1.0 UTANGULIZI
Kumekuwepo
na taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya
habari, hasa gazeti la Jamboleo toleo namba 2541 la 23 Agosti, 2016
kuhusu Bodi ya Mikopo kuwadai wasionufaika na mikopo. Taarifa hizi
zinalenga kuleta hofu na mkanganyiko usiokuwa wa lazima kwa wadau.
Kufuatia hatua hiyo Bodi ya Mikopo inapenda kutoa ufafanuzi wa suala
hili kama ifuatavyo:-
2.0 MADAI KUHUSU KUDAIWA MIKOPO KWA WALE WASIONUFAIKA
Bodi
ya Mikopo inapenda kuufahamisha Umma kuwa ‘database’ yake ya wanufaika
wa mikopo ina taarifa zote muhimu zilizo sahihi. Hii inatokana na
utunzaji mzuri wa kumbukumbu za ukopeshaji kuanzia hatua ya utoaji
mikopo (loan allocation and disbursement) hadi urejeshaji wake (loan
repayment). Kutokana hamasa na elimu inayotolewa, kumekuwepo na
mwitikio mkubwa wa wanufaika wa mikopo na waajiri wao kujitokeza na
kuanza kurejesha mikopo. Hivyo, katika utekelezaji wa jukumu hilo,
tumebaini kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadaiwa kwamba ama
hawakuwahi kukopa au hawajawahi kufikia kiwango cha elimu ya juu.
Hadi
sasa, imebainika kuwepo kwa baadhi ya wanufaika ambao wanadai hawakujua
iwapo fedha walizopatiwa na serikali wakati huo zilikuwa za mkopo. Pia
kuna wachache ambao vyeti vyao vilitumiwa na ndugu zao kwa ajili ya
masomo ya elimu ya juu. Katika hali hii, mdaiwa atalazimika kumtaja mtu
halisi anayepaswa kukatwa deni hilo ili Bodi iweze kusitisha makato hayo
kwake.
Ili kupata ufumbuzi wa malalamiko hayo, Bodi inawataka walalamikaji kuzingatia yafuatayo:
2.1
Kwa mtu anayedai kwamba hajasoma elimu ya juu kwa ufadhili wa serikali
au Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu; mtu huyu awasilishe
vielelezo vinavyodhihirisha kuwa hakusomeshwa kwa ufadhili wa serikali.
2.2
Kwa mtu anayedai amekatwa mshahara ingawa hajawahi kufikia kiwango cha
elimu ya juu; mtu huyo anapaswa kuwasilisha vielelezo vya kiwango cha
elimu yake.
2.3
Iwapo kuna mnufaika wa mkopo anadai amekatwa zaidi ya kiwango cha mkopo
anaodaiwa; mnufaika huyo anapaswa kuwasilisha vielelezo
vinavyothibitisha kumaliza kurejesha deni lake. Itakapothibitika kuwa
kuna makato zaidi yalifanyika, basi kiasi kilichozidi kitarejeshwa kwa
mhusika.
3.0 HITIMISHO
Bodi
inapenda kuwahakikishia wadau wake kuwa imetunza vizuri taarifa zote
muhimu za wanufaika wa mikopo ambazo ndizo zinazotumika kwenye zoezi la
urejeshaji wa mikopo. Kasoro ndogo ndogo zinazojitokeza zinatatuliwa
kwa kufanya rejea kwenye kumbukumbu zilizopo.
Aidha,
Bodi inaendelea kuwahimiza wanufaika wote wa mikopo ambao hawajaanza
kurejesha mikopo yao kuhakikisha wanawasilisha taaifa zao ofisi za Bodi
au wanajaza taarifa zao kweye fomu ‘Loan Inquiry Form’ iliyopo kwenye
tovuti ya Bodi na kuituma kwa anuani ya barua pepe info@heslb.go.tz ili
kila mmoja ajulishwe deni lake na kuanza kurejesha.
Kwa
mnufaika anayetaka kuanza kurejesha mkopo wake baada ya kuwa amepata
taarifa ya deni lake; aweke fedha kwenye akaunti za Benki zifuatazo na
kisha kuwasilisha hati ya malipo:
A/C No. 2011100205 – NMB
A/C No. 01J1028467503 – CRDB
A/C No. CCA0240000032 – TPB
Imetolewa na:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Agosti 24, 2016
0 comments:
Post a Comment