Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa leo tarehe 27
Agosti, 2016 ameadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya Miaka 50 ya Ndoa yake na
Mama Anna Mkapa katika kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay
Jijini Dar es Salaam.
Hafla ya Jubilei hiyo imefanyika nyakati za mchana katika ukumbi wa
Kardinali Rugambwa uliopo kando ya kanisa la Mtakatifu Petro-Oysterbay
na imetanguliwa na Misa ya shukrani iliyofanyika katika kanisa hilo
majira ya asubuhi.
Jubilei hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama
Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais Mstaafu
wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu ya
Sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, Mke wa Baba wa Taifa Mama
Maria Nyerere, Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. Cleopa Msuya, Dkt. Salim
Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba na Mhe. Edward Lowassa.
Misa Takatifu ya Shukrani imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Arusha Mhashamu Askofu Josephat Lebulu na kuhudhuriwa na
Maaskofu na Maaskofu Wakuu saba akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu Rais Magufuli
amempongeza Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa kwa kutimiza miaka 50 ya
ndoa na ameeleza kuwa ndoa hiyo iliyowaunganisha wanandoa wanaotoka
katika madhehebu tofauti ya Kikristo imetoa fundisho kubwa kuwa binadamu
wanapaswa kuwa wamoja hata kama wana tofauti mbalimbali zikiwemo za
kimadhehebu ya dini, siasa na kanda.
Rais Magufuli amesema miaka 50 ya ndoa ya Mhe. Benjamin William Mkapa
ambaye ni Muumini wa Kanisa Katoliki na Mkewe Mama Anna Mkapa ambaye ni
Muumini wa Kanisa la Kilutheri inawafundisha watanzania wote hususani
wanasiasa kuishi kwa upendo na kuilinda amani waliyonayo na ametoa wito
kwa viongozi dini kuendeleza juhudi zao za kuliombea taifa na
kuwaunganisha wananchi licha ya tofauti walizo nazo.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William
Mkapa pamoja na kuwashukuru Viongozi wote, ndugu, jamaa na marafiki
waliohudhuria Misa ya Shukrani na Jubilei hiyo ya miaka 50 ya ndoa yake
amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia ndoa yake umri mrefu.
Rais Mstaafu Mkapa pia ametoa wito kwa watanzania kupenda na
kushirikiana huku akibainisha mafunzo aliyoyapata kutoka kwa viongozi wa
dini kuwa "Kila mmoja ni zawadi kwa mwenzake"
Nae Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo amempongeza Rais Mstaafu Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa
kwa kuadhimisha miaka 50 ya ndoa na amewasihi watanzania kuiga mfano
mwema uliooneshwa na wana ndoa hao ambao wamedumu katika imani bila
kuyumba.
Kardinali Pengo amesema ndoa ya Rais Mstaafu Mkapa anaifundisha jamii kuwa tunaweza kuishi kwa imani zetu bila kubadili dini
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
27 Agosti, 2016
0 comments:
Post a Comment