewataka wahitimu wa mahafali ya 42 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuitumia elimu waliyoipata kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii zinazowazunguka kupitia maeneo yao ya kazi ama makaazi.
Dkt. Ndumbaro, ametoa rai hiyo Disemba 14, 2023 katika uwanja wa Majimaji uliopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, alipohudhuria mahafali hiyo kama mgeni rasmi.
“Mlichopata hapa siyo cheti, bali ni elimu ambayo ili iwe na manufaa inabidi mkaitumie kutatua changamoto zilizopo katika jamii kwa kuisaidia na kufanya tafiti zenye tija. Wakati tunaelekea kupata dira mpya ya taifa ya mwaka 2025, katumieni elimu mliyopata kutoa maoni, uzoefu na maono yenu kupitia mijadala itakayowezesha kupata dira makini kwa taifa letu, Pia, mnapaswa kutumia ujuzi na maarifa mliyopata kuwa wabunifu wa kuziona fursa na kuzichangamkia ili kuzalisha ajira kwa vijana na jamii kwa jumla,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Aidha, amekitaka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuutumia upekee wake kueneza na kukuza Kiswahili ulimwenguni.Vile vile, ametoa rai kwa chuo kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa kuhakikisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni ndani na nje ya nchi unafanikiwa ili kuendana na ajenda mahsusi ya taifa ya kukuza, kueneza na kubidhaisha Kiswahili katika Bara la Afrika na duniani kwa jumla.
Akizungumza katika mahafali hiyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Omary Juma Kipanga, akimuwakilisha Waziri wa wizara hiyo Prof. Adolf Mkenda, amesema mifumo ya elimu imekuwa ikiimarishwa mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya ulimwengu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, teknolojia na kijamii.
“Mabadiliko haya yanailazimu serikali kufanya mapitio ya sera ya elimu kuanzia ngazi ya msingi ili kuiwezesha nchi kupiga hatua. Tunajua kuwa hili pia ni kipaumbele kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na chuo hiki kina jukumu la kubeba dhamana ya haya mabadiliko yanayofanyika kwa kuwa ni wadau muhimu wa mabadiliko hayo. Lengo ni kuwa na aina ya elimu itayozalisha wahitimu wenye ujuzi, maarifa na uwezo wa kujitegemea katika kujiajiri na kuajiri wengine," amesema Mh. Kipanga.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Joseph Kuzilwa, amesema kitendo cha serikali kukipatia chuo hiki fedha za ujenzi maabara saba za sayansi za kikanda nchini, ni ishara tosha kuwa serikali inathamini elimu ya juu hususani inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia mifumo ya masafa, mtandao, ana kwa ana na huria.
“Chuo hiki kimekuwa mstari wa mbele katika kusambaza utamaduni wetu kupitia lugha ya Kiswahili, kimeanzisha programu za kufundisha Kiswahili katika nchi ya Malawi na sasa kinakamilisha mipango ya kufundisha Kiswahili nchini Namibia. Chuo kinakaribisha ushauri na ushirikiano wa namna yoyote ili kufanikisha kukipeleka Kiswahili sehemu mbalimbali duniani,” amesema Prof Kuzilwa.
Naye Makamu Mkuu wa chuo, Prof. Elifas Bisanda, amesema kitendo cha serikali kuendelea kuchangia maendeleo ya chuo ni kuthamini machango wake kwa jamii na hivyo kukifanya chuo kiendelee kutimiza wajibu wake wa kutoa elimu kwa wanachuo huku wakiwa wanaendelea na shughuli zao huko huko walipo.
“Siyo lazima uache kazi zako uende chuoni, tunatumia zaidi TEHAMA katika ufundishaji na hata ada unalipa kwa kiwango unachotaka wewe mwanafunzi. Pia, mwanafunzi anaweza kuomba kufanya mitihani wakati wowote, ni mifumo tofauti na vyuo vingine,” amesema Prof. Bisanda.
Katika Mahafali ya 42 yaliyofanyika mjini Songea, jumla ya wahitimu 3980 katika ngazi za cheti, astashahada, shahada za kwanza, shahada za umahiri na uzamivu wamehitimu, ambapo asilimia 44 ya wahitimu hao ni wanawake. Hii ni hatua kubwa katika kuinua uwiano wa kijinsia katika elimu ya juu ikilinganishwa na miaka 12 iliyopita ambapo wahitimu wanawake walikuwa hawazidi asilimia 25 ya wahitimu wote.
0 comments:
Post a Comment