Serikali
imeendelea kufanya msako wa kuwabaini watumishi hewa ambapo mpaka
kufikia tarehe 20 mwezi huu jumla ya watumishi 16,127 wamebainika kukosa
vigezo vya kuajiriwa huku sekta ya elimu ikitajwa kuongoza.
Takwimu hizo zinatolewa na naibu waziri wa fedha na mipango Dkt.
Ashatu Kijaji wakati wa zoezi la ugawaji madawati kwenye kata 21 za
halmashauri ya wilaya ya Kondoa ambapo amesema tatizo la watumishi hewa
limeigharimu serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Awali katika zoezi hilo mkurugenzi wa halmashauri ya Kondoa Falesy
Kibasa amesema licha ya zoezi la madawati kufanyika kwa ufanisi lakini
bado wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa
pamoja na waalimu.
Katika ugawaji huo mwenyekiti wa kamati ya elimu afya na maji ya
halmashauri hiyo Zakaria Balajina amesema halmashauri imejiwekea mkakati
wa kuyatunza madawati kwa kuwakabidhi kwa mikataba maalum wakuu wa
shule ili waweze kuwajibishwa itakapobainika kumekuwepo na uzembe katika
utunzaji wake.
Katika zoezi hilo jumla ya madawati 2,260 yamekabidhiwa katika
hatua ya awali na linatarajiwa kuwa endelevu ili kukidhi mahitaji katika
shule zote za msingi na sekondari.
0 comments:
Post a Comment