Tunapenda
kutoa maelezo kutokana na taarifa iliyotolewa katika gazeti la Jamhuri
la Jumanne tarehe 16 – 22, 2016. Toleo na. 255 iliyokuwa na kichwa cha
habari Prof. Muhongo avurunda.
Watanzania na Taifa kwa jumla wanashuhudia jinsi Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Muhongo na viongozi wengine wote wa Wizara ya Nishati na Madini wanavyofuatilia majukumu yao kwa karibu ikiwemo sekta ya mafuta.
Mhe.
Prof. Muhongo na viongozi wa Wizara wamekuwa wakitoa miongozo na
maelekezo juu ya sekta ya mafuta ambapo kumeendelea kuwa na uhakika wa
upatikanaji wa mafuta nchini kwa wakati wote.
Ni
imani yetu kuwa Mhe. Prof. Muhongo ataendelea kutekeleza majukumu yake
vizuri na hivyo kuendelea kutimiza matumaini ya Mhe. Rais na Taifa kwa
jumla katika mambo yote yanayohusu wizara ya nishati na madini ikiwemo
sekta ya mafuta.
Tunapenda
pia kueleza kuwa maagizo yote aliyotoa kuhusiana na mafuta ya ndege
yaliyokuwa yamechanganyika na mafuta ya petroli yalitekelezwa kwa
ukamilifu.
Maagizo
hayo yalikuwa ni Kampuni ya Sahara kuondoa mafuta yaliyochanganyika
kutoka katika maghala na mabomba na pia kusafisha maghala na mabomba
hayo ili kuwezesha kupokea mafuta mengine safi.
Kampuni
ya Sahara ilitekeleza kwa ukamilifu maagizo haya. Usimamizi wa maagizo
haya ulikuwa kwa PBPA na EWURA ambapo taasisi hizi zilisimamia
utekelezaji wake. Hivyo si kweli kwamba Prof. Muhongo ameshindwa
kusimamia maagizo yake.
Zuio
la Kampuni ya Sahara kushiriki katika zabuni lilitolewa na PBPA kwa
kutumia mamlaka yaliyo katika Kanuni. Zuio hili lilitolewa na PBPA ili
kuhakikisha mafuta yaliyochanganyika yanaondolewa katika maghala na
kusafishwa kwa maghala hayo na mabomba ikiwa ni pamoja na kukamilishwa
kwa uchunguzi ili kutambua kuwa mafuta haya yalichanganyika sehemu
gani.
Ifahamike
kuwa mara baada ya meli iliyokuwa imeleta mafuta haya (mafuta ya ndege
na mafuta ya petroli) kufika hapa, mafuta hayo yalipimwa na TBS.
TBS
walithibitisha kuwa mafuta yote katika meli hii yako katika kiwango cha
ubora unaotakiwa. Aidha, TBS walitoa idhini ya kuteremshwa kwa mafuta
hayo. Meli ilianza kuteremsha mafuta haya tarehe 4/5/2016 na kumaliza
kuteremsha tarehe 8/5/2016. Meli hii iliruhusiwa kuondoka mara baada ya
kumaliza kupakua mafuta na taratibu zote kukamilika.
Taarifa
ya kuchanganyika kwa mafuta haya ilitolewa tarehe 12/5/2016 wakati meli
tayari ilikuwa imekwishaondoka. Hivyo kulazimu kufanyika uchunguzi wa
kujua ni wapi mafuta haya yalichanganyika.
Suala
la uchunguzi wa wapi mafuta yalichanganyika lilikataliwa na makampuni
ya mafuta kama ilivyokuwa imependekezwa na kampuni ya Sahara. Makampuni
ya mafuta yalisimamia katika taarifa ya uchunguzi ya awali iliyofanywa
na pande zote husika.
Taarifa
hii ilikuwa na mapendekezo tofauti kati ya makampuni ya mafuta na
kampuni ya Sahara. Hivyo, kwa kuzingatia hatua hii kilichokuwa kimebakia
ni kufuata mkataba kati ya pande mbili hizi.
Kuondolewa
zuio la Kampuni ya Sahara kushiriki katika zabuni kulitolewa pia na
PBPA kwa kutumia mamlaka yaliyo katika Kanuni. Hii ilikuwa ni baada ya
kuhakikisha kuwa mafuta yaliyochanganyika yameondolewa, usafi wa maghala
na mabomba umefanyika na kampuni ya Sahara imelipa thamani ya mafuta
yote yaliyoondolewa katika maghala.
Sheria
ya Petroli (Petroleum Act, No. 21) ya mwaka 2015 imetoa adhabu kwa yule
atayaleta mafuta ambayo hayakidhi viwango vya vya ubora unaotakiwa.
Aidha, Kanuni ya uagizaji wa mafuta kwa pamoja (The Petroleum (Bulk
Procurement) Regulations) ya mwaka 2015 nayo imetoa adhabu juu ya kosa
la kuleta mafuta yasiyokidhi viwango vya ubora.
Kutokana
na mazingira haya ya adhabu katika kosa tajwa, PBPA iliomba kupata
mwongozo kutoka katika Mamlaka za kisheria ili kuhakikisha kuwa adhabu
inayotolewa iko katika misingi sahihi ya ki-sheria.
Ni
vyema ikafahamika kuwa hakuna sehemu ambapo PBPA imedanganya Taifa. Ni
kweli kabisa kuwa Sheria, Kanuni na Mikataba inaeleza juu ya mafuta
yaliyoletwa na kukutwa hayajafikia viwango vya ubora unaotakiwa. Mafuta
haya hayateremshwi na hutakiwa kurudishwa na yule aliyeyaleta, ikiwa ni
pamoja na kutekelezwa kwa taratibu zingine kwa mujibu wa Sheria, Kanuni
na Mkataba.
Lakini,
Sheria, Kanuni na Mkataba havina sehemu inayoeleza juu ya mafuta
yaliyofika, yakapimwa na kuthibitika kuwa yako katika viwango vya ubora
unaotakiwa, yakaruhusiwa kuteremshwa, meli ikaoondoka na baadae
kutambulika kuwa mafuta yaliyo katika maghala yamechanganyika.
Suala
la ubora wa meli hushughulikiwa na TPA. Taarifa za meli inayotakiwa
kuleta mafuta hutumwa TPA ambao huthibitisha kama meli hiyo inaruhusiwa
au hairuhusiwi kuingia katika bandari zetu zinazotumika kuteremsha
mafuta.
Hitimisho,
ni vyema ikafahamika kuwa utaratibu wa uagizaji mafuta kwa pamoja hapa
nchini umeanza tangu 2011. Utaratibu huu umekuwa na mafanikio makubwa,
hasa ikizingatiwa kuwa umejengwa katika misingi ya uwazi na
ushirikishwaji.
Nchi
nyingi za Afrika zimekuwa zikifika kujifunza kwetu. Aidha, hata taasisi
zingine ndani ya nchi yetu ziko katika kutekeleza manunuzi yao kwa
kutumia utaratibu unaotumiwa na PBPA. Hii ni baada ya kujifunza kutoka
PBPA. Hii inaonesha ni kwa kiasi gani wadau mbali mbali wanaona
mafanikio ya utaratibu huu.
PBPA
inapenda kuufahamisha umma kuwa itaendelea kusimamia uagizaji wa mafuta
kwa pamoja kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu. Shughuli hizi
zitafanywa kwa uwazi zaidi na kushirikisha wadau wote wanaohusika.
Tutabuni njia mbali mbali ili kuwezesha makampuni ya Watanzania kuweza
kushiriki katika biashara ya mafuta. Tunaamini kuwa tutaungwa mkono na
watu wote ili kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Imetolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)
DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment