Thursday 25 August 2016

Rais Magufuli Atuma salamu za Rambirambi Ajali Morogoro Iliyoua Watu 12

...

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa, Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.

Ajali ya kwanza imetokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016 ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016 baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.

Katika salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu, ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.

“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na uwaambie naunga nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina”amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili waendelee na kazi zao za kila siku.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
02 Julai, 2016
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger